
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu, amesisitiza uzito wa hali hii kwa kusema, “kazi hii inaonesha jinsi joto kali lilivyo hatari kubwa inayoongezeka, likiweka shinikizo linalopanda kwenye mazao, mifugo, uvuvi na misitu, na kwenye jamii na uchumi unaozitegemea.”
Athari kwa mimea, wanyama na binadamu
Ripoti hiyo iliyopewa jina ‘Extreme heat and agriculture’, yaani ‘joto la kupita kiasi na kilimo’ imeonesha kuwa viumbe kama kuku na nguruwe huanza kupata msongo wa joto pale joto linapozidi nyuzi 25, huku mazao mengi kama viazi yakianza kunyauka joto linapovuka nyuzi 30.
Kuhusu viumbe wa majini, samaki wamekuwa wakikabiliwa na hitilafu ya mfumo wa moyo wanaposhindwa kupumua vizuri kwenye maji yenye joto kali yanayopunguza hewa safi ya oksijeni. Katika hali ya kushtusha, ripoti imebainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya bahari kote duniani imeshuhudia angalau wimbi moja la joto la baharini mwaka 2025, jambo ambalo limeathiri vibaya sekta ya uvuvi na kutishia upatikanaji wa chakula kwa kila mwanadamu duniani hivi sasa.
Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, ameelezea hali hiyo akisema, “joto kali linazidi kubainisha mazingira ambayo mifumo ya chakula inafanyia kazi. Zaidi ya kuwa tu janga la tabianchi lililojitenga, linafanya kazi kama sababu inayozidisha hatari na kukuza udhaifu uliopo kwenye mifumo ya kilimo”.
Mbinu za kukabiliana na joto kali
Ili kunusuru sekta hii, wataalamu wameshauri kuanza kutumia mbegu zinazostahimili ukame na kubadilisha muda wa kupanda kulingana na mabadiliko ya msimu. Bi. Saulo ameongeza kuwa, “tahadhari za mapema na huduma za hali ya hewa kama utabiri wa msimu ni muhimu sana kutusaidia kuzoea ukweli huu mpya.”
Ripoti imehimiza umuhimu wa mifumo ya tahadhari ili kuwasaidia wakulima kujiandaa kabla ya majanga ya joto na ukame wa ghafla kutokea, hasa katika maeneo ya Afrika na Asia ambako joto kali limekuwa likizuia wafanyakazi wa kilimo kufanya kazi zao vizuri.
Mapendekezo muhimu ya sera
Upatikanaji wa huduma za kifedha kama bima na mikopo ya dharura umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kuwasaidia wakulima wadogo kuhimili majanga haya ya mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano wa kimataifa umekuwa hitaji la lazima katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambao ndio chanzo kikuu cha kupanda kwa joto hili duniani.
Ripoti inasema, “Kulinda mustakabali wa kilimo na kuhakikisha uhakika wa chakula duniani kutahitaji si tu kujenga mnepo mashambani, bali pia kutekeleza mshikamano wa kimataifa na utashi wa kisiasa wa kugawana hatari.”