Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa Jorge Moreira da Silva, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Miradi na Huduma (UNOPS) na mkuu wa kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa katika Mlango bahari wa Hormuz, amesema usumbufu wa usafiri katika eneo hilo tayari unaathiri mnyororo wa usambazaji wa mbolea duniani.

Ameeleza kuwa takribani theluthi moja ya biashara ya mbolea duniani hupita katika mlango huo wa bahari, na kwamba kuchelewa kwa malighafi za mbolea kama urea, amonia na salfa kunaathiri moja kwa moja uzalishaji wa kilimo, hali inayoweza kusababisha uhaba wa chakula na kuongezeka kwa njaa.

UN yachukua hatua

Katika kukabiliana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tayari ameunda kikosi kazi cha kuandaa mfumo maalum wa kurahisisha usafirishaji wa mbolea na malighafi zake, ukijikita katika kujenga uaminifu kupitia usajili, uratibu, ufuatiliaji na uhakiki.

Da Silva amesema mfumo huo unaweza kuanza kufanya kazi ndani ya siku saba endapo kutakuwa na ridhaa ya kisiasa, akisisitiza kuwa changamoto kubwa si rasilimali bali ni nia ya kisiasa ya kuutekeleza. “Hatuwezi kusubiri hadi kila kitu kitatuliwe ndipo tuchukue hatua, wakati msimu wa kilimo tayari umeanza,” amesema.

Ameonya kuwa kuchelewa kuchukua hatua kunaweza kuongeza hatari ya njaa duniani, huku makadirio yakionesha kuwa watu milioni 45 zaidi wanaweza kukumbwa na ukosefu wa chakula iwapo usumbufu huo utaendelea. 

Mkuu huyo wa UNOPS amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuanza utekelezaji mara moja endapo kutakuwa na makubaliano, ili kuzuia kuongezeka kwa mgogoro wa chakula duniani.

Pia amebainisha kuwa uzoefu uliopo katika mifumo mingine kama ule wa usafirishaji wa nafaka katika Bahari Nyeusi unaweza kusaidia kuzuia kuongezeka kwa njaa na kulinda uhakika wa upatikanaji wa chakula duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *