Shinyanga. Katika jitihada za kuimarisha uwajibikaji wa viongozi kuhusu maslahi na ushirikishwaji wa watoto, viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wamepatiwa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kuwashirikisha watoto katika vikao vya maamuzi.
Akizungumza leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO, Gerald Ng’ong’a, amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha vipaumbele na mahitaji ya watoto yanazingatiwa na kujumuishwa katika mipango ya bajeti.
Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki SDO, Gerald Ng’ong’a akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali Manispaa ya Shinyanga.
“Awali tuliwajengea uwezo watoto kupitia mabaraza yao kuhusu namna ya kushiriki katika vikao vya maamuzi. Sasa tumeelekeza nguvu kwa viongozi ili kuhakikisha wanawashirikisha watoto ipasavyo katika vikao vinavyohusu masuala yao,” amesema Ng’ong’a.
Kwa upande wake, Mratibu wa Baraza la Watoto Manispaa ya Shinyanga, Kashinje Shija, amesema mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na Save the Children yanalenga kuimarisha ushiriki wa watoto katika michakato ya maamuzi.
“Mafunzo haya yatahakikisha watoto wanashirikishwa kikamilifu katika vikao vya maamuzi, waweze kueleza vipaumbele vyao na hatimaye viingizwe katika mipango ya bajeti, hasa katika masuala yanayowahusu moja kwa moja,” amesema Shija.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kitangili, Kabula Michael, amesema baada ya mafunzo hayo wataanza kushirikisha mabaraza ya watoto katika vikao vya maamuzi ngazi ya kata, hususan wakati wa maandalizi ya mipango ya bajeti.
“Hatua hii itasaidia kubaini mahitaji halisi ya watoto na kuyajumuisha katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Michael.
Aidha, Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Gabriel Walinguzo, amesema ushirikishwaji wa watoto utasaidia kutenga bajeti inayolenga moja kwa moja mahitaji yao.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha maoni ya watoto yanazingatiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.