WAKATI ikielezwa Yanga inafanya mazungumzo ya kimya kimya na uongozi wa Wydad Casablanca ya Morocco kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, mabosi wa Simba wameweka ngumu kwa nyota huyo wakihitaji kubakia naye.
Mshambuliaji huyo anayeichezea Simba kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca, mkataba wake na kikosi hicho unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026, huku kukiwa hakuna kipengele kinachomruhusu kuongeza mwingine pindi utakapoisha.
Wakati hilo likiendelea, mabosi wa Yanga wameingilia kati na kumhitaji mshambuliaji huyo kwa ajili ya kumtumia msimu ujao, ingawa, uongozi wa Simba umeshtukia janja ya watani zao wa jadi na sasa inapambana ikiwezekana iendelee naye pia.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza mabosi wa Simba wamevutiwa na uwezo wa mshambuliaji huyo na wapo tayari kuendelea naye ikiwa waajiri wake watamtoa tena kwa mkopo, ili kuwakomoa watani zao Yanga ambao wameonyesha nia pia.
“Mkataba wake na Simba ni wa mkopo na hauna kipengele cha kuongeza mwingine, baada ya msimu kuisha Wydad itakaa chini na kuamua sehemu itakayompeleka, kuna ofa zaidi ya tatu ila hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa taarifa huyo, amesema lengo la Simba ni kuona mchezaji huyo kama hawatampata msimu ujao basi asiende kwa wapinzani wao Yanga kutokana na uwezo alionao, ingawa, hatima yake itaamuliwa na waajiri wake baada ya msimu huu kufikia mwishoni.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kwa mkataba wa miaka minne kuanzia 2025 hadi 2029 baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Fountain Gate na kabla ya kuondoka dirisha dogo la Januari 2025, aliifungia timu hiyo mabao sita ya Ligi.
Nyota huyu alijiunga na Fountain Gate akitokea Singida Black Stars iliyomsajili akitokea KVZ ya Zanzibar, ambapo msimu wa 2023-2024, alikuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 20 na kutoa asisti saba katika mechi 27, kati ya 30 alizocheza.
Usajili wa mshambuliaji huyo ndani ya kikosi hicho cha Simba, umekuwa na manufaa makubwa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, kwa sababu hadi sasa ndiye kinara wao wa mabao Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga sita.
Inaelezwa Yanga ina uhitaji wa kusajili mshambuliaji mzawa na imevutiwa na uwezo wa Mwalimu ambaye kabla ya kwenda Wydad, alifanya vizuri Fountain Gate, hivyo uzoefu wake na Ligi Kuu Bara hauna shaka.