Katika taarifa iliyotolewa tarehe leo Jumanne 21 Aprili 2026 mjini Geneva na Khartoum, viongozi wa IOM akiwemo Naibu Mkurugenzi Mkuu SungAh Lee wamesema licha ya matumaini yanayoambatana na kurejea kwa wananchi hao, hali halisi katika maeneo mengi bado ni tete na inahatarisha mafanikio ya juhudi hizo.

Wanaorejea wakikabiliwa na hali ngumu

IOM imeeleza kuwa wengi wa wanaorejea wanakuta mazingira yaliyoharibiwa vibaya na vita, ikiwemo makazi, hospitali, mifumo ya maji na umeme. 

Hali hiyo inafanya maisha kuwa magumu na kuongeza hatari ya watu kulazimika kukimbia tena.

Takwimu zinaonesha kuwa tangu kuanza kwa mgogoro huo, karibu watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku zaidi ya milioni nne wakikimbilia nchi jirani na takribani milioni tisa wakiendelea kuwa wakimbizi wa ndani.

Familia zilizohamishwa kutoka Kordofan huosha nguo katika kituo cha mapokezi kinachoungwa mkono na UNICEF katika Jimbo la Gedaref, Sudan, wakati wa mapigano yanayoendelea.

© UNICEF/Osman Saif

Familia za wakimbizi kutoka Kordofan wanaosha nguo katika kituo cha mapokezi katika Jimbo la Gedaref nchini Sudan.

Shinikizo laongezeka kwa jamii zinazowapokea

Kwa mujibu wa shirika hilo, kurejea kwa idadi kubwa ya watu kumeongeza shinikizo kwa jamii zinazowapokea, hasa katika majimbo ya Kassala, Gedaref na mji mkuu Khartoum, ambako miundombinu ya kijamii na kiuchumi imeharibika kwa kiasi kikubwa.

Aidha, katika jimbo la Al Jazirah, ambalo ni kitovu muhimu cha uzalishaji wa kilimo, uharibifu wa mifumo ya uzalishaji unaendelea kutishia uhakika wa chakula na ustawi wa kiuchumi wa wakazi.

Uhitaji wa uwekezaji wa haraka

IOM imesisitiza kuwa kurejea kwa wakimbizi na uhamaji wa ndani ni masuala yanayohusiana kwa karibu, hivyo yanahitaji mipango jumuishi na uratibu wa pamoja kati ya wadau wote.

Shirika hilo linaendelea kushirikiana na serikali ya Sudan na washirika wa kibinadamu kusaidia jamii kuondoka katika utegemezi wa misaada ya dharura na kuelekea katika uokoaji na uthabiti wa muda mrefu.

Hata hivyo, mpango wa kukabiliana na mgogoro wa mwaka 2026 unakabiliwa na uungufu wa dola milioni 97.2, hali inayotishia juhudi za kusaidia mamilioni ya watu wanaohitaji msaada.

Wito wa hatua za haraka

IOM imeonya kuwa bila uwekezaji wa kutosha na ushirikiano wa kimataifa, kurejea kwa wananchi hao kunaweza kuwa cha muda mfupi na kuongeza hatari ya kurejea kwa mzunguko wa uhamaji.

Shirika hilo limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada ili kuhakikisha kuwa kurejea kwa wananchi kunakuwa salama, kunadumu na kunachangia amani na utulivu wa muda mrefu nchini Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *