Dar es Salaam. Ukuaji wa teknolojia umetajwa kama kichocheo kikuu katika kuleta mapinduzi katika uhifadhi wa nyaraka na taarifa kutoka kutumia makaratasi hadi mifumo ya kompyuta.

Hayo yameelezwa leo Aprili 18,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Top Archive, Paul Muhato wakati wa hafla ya kusheherekea taasisi hiyo kupata ithibati ya kimataifa ya mfumo wa usimamizi wa mwendelezo wa biashara.

Muhato amesema awali utunzaji wa nyaraka ulitegemea zaidi makaratasi, Hata hivyo, ujio wa mifumo ya kisasa kama umebadilisha kabisa hali hiyo kwa kuwezesha nyaraka kuhifadhiwa kidijitali.

Amesema mifumo hiyo ya kidigitali imesaidia kurahisisha utendaji, kuokoa muda na gharama.

Muhato ametoa wito kwa Serikali na kampuni binafsi kuweka nyaraka zao kwenye mifumo ya kompyuta badala ya kutumia makaratasi kwa kuwa yanachelewesha utendaji wao wa kazi za kila siku.

Muhato amesema kampuni hizo zikihifadhi nyaraka zao kidigitali, itawarahisishia utendaji wao wa kazi na itasaidia kupunguza gharama kutokana na karatasi wanazotumia kuhifadhi nyaraka mbalimbali na itarahisisha utendaji wao wa kazi.

Katika hatua nyingine Muhato amesema taasisi hiyo kupata ithibati na cheti cha kimataifa cha ISO 22301:2019 cha Mfumo wa Usimamizi wa Uendelevu wa Biashara (BCMS) ni hatua kubwa inayoonesha uimara na utayari wao katika kukabiliana na changamoto za kiutendaji. 

Pia inaiweka taasisi hiyo katika ramani ya kimataifa, ikidhibitisha uwezo wake wa kuhimili changamoto mbalimbali na kuhakikisha huduma kwa wateja haziingiliwi na majanga ya kiteknolojia au dharura nyinginezo.

“Katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi, taasisi hupimwa kwa namna inavyoweza kukabiliana na changamoto na kuendelea kutoa huduma bila kukatika,”amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *