
Video ya WFP na FAO inaanza katika eneo la Kalobeyei, Kakuma, ikimuonesha Afisa Mawasiliano wa WFP Kenya, Mercy Juma, akiwa ndani ya shamba lililojaa mazao ya kijani kibichi yenye kustawi na mboga mbalimbali zilizopevuka vizuri.
“Nipo hapa Kalobeyei, Kakuma, ndani ya shamba hili la ajabu la kilimo endelevu au greenhoouse. Tazameni tu hii! Hii si kilimo tu,hii ni matumaini, ni ustahimilivu. Wakimbizi pamoja na jamii wenyeji wanazalisha chakula kwa pamoja kwa msaada wa WFP na FAO.”
Aidha, video hiyo inamuonesha mkulima Neema Agwe, mkimbizi aliyepata ujuzi wa kilimo akiwa kambini.
“Nimeishi Kakuma kwa takribani miaka 8 au 9. Nikiwa nchini Kongo sikuwa mkulima. Nilijifunza kilimo nikiwa hapa. Tulitegemea kabisa msaada wa chakula, lakini ilibidi tutafute njia za kujitegemea zaidi. Ninachopanda hapa kinailisha familia yangu, na ninaweza kuweka akiba ya sehemu ya fedha ninayopokea.”
Mandhari inaonesha wakulima wakifanya kazi mashambani, kwa ushirikiano, wakulima wengine wanapanda mazao ya nyanya, bamia, vitunguu na mboga za majani.
Neema anaeleza umuhimu wa mazao hayo kwa lishe ya familia:
“Kunde ni nzuri sana; huongeza damu na kuboresha lishe kwa watoto. Mchicha na mboga nyingine pia husaidia watoto kukua wakiwa na afya njema. Ninapanda kunde, bamia, viazi vitamu na muhogo. Mboga zinapokuwa tayari, wafanyabiashara huja kuzinunua.”
Mpango huu umeleta mabadiliko makubwa, si tu kwa wakimbizi bali pia kwa jamii zinazowazunguka, kwa kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato.
Mpango huu unaoungwa mkono na Muungano wa Ulaya pamoja na serikali ya Kaunti ya Turkana unatekelezwa katika mojawapo ya maeneo yenye joto kali na ukame zaidi nchini Kenya—Turkana na unaonesha mafanikio.
Katika msimu mmoja tu, mashamba ya bustani ya Kalobeyei, Nalingangor na Elelea kwa pamoja huzalisha zaidi ya kilo milioni 1 za mboga, na kuingiza zaidi ya dola laki moja.
Uwekezaji katika kilimo na lishe unaweza kubadilisha maisha ya wakimbizi kutoka utegemezi wa misaada hadi kujitegemea na kujenga jamii imara.