Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa, shirika hilo limeonya kuwa tukio hilo linahatarisha shughuli muhimu za kibinadamu zinazotoa maji safi kwa mamia ya maelfu ya watu Gaza.

Tunalaani vikali tukio hili:UNICEF

“UNICEF imesikitishwa na kuuawa kwa madereva wawili wa malori waliokuwa wamepewa kandarasi na UNICEF kutoa maji safi kwa familia katika Ukanda wa Gaza,” shirika hilo lilisema katika taarifa yake.

Wanaume hao wawili waliuawa kwa risasi za Israel mapema Ijumaa katika kituo cha kujazia maji cha Mansoura kaskazini mwa Gaza, tukio lililosababisha pia watu wengine wawili kujeruhiwa.

UNICEF imesema shambulio hilo lilitokea wakati wa shughuli za kawaida za usambazaji maji, bila mabadiliko yoyote ya mienendo au taratibu.

Eneo la Mansoura kwa sasa ndilo kituo pekee kinachofanya kazi cha kujazia malori maji kutoka kwenye mfumo wa maji wa Mekorot unaohudumia Gaza City. Hutumiwa mara kadhaa kila siku na UNICEF pamoja na washirika wa kibinadamu kuendeleza usambazaji muhimu wa maji kwa sehemu kubwa ya wakazi, wakiwemo watoto.

Shughuli zasitishwa kwa muda

Kufuatia tukio hilo, UNICEF imesema wakandarasi wake wameelekezwa kusitisha shughuli katika eneo hilo hadi hali ya usalama itakapoimarika.

Shirika hilo limetoa wito kwa mamlaka za Israel “kufanya uchunguzi wa haraka wa tukio hili na kuhakikisha uwajibikaji kamili,” likisisitiza kuwa “wahudumu wa kibinadamu, watoa huduma muhimu, pamoja na miundombinu ya kiraia, ikiwemo vituo muhimu vya maji, havipaswi kamwe kulengwa.”

Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa “Ulinzi wa raia na wale wanaotoa msaada wa kuokoa maisha ni wajibu chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *