Chanzo cha picha, Andriy Onufriyenko/Jackyenjoyphotography via Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Je binadamu bado wanapitia mageuzi? Je, vizazi vijazo vinaweza kuwa vifupi au virefu an kuwa na sifa tofauti za kimaumbile, au kuwa na jeni tofauti?
Pamoja na maendeleo ya ustaarabu, shinikizo nyingi zilizotokana na uteuzi wa asili ambazo ziliunda jamii ya binadamu kwa maelfu ya miaka kama vile magonjwa, njaa, na mazingira magumuzimepungua kutokana na maendeleo ya tiba, kuboreshwa kwa mifumo ya usafi wa mazingira, na upatikanaji wa chakula kwa utaratibu zaidi.
Lakini Dkt. Jason Hodgson, mwanaanthropolojia wa mageuzi na mtaalamu wa jenetiki katika Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin nchini Uingereza, anasisitiza kwamba mageuzi bado yanaendelea hadi leo.
Utofauti wa binadamu
Brianna Poppiner, mwanaanthropolojia wa kale anayechunguza mageuzi ya binadamu katika Makumbusho ya Kitaifa ya Historia ya Asili ya Taasisi ya Smithsonian nchini Marekani, anasema kwamba lishe imekuwa na jukumu muhimu katika mageuzi ya binadamu wa kisasa.
“Takriban theluthi moja ya watu duniani leo wana uwezo wa kumeng’enya maziwa wanapokuwa watu wazima, ilhali kati ya miaka elfu tano hadi elfu kumi iliyopita, hakuna mtu aliyekuwa na uwezo huo. Haya ni mabadiliko ya mageuzi yaliyotokea kwa kasi kubwa sana.”
Anaongeza kuwa mabadiliko haya yalitokea baada ya wanadamu kuanza kufuga wanyama wanaotoa maziwa.
Msimu wa njaa, wale walioweza kumeng’enya maziwa, ambayo yana mafuta na protini nyingi, walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuishi na kupitisha jeni hizi kwa watoto wao, jambo lililosababisha jeni hizo kuenea kwa haraka sana, hii ni kulingana na Poppiner.
Chanzo cha picha, Sabrina Bracher via Getty Images
Wakati binadamu walipohama kutoka Afrika kwenda sehemu mbalimbali za dunia maelfu ya miaka iliyopita, walikumbana na hali tofauti za tabianchi, jambo lililosababisha kuibuka kwa mabadiliko mapya ya kimwili yaliyowasaidia kuzoea mazingira yao tofauti.
Kwa mfano, ngozi yenye rangi nyepesi ilitokea katika maeneo yenye kiwango kidogo cha mionzi jambo linalosaidia mwili kuzalisha vitamini D.
Hodgson anaeleza kwamba utofauti huu wa kikanda ulitokea “kutokana na makundi ya binadamu kutengana.Leo, tumekutana tena kwa njia mbalimbali, kupitia uhamiaji, utandawazi, na sababu nyingine.”
Hodgson anafanya utafiti kuhusu kile kinachojulikana kama “uchaguzi wa wenzi wenye kufanana” jambo analolielezea kuwa ni “mwelekeo wa viumbe kuchagua wenzi wanaofanana nao zaidi kuliko wengine.”
Chanzo cha picha, imaginima via Getty Images
Hodgson anasema kwamba uchaguzi wa wenzi wenye kufanana unaweza kuimarisha uteuzi wa asili ambao tayari unaendelea, na kusaidia kuweka sifa fulani kwa binadamu.
Watafiti wamebaini, kwa mfano, kwamba “kadri mtu anavyokuwa mrefu, ndivyo uwezekano unavyoongezeka kwamba mwenzi wake pia atakuwa mrefu.”
Anaongezea kuwa “Imeonyeshwa kwamba urefu, uzito, muundo wa uso, na sifa nyingine zinatokana kwa kuzaana katika makundi mengine jambo ambalo “hatimaye huathiri mzunguko wa jeni.”
Hodgson anasema: “Kuna mambo mengi sana yanayoathiri maendeleo ya binadamu wakati wote.”
Hali ya kuwa binadamu
Kuna baadhi ya maamuzi tunayofanya ambayo hayaathiri maendeleo ya kijenetiki.
Kwa mfano, Bobiner anasema “Ukikwenda kufanya mazoezo, ukafanya mazoezi na kujenga misuli mikubwa, hilo halimaanishi kwamba utarithisha jeni za misuli mikubwa kwa watoto wako.”
Kuanzia matibabu ya kurekebisha meno hadi upasuaji wa urembo, sasa inawezekana kubadilisha sifa nyingi katika kipindi cha maisha ya mtu mmoja, ili ziweze kuendana zaidi na mitazamo ya kijamii.
Kitaifa na kimataifa, takriban visa milioni 38 vya upasuaji na zisizo za upasuaji za urembo zilifanyika mwaka 2024, kulingana na Jumuiya ya Kimataifa ya Upasuaji wa Urembo wa Plastiki. Hii ni ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 2020.
Chanzo cha picha, GMint via Getty Images
Thomas Meilund, aliyekuwa profesa mshiriki wa bioinformatics katika Chuo Kikuu cha Aarhus nchini Denmark, anasema kwamba uwezo huu wa kubadilisha sura na mwonekano unamaanisha kuwa mwili wako hauonyeshi tena kile ambacho jeni zako zinasema unapaswa kuwa nacho.
Katika siku zijazo, mabadiliko yanaweza yasibakie tu kwenye mwonekano wa nje, kwani wanasayansi wanatumia teknolojia inayojulikana kama CRISPR kuhariri jeni za binadamu.
Teknolojia hii kimsingi hufanya kazi kama mkasi wa molekuli unaolenga sehemu maalum, kipengele kimoja hutambua sehemu lengwa ya DNA, ilhali kingine hubadilisha sehemu hiyo. Teknolojia hii imepiga hatua na tayari inatumika kutibu idadi ndogo ya magonjwa ya kijenetiki, kama baadhi ya matatizo ya damu.
Ikiwa itaendelea kukua na kupatikana kwa wingi, siku moja inaweza kubadilisha sifa nyingi za binadamu katika kiwango cha kijeni, na kubadilisha kizazi cha mtu.
Iwapo mabadiliko haya yatafanywa kwenye seli za uzazi yaani zile zinazotengeneza mbegu za kiume au za kike, mabadiliko hayo ya kijeni yanaweza pia kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Hata hivyo, wanasayansi bado wako mbali na uwezo wa kufanya hili kwa usalama na matokeo yaliyo hakikishwa, na teknolojia hii inaleta masuala mengi ya kimaadili, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuzalisha kile kinachoitwa “watoto waliobuniwa kijeni”, pamoja na kuendeleza unyanyapaa unaohusishwa na ulemavu, na masuala mengine mengi.
Chanzo cha picha, Just_Super via Getty Images
Hodgson anasema,”Kuna makubaliano ya ulimwengu mzima leo kwamba hili si jambo linaloweza kutumika kwa binadamu, na ni kinyume kabisa na maadili.”
Ikiwa teknolojia hii itapatikana kwa wingi, inaweza hata kuwapa wazazi chaguo la kuamua mwonekano wa watoto wao kwa kubadilisha jeni ili kuchagua sifa zinazotamanika.
Aina mpya?
Mailund anasema ni vigumu kutabiri jinsi wanadamu watakavyoonekana katika siku zijazo bila kujua jinsi mazingira yetu yatakavyobadilika.
Na kama tunazungumzia mustakabali wa mbali sana, huenda hata tukabadilika na kuwa spishi mpya kabisa.
Miaka milioni moja iliyopita, spishi za binadamu kama Homo erectus zilikuwa zikitembea duniani. Spishi yetu ya sasa, Homo sapiens, ilijitokeza takriban miaka 300,000 iliyopita tu.
“Kwa hiyo, subiri miaka milioni moja, na vizazi vyetu watakuwa wametofautiana nasi kwa kiwango cha mageuzi kama ambacho Homo erectus anatofautiana nasi leo,” anasema Mailland.
Chanzo cha picha, 3quarks/Stocktrek Images via Getty Images
Hata hivyo, anaonya kwamba tofauti kati ya spishi zinaweza kuwa si za wazi kama tunavyofikiri.
Pia inawezekana kwamba spishi yetu inaweza kugawanyika mara mbili, ikiwa baadhi yetu, kwa mfano, tutahamia mazingira mapya kama vile angani.