
Baraza la Juu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) limesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kusimamia na kudhibiti trafiki yote inayopita katika Lango Bahari la Hormuz, ambalo ni njia ya kimkakati, hadi kufikiwa mapatano kamili ya kumaliza vita vya kulazimishwa vya Marekani na Israel dhidi ya nchi hii.
Sekretarieti ya Baraza la Juu la Usalama wa Taifa ilitoa taarifa siku ya Jumamosi kuhusu hali ya mazungumzo ya Iran na Marekani, yanayofanyika kwa upatanishi wa Pakistan, yanayolenga kumaliza vita vinavyoendelea, ambavyo kwa sasa vimesimamishwa kwa muda baada ya kusitishwa kwa mapigano kutangazwa tarehe 8 Aprili.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yanatarajiwa kuisha siku ya Jumatano. Duru ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika Islamabad haikuzaa makubaliano, huku maafisa wa Iran wakiilaumu Marekani kwa kuwasilisha madai makubwa kupita kiasi na kubadilisha msimamo wake mezani wakati wa majadiliano.
Mojawapo ya hoja zilizokwama ilikuwa udhibiti wa Iran juu ya Lango Bahari la Hormuz, ambalo Jamhuri ya Kiislamu iliufunga kwa meli za maadui pamoja na washirika wao muda mfupi baada ya vita kuanza tarehe 28 Februari.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba meli za kivita za Marekani katika Ghuba ya Uajemi hupitia Lango Bahari la Hormuz jambo ambalo Iran inaliona kuwa tishio kwa usalama wake wa taifa na uthabiti wa eneo.
Sekretarieti ya Baraza la Juu la Usalama wa Taifa pia imesisitiza kwamba Iran ilikuwa imefunga tena kwa masharti Lango Bahari la Hormuz kwa usafiri wa kibiashara siku ya Ijumaa, baada ya Marekani na utawala wa Israel kukubali kusitisha uhasama katika maeneo yote ya mapigano, ikiwa ni pamoja na kusimamisha mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, jambo ambalo lilikuwa sharti muhimu kwa Iran kukubali usitishaji wa mapigano wa muda.
Aidha taarifa hiyo imesema Iran itatekeleza hatua za kukusanya taarifa kamili za meli zote zinazopita, kutoa vibali vya kupita kulingana na kanuni zilizowekwa mahsusi kwa mazingira ya wakati wa vita, kukusanya ada za huduma za ulinzi, usalama na ulinzi wa mazingira, pamoja na kuweka njia maalumu za kuongozea meli, taarifa hiyo ilisema.
Aidha taarifa hiyo mesema: “Tukio lolote ambapo adui atajaribu kuvuruga usafirishaji baharini au kutekeleza hatua kama vile mzingiro wa kijeshi baharini, litatambuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, na hivyo itasitisha mara moja ufunguzi wa masharti na wa kiwango kidogo wa Lango Bahari la Hormuz.”
Jamhuri ya Kiislamu ilikubali rasmi kuanza mazungumzo siku ya arobaini ya vita, baada ya rais wa Marekani kukubali rasmi mpango wa vipengele kumi wa Iran kuwa msingi wa mazungumzo, taarifa hiyo ilieleza.
Hata hivyo, licha ya Washington kukubali mpango huo wa vipengele kumi kabla ya mazungumzo kuanza, ilianzisha “madai mapya na ya kupindukia” wakati wa majadiliano, jambo ambalo lilijibiwa kwa msimamo thabiti na ujumbe wa Iran.