
Manchester City imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuichapa Burnley, lakini ushindi huo haukumridhisha kocha Pep Guardiola kufuatia wachezaji wake kupoteza nafasi nyingi za wazi.
Ushindi huo umeifanya City kuendelea kujisogeza taratibu katika mbio za ubingwa, huku wapinzani wao wa karibu Arsenal wakibaki nyuma kwa tofauti ndogo sana. Hata hivyo, mbio za ubingwa msimu huu zinaonekana kuwa ngumu kutokana na ushindani wa timu zinazogombania ubingwa.
Kwa upande wa Burnley imerudi rasmi Ligi ya Championship baada ya leo kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Manchester City.
Burnley imeshuka daraja baada ya kucheza Ligi England kwa msimu mmoja pekee tangu ipande daraja 2024.
Timu hiyo inashika nafasi ya 19 kwenye ligi ikiwa na pointi 20 ambapo imebakiza mechi nne ambazo ikishinda zote inafikisha ponti 32 moja pungufu dhidi ya Westham United ambayo ipo nafasi ya 17 na pointi 33.
Katika mchezo huo Bao la mapema lililofungwa na Erling Haaland dakika ya tano ndilo limeifanya City kuondoka na ushindi, lakini baada ya hapo City walishindwa kutumia vyema nafasi walizozipata.
Vipindi kadhaa vya mchezo vilimuonyesha Guardiola akiwa na hasira pembeni ya uwanja, akilalamikia makosa ya wachezaji wake na upotevu wa nafasi kirahisi. Licha ya ushindi, kiwango hicho kimeacha maswali mengi katika kipindi hiki muhimu cha msimu.
Tofauti na misimu iliyopita ambapo City walikuwa na mfululizo mrefu wa ushindi, safari hii hawajaonyesha mwendelezo huo. Hadi sasa, wanaweza kufikisha pointi zisizozidi 85 idadi ndogo ukilinganisha na misimu yao ya mafanikio chini ya Guardiola.
Licha ya majaribio ya kimkakati ya Guardiola ikiwemo kubadili mifumo ya uchezaji mara kwa mara bado City wanaonekana kuwa katika kipindi cha mpito.
Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu zinaelekea kuamuliwa katika dakika za mwisho, huku kukiwa hakuna timu yenye kiashiria cha wazi cha kutwaa taji.