Haya yamebainika katika ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD ambayo imebainisha kinaga ubaga jinsi nchi zinavyojenga uwezo wa uzalishaji na kwa nini maendeleo hayo bado hayalingani kati ya kanda mbalimbali duniani.

Uwezo wa uzalishaji ni nini?

Kwa mujibu wa UNCTAD, uwezo wa uzalishaji ni mchanganyiko wa rasilimali, ujuzi na mifumo ya kiuchumi inayowezesha uzalishaji wa bidhaa na huduma. Huu ndio msingi wa ukuaji wa muda mrefu, ajira na kupunguza umaskini.

Katika dunia inayokumbwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kisiasa na kuyumba kwa uchumi, nchi zenye uwezo imara wa uzalishaji zina nafasi kubwa zaidi ya kustahimili misukosuko hiyo na kuendelea kukua.

Kipimo kipya cha maendeleo ya uchumi

Ili kupima uwezo huu kwa usahihi zaidi, UNCTAD imeanzisha kielelezo cha uwezo wa zalishaji (Productive Capacities Index – PCI) hiki ni tofauti na vipimo vya kawaida kama Pato la Taifa (GDP), PCI huangazia vichocheo halisi vya maendeleo.

Kielelezo hicho hupima uwezo wa nchi kuzalisha bidhaa na huduma kupitia viashiria 43 katika maeneo nane muhimu, yakiwemo rasilimali watu, miundombinu, nishati, taasisi na sekta binafsi.

Tofauti kubwa kati ya nchi na kanda

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha pengo kubwa kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Nchi zilizoendelea zinaongoza kwa kiwango kikubwa, huku Asia na Amerika ya Kusini zikifanya vizuri zaidi kuliko Afrika miongoni mwa nchi zinazoendelea.

Barani Afrika, baadhi ya nchi zina alama chini ya 20 katika kipimo hicho, ishara ya changamoto za kimuundo zinazoendelea. Hata hivyo, nchi kama South Africa, Tunisia na Morocco zimejitokeza kwa kufanya vizuri zaidi, zikifikia wastani wa alama 49.2.

Maendeleo yapo, lakini pengo bado kubwa

Tangu mwaka 2000, nchi zinazoendelea zimepiga hatua katika kujenga uwezo wa uzalishaji, lakini pengo kati yao na nchi zilizoendelea bado ni kubwa na halionekani kufungwa haraka.

Nchi zilizo katika kundi la nchi maskini zaidi (LDCs) zimeonesha maendeleo ya polepole zaidi tangu mwaka 2016, huku nchi ndogo za visiwa nazo zikikosa kasi ya awali ya ukuaji.

Teknolojia yaongoza mabadiliko

Ukuaji wa uwezo wa uzalishaji katika nchi maskini zaidi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na maendeleo katika teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT). Hii inaonesha nafasi muhimu ya teknolojia katika kuharakisha mageuzi ya uchumi.

Hata hivyo, rasilimali asilia bado zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hizi, jambo ambalo linaweza kuwa fursa lakini pia hatari kutokana na utegemezi wa bidhaa ghafi.

Ripoti hyo imetolea mfano wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC, serikali imeahidi kuongeza uwekezaji katika kujenga uwezo wa uzalishaji kwa kushirikiana na UNCTAD. Hatua hii inalenga kubadilisha uchumi kutoka utegemezi wa rasilimali ghafi kwenda kwenye viwanda vinavyoongeza thamani.

Wito 

UNCTAD inasisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali na washirika wa maendeleo kuacha kutegemea vipimo vya kawaida kama GDP pekee, na badala yake kutumia zana pana kama PCI kupanga na kutathmini sera za maendeleo.

Lengo kuu la kufanya hivyo ni kuhakikisha wana jenga uchumi unaozalisha bidhaa zenye thamani zaidi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi hasa katika nchi za Afrika na kwingineko duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *