MASHINDANO ya Kombe la Muungano yanaendelea tena leo Alhamisi ambapo kutakuwa na mechi mbili kubwa zikihusisha Simba na Singida Black Stars zitakazokuwa na hesabu zinazoweza kuwakutanisha baadaye.

Mchezo wa mapema utakaotangulia itakuwa ni Singida Black Stars itakayokutana na Mlandege kwenye mchezo wa tatu wa robo fainali, kuanzia saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Amaan hapa Zanzibar.

Singida ambayo ilitua hapa Zanzibar juzi, imekuja na wachezaji 27 kwenye mashindano haya wakilenga kuwa na silaha zao zote, ambapo itawakosa mshambuliaji Elvis Rupia, viungo Marouf Tchakei na Habib Gego ambao ni majeruhi.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Desemba 28, 2025 kwenye Kombe la Mapinduzi na Singida ilishinda kwa mabao 3-1 kisiwani hapa. Kocha wa Singida, Muhibu Kanu akizungumzia mchezo huo, alisema wamejipanga kumaliza mapema mechi hiyo, kutafuta ushindi ndani ya dakika 90 na kwamba hawataki kusubiri hatua ya matuta kujua mshindi.

“Tumejiandaa vizuri na tuko sawa, tumekuja na kila mchezaji hapa kwa ajili ya kuhakikisha tunafanikiwa, hesabu zetu ni kushinda hii mechi ingawa tunatambua tunakutana na timu ngumu lakini kitu ambacho tumekiweka vichwani ni kuimaliza mechi ndani ya dakika 90,” alisema Kanu.

Wakati Kanu akiyasema hayo, Mlandege imewaita mashabiki wake huku ikitamba kwamba haitaki kurudia makosa na kwamba watafurahi wakifika uwanjani.

Kocha msaidizi wa Mlandege, Mohammed Abdallah, akizungumzia mchezo huo alisema kila kitu kuhusu maandalizi ya mchezo huo kimekamilika ambapo kilichosalia ni wachezaji wake kwenda kufanya kweli.

“Tumekamilisha maandalizi yetu leo (jana) asubuhi tayari kwa kukutana na Singida, tunatambua kwamba tunakwenda kukutana na timu nzuri yenye wachezaji wengi wa kigeni lakini maandalizi yetu ndiyo yatakayowapa ushindi,” alisema Abdallah.

Baada ya mchezo huo, usiku wake Simba ambayo jana mchana ilifika Zanzibar, itashuka uwanja huohuo kwa mchezo wa nne wa robo fainali ikikutana na Mafunzo ya hapa Zanzibar.

Simba imeshuka Zanzibar na mziki wake kamili na kama haitoshi ikamuongeza kiungo wake aliyekuwa majeruhi Mohammed Bajaber akipewa mechi hizo kuangaliwa juu ya kupona kwake.

Hesabu za Simba kulingana na alichokisema kocha wao, Steve Barker ni kwamba hawataki masihara katika mashindano hayo na kwamba wanalitaka taji hilo kwenye kabati la mataji.

Kocha Barker kwenye hesabu zake alishatangaza kwamba atakuwa na mzunguko mdogo wa wachezaji (rotation) lakini wenye kulenga kulihitaji taji hilo ambalo kama wekundu hao watafanya kweli linaweza kuwa la kwanza kwao msimu huu. Simba mara ya mwisho kubeba Kombe la Muungano ilikuwa mwaka 2024 chini ya kocha Abdelhack Benchikha, kisha 2025 Yanga ikabeba, huku msimu huu Barker ana kazi ya kulibeba tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *