Kati ya Desemba na Februari mwaka huu, operesheni zilizohusisha Kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa cha kudhibiti magenge ya uhalifu zilisababisha vifo vya washukiwa 1,343 wa magenge ya uhalifu.
Hata hivyo, wanadiplomasia wanasema gharama ya kibinadamu inaendelea kuwa kubwa, huku raia wakibeba mzigo mkubwa wa mgogoro huo.
Carlos Ruiz Massieu, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kwa Haiti na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, anatoa taarifa kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu suala linalohusu nchi hiyo.
Haiti katika wakati muhimu
Akilihutubia Baraza hilo, Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa Haiti BINUH, Carlos Ruiz Massieu amesema nchi hiyo iko katika hatua nyeti ya mabadiliko.
“Haiti ipo katika wakati muhimu sana,” amesema, akisisitiza kuwa hatua za kisiasa na taasisi zilizochukuliwa zinaweka msingi wa njia ya kusonga mbele yenye matumaini.
Ameeleza kuwa uhamishaji wa mamlaka ya kiutendaji mwezi Februari ulikuwa hatua muhimu ya kuhakikisha mwendelezo wa serikali katika kipindi cha udhaifu mkubwa.
Uchaguzi ndio njia pekee ya kurejea utawala wa kikatiba
Massieu amesisitiza kuwa kurejea kwa utawala wa kikatiba kunategemea kufanyika kwa uchaguzi huru na wa kuaminika.
“Wadau wa Haiti wako wazi, uchaguzi ndio njia pekee halali ya kurejea katika utawala wa kikatiba,” alisema.
Ameongeza kuwa Mkataba wa Kitaifa wa Utulivu na Uandaaji wa Uchaguzi, uliosainiwa na makundi ya kisiasa na kiraia, unaonesha dhamira ya pamoja ya kuiongoza nchi katika kipindi cha mpito.
Mtoto akipokea matibabu katika kliniki tembezi ya UNICEF kwa familia zilizofurushwa na vita huko Boucan Carré, Haiti
Mafanikio yapo lakini hali bado tete
Licha ya hatua kadhaa za mafanikio, ikiwa ni pamoja na kuboreshwa kwa usalama katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu Port-au-Prince na kurejea kwa mikutano ya serikali katika Ikulu ya Taifa, hali bado ni tete.
“Maendeleo haya ni ya kweli lakini mazingira bado ni dhaifu,” ameonya Massieu, akisisitiza umuhimu wa mshikamano na uratibu wa juhudi za kisiasa na kiusalama.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama Ofisi ya Umoja wa Mataifa Haiti (BINUH) na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Msaada Haiti (UNSOH) yanaendelea kushirikiana na serikali ya Haiti kuimarisha utulivu.
Safari ni ndefu kuelekea utulivu
Wakati Baraza la Usalama likijadili, changamoto kubwa inasalia kuwa kusawazisha operesheni za usalama na ulinzi wa raia pamoja na kujenga upya taasisi za kidemokrasia.
Wanadiplomasia wanasema mjadala huo unaonesha ukweli mgumu, licha ya juhudi za kupambana na magenge kuongezeka, utulivu wa kudumu nchini Haiti bado uko mbali kufikiwa.
“Mshikamano, uwazi wa malengo na uratibu madhubuti ni muhimu sana,” amehitimisha taarifa yake Massieu, akitoa wito wa juhudi endelevu za kitaifa na kimataifa kusaidia Haiti kuvuka kipindi hiki kigumu.
Jack Christofides, Mwakilishi Maalum wa Kikosi cha Kuzuia Magenge, anatoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu suala la Haiti.
Operesheni ya kudhibiti magenge Haiti yafikia hatua muhimu: Christofides
Jack Christofides Mwakilishi Maalum kwa ajili ya Kikosi cha Kudhibii Magenge Haiti amesema kuwa mchakayo wa kuanzishwa kwa Kikosi cha Kudhibiti Magenge (GSF) upo katika hatua muhimu ya awali.
“Tunaelewa kwa kina mateso wanayopitia wananchi wa Haiti, hasa wale wanaoishi chini ya udhibiti wa magenge,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa GSF inajengwa kama “kikosi chenye nidhamu, kinachowajibika na kinachotegemea ushirikiano,” kikiwa na lengo la kutoa matokeo mahususi ya kiusalama huku kikizingatia viwango vya juu vya maadili na kuheshimu kikamilifu mamlaka ya Haiti.
Mpango wa utekelezaji tayari umeandaliwa kwa kushirikiana na mamlaka za Haiti, ukilenga maeneo ya kipaumbele na kutumia uwezo maalum wa vikosi vinavyoshiriki.
“Lengo ni bayana, kupunguza uwezo wa magenge hadi kiwango ambacho taasisi za Haiti zinaweza kudhibiti kwa uendelevu,” almeafanua.