Mazungumzo hayo yalifanyika Aprili 13 hadi 18 chini ya Mchakato wa Doha, yakiratibiwa na serikali ya Qatar kwa kushirikiana na Marekani, Muungano wa Afrika AU, na serikali ya Uswisi.
“Maendeleo kuelekea kusainiwa kwa Itifaki ya Upatikanaji wa Misaada ya Kibinadamu na Ulinzi wa Kisheria ni hatua muhimu,” imesema MONUSCO, ikiwasihi wahusika “kuharakisha makubaliano ili kupunguza mateso ya raia.”
Ahadi za misaada ya kibinadamu na ulinzi wa raia
MONUSCO imebainisha ahadi za pande zote kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu “kwa haraka, salama na bila vikwazo,” kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
“Ulinzi wa raia, hasa wanawake na watoto, lazima uwe kipaumbele,” imesisitiza.
Pia imekaribisha jitihada za kulinda maisha na miundombinu, ikisema ni muhimu kwa kuimarisha haki za msingi na kufufua uchumi wa jamii zilizoathiriwa.
Walinda amani wa MONUSCO wakiwa kwenye doria mashariki mwa DR Congo
Hatua za kujenga imani zaimarika
Ujumbe huo umesifu hatua za kujenga imani, ikiwa ni pamoja na kubadilishana wafungwa kwa msaada wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).
Pia umetambua kutiwa saini kwa makubaliano kati ya pande husika na Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), vinayowezesha utekelezaji wa mfumo wa EJVM+.
“Hatua hizi ni muhimu katika kujenga imani na kuendeleza mazungumzo,” MONUSCO imesema.
Ufuatiliaji wa usitishaji mapigano waonekana muhimu
MONUSCO imesisitiza umuhimu wa mfumo madhubuti wa kufuatilia usitishaji mapigano.
“Mfumo wa uwazi na unaofanya kazi ni muhimu kupunguza vurugu na kulinda raia,” imesema MONUSCO.
Hata hivyo, imebainisha kuwa mafanikio yatategemea masharti kama “kusitishwa kwa matumizi ya ndege za kivita zisizo na rubani, kukomesha kuvuruga GPS, na uhuru kamili wa harakati kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa”.
Watu wanaendelea kukimbia ghasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Wito wa kuendeleza mafanikio
MONUSCO imehimiza pande zote kugeuza mafanikio ya mazungumzo kuwa matokeo halisi.
“Kasi ya sasa lazima ilete matokeo yanayoonekana kwa wananchi wanaoathirika na mzozo,” ilisema.
Pia imetoa wito wa kuendelea na mazungumzo ili kufikia amani ya kudumu mashariki mwa DRC.