
Macho na masikio ya ulimwengu yalikuwa yameelekezwa kwa karibu kwenye mvutano kati ya Iran na Marekani, baada ya pande hizo mbili kuwa katika hali ya uhasama kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Sitisho la mapigano la muda lililokuwa limekubaliwa awali lilitarajiwa kumalizika leo Jumatano tarehe 22 Aprili, hali iliyozua wasiwasi wa kurejea kwa mapigano makali.
Hata hivyo, saa chache kabla ya muda huo kuisha, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuongeza muda wa sitisho hilo bila kuweka kikomo maalum, akisema anasubiri mapendekezo ya pamoja kutoka Iran kuhusu hatua za mazungumzo ya amani. Marekani inasema imechukua uamuzi huo kufuatia ombi la Pakistan, ambayo imekuwa ikijaribu kusuluhisha mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia msemaji wake Stéphane Dujarric amesema tamko hilo la Marekani kuongeza muda wa sitisho la mapigano ni hatua muhimu katika kupunguza mvutano na kutoa nafasi kwa diplomasia pamoja na kujenga imani kati ya Iran na Marekani.
Umoja wa Mataifa umezitaka Marekani na Iran kujenga juu ya hatua hiyo, kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga sitisho hilo, na kushiriki mazungumzo kwa njia ya kujenga ili kufikia suluhu ya kudumu.
Aidha, Umoja wa Mataifa umeunga mkono juhudi za Pakistan katika kuwezesha mazungumzo zaidi, ukieleza matumaini kuwa juhudi hizo zitachangia kupatikana kwa suluhu ya kina na ya kudumu ya mgogoro huo.
Hata hivyo, duru mbalimbali za habari duniani zinaripoti kuwa bado kuna tofauti kubwa kati ya Marekani na Iran kuhusu masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na mpango wa nyuklia wa Iran, udhibiti wa Mlango baharí wa Hormuz, na uhusiano wake na makundi yenye silaha katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hatma ya mazungumzo ya amani bado haijawa wazi, huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea ili kuepusha kurejea kwa vita kamili kati ya mataifa hayo mawili.
Tags: Vita, Marekani, Iran, Mlango baharí wa Hormuz, sitisho la mapigano