Asubuhi ya Septemba 11, 2001, saa 3:37 asubuhi kwa saa za Washington, ndege ya Shirika la American Airlines, Flight 77, Boeing 757 iliyokuwa imebeba watu 64 iligonga upande wa magharibi wa Pentagon.
Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kwa kasi ya takribani maili 530 kwa saa na ilikuwa imebeba galoni 5,300 za mafuta ya ndege. Kwa nguvu kubwa ya mgongano huo, ndege ilipenya ndani ya pembe tatu kati ya tano za jengo hilo.
Jumla ya watu 184 walipoteza maisha katika tukio hilo. Miongoni mwao, 125 walikuwa ndani ya Pentagon wakati wa shambulio, huku 59 waliokuwa ndani ya ndege hiyo pia walifariki dunia.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya sasa, makao makuu yenye nguvu zaidi ya kijeshi duniani yalishambuliwa si na jeshi la taifa adui, si kwa makombora ya kisasa wala mfumo wa hali ya juu wa silaha, bali kwa kutumia ndege ya kawaida ya abiria iliyotekwa nyara.
Athari za tukio hilo zilikuwa za haraka na zenye uzito mkubwa. Ikiwa Pentagon ingeweza kufikiwa na kushambuliwa kwa namna hiyo, basi baadhi ya misingi iliyokuwa imejenga imani ya Marekani kuhusu usalama wa taasisi zake muhimu ilihitaji kutathminiwa upya tangu mwanzo.
Mwonekano wa makao makuu ya Idara ya Ulinzi ya Marekani maarufu Pentagon.
Sehemu ya magharibi ya Pentagon iliyoharibiwa ilijengwa upya kwa kasi ya ajabu ndani ya kipindi cha miezi 14 pekee. Katika mchakato huo, maboresho makubwa ya kiusalama yalifanyika.
Kwa mara ya kwanza tangu Pentagon ilipojengwa miaka ya 1940, mfumo mzima wa usanifu wa usalama wa jengo ulifanyiwa mapitio makubwa.
Hata hivyo, kuelewa kinachoilinda Pentagon leo kunahitaji kutambua kwamba uimara wa kuta na miundombinu yake ni sehemu moja tu ya mfumo mpana wa ulinzi ulio na tabaka nyingi unaoenea kwa umbali mkubwa nje ya mipaka ya jengo lenyewe.
Tabaka za ulinzi
Usalama wa Pentagon unasimamiwa na Wakala wa Kulinda Usalama wa Pentagon (PFPA), taasisi maalumu ya Idara ya Ulinzi ya Marekani yenye jukumu la kulinda jengo hilo, wafanyakazi wake na miundombinu muhimu dhidi ya vitisho vya aina mbalimbali. Wakala ulianzishwa mwaka 2002.
Taasisi hiyo ina takribani wafanyakazi 1,300 ambao kazi yao kuu ni kuhakikisha usalama wa jengo hilo na maeneo yanayolizunguka.
Tofauti na vikosi vya kawaida vya polisi vinavyolinda majengo mengi ya serikali, PFPA ina uwezo wa hali ya juu unaokaribiana na ule wa taasisi za kijeshi. Maofisa wake hutumia vifaa vya kisasa vya usalama, hupata taarifa za kiintelijensia zinazohitajika kwa kazi zao na wana mamlaka ya kutumia nguvu za kiwango cha juu pale mazingira ya tishio yatahitaji hatua hizo.
Anga juu ya Pentagon
Ulinzi wa Pentagon hauishii ardhini pekee. Anga la Washington D.C ni miongoni mwa maeneo yenye masharti makali zaidi ya usafiri wa anga duniani.
Pentagon ipo ndani ya eneo maalumu la udhibiti wa ndege linalosimamiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA).
Ndege zote za kiraia zinazoruhusiwa kuruka katika ukanda huo hulazimika kufuata masharti maalumu ya njia za safari na viwango vya mwinuko vinavyoruhusiwa.
Madhara ya kukiuka masharti hayo ni ya haraka na makubwa. Tangu mwaka 2001, Kamandi ya Ulinzi wa Anga na Anga za Juu ya Amerika Kaskazini (Norad) imeendelea kuwa katika hali ya tahadhari muda wote.
Ndege za kivita zenye silaha kamili huwekwa tayari kuondoka ndani ya dakika chache pale panapobainika tishio lolote la anga.
Ngao ya kidijitali
Katika zama za sasa, changamoto kubwa zaidi Pentagon ipo ndani ya mifumo yake ya kidijitali. Kadiri teknolojia ilivyozidi kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kijeshi, ndivyo mtandao wa taarifa unavyochukua nafasi kubwa zaidi katika uendeshaji wa jeshi la Marekani.
Idara ya Ulinzi ya Marekani inaendesha mtandao mkubwa zaidi wa kompyuta duniani. Mtandao huo unahusisha zaidi ya vifaa milioni nne vya kidijitali vinavyounganishwa kupitia takribani mitandao 15,000 tofauti.
Mtandao wa Taarifa wa Idara ya Ulinzi ya Marekani (DoDIN) unaunganisha Pentagon na kila kambi ya kijeshi, ubalozi na makao ya operesheni za kijeshi za Marekani yaliyoko katika sehemu mbalimbali za dunia.
Kupitia mtandao huo, taarifa za kiintelijensia, maagizo ya kiutendaji, tathmini za usalama na mawasiliano ya kimkakati husafirishwa kwa kasi kubwa kati ya vituo mbalimbali vya mamlaka.
Kwa sababu hiyo, kulinda mtandao huo dhidi ya uvamizi, hujuma, usumbufu wa mifumo au wizi wa taarifa nyeti ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za kiusalama zinazokabili Marekani katika karne ya 21.
Wakuu wengi wa jeshi la Marekani wamekuwa wakisisitiza kwamba vita vya siku zijazo havitapiganwa kwa silaha za kawaida pekee, bali pia kupitia mashambulizi dhidi ya mifumo ya taarifa. Ndiyo maana usalama wa mtandao umepewa uzito unaokaribiana na ule wa ulinzi wa kijeshi wa jadi.
Wakala wa Mifumo ya Taarifa za Ulinzi (Disa), wenye makao karibu na Pentagon, unasimamia usalama wa kiutendaji wa mitandao hiyo.
Kamandi ya Mtandao ya Marekani iliyoanzishwa mwaka 2009 na baadaye kupewa hadhi kamili ya kamandi ya kijeshi mwaka 2018, inaendesha shughuli za ulinzi na mashambulizi ya kimtandao kutoka makao yake yaliyopo Fort Meade, Maryland.
Kwa pamoja, taasisi hizi zinaajiri maelfu ya wataalamu wa usalama wa mtandao wanaofanya kazi saa 24 kwa siku. Majukumu yao ni pamoja na kufuatilia mienendo isiyo ya kawaida katika mtandao, kubaini udhaifu wa mifumo ya kidijitali na kuurekebisha kwa wakati halisi, pamoja na kutekeleza operesheni za kimtandao dhidi ya mifumo ya wapinzani pale mamlaka husika zinaporuhusu hatua hizo.
Ukubwa wa tishio linalokabili mifumo ya Pentagon ni mkubwa kiasi cha kushangaza. Kwa mujibu wa taarifa za Idara ya Ulinzi, mitandao yake hukabiliwa na mamia ya mamilioni ya majaribio ya kuichunguza, kuipenya au kuishambulia kila siku.
Katika kukabiliana na changamoto hizi, Pentagon imejenga mkakati wa usalama unaotegemea ufuatiliaji endelevu wa mifumo yake. Imepitisha falsafa ya usalama inayojulikana Zero Trust Architecture (kutomwamini mtumiaji au kifaa chochote bila uthibitisho).
Chini ya falsafa hiyo, hakuna mtumiaji wala kifaa kinachoaminika moja kwa moja hata kama tayari kipo ndani ya mtandao. Kila ombi la kufikia taarifa au mfumo lazima lithibitishwe upya kabla ya kuruhusiwa.
Funzo baada ya mashambulizi
Mashambulizi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Pentagon yalisababisha mabadiliko makubwa ya kimuundo yaliyobadilisha kwa kina namna Marekani ilivyofikiria na kusimamia usalama wake wa taifa.
Mwaka 2004, Sheria ya Mageuzi ya Ujasusi na Kuzuia Ugaidi ilianzishwa, na kusababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Taifa wa Ujasusi. Lengo lake lilikuwa kuimarisha uratibu kati ya mashirika 17 ya ujasusi ambayo awali yalikuwa yakifanya kazi kwa kiwango kikubwa bila mfumo madhubuti wa ushirikiano.
Vilevile, mwaka 2002 iliundwa Idara ya Usalama wa Ndani wa Taifa ambayo iliunganisha majukumu mbalimbali yaliyokuwa yamesambaa katika taasisi tofauti. Ulinzi wa mipaka, usalama wa usafiri, ulinzi wa miundombinu muhimu na usimamizi wa majanga yaliwekwa chini ya mfumo mmoja wa uratibu.
Vitisho katika zama za sasa
Katika miaka ya hivi karibuni, aina ya vitisho vinavyoikabili Pentagon vimeongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyokuwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11.
Miongoni mwa changamoto mpya ni kuenea kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani zinazopatikana kwa urahisi katika soko la kawaida la kibiashara.
Teknolojia ambayo awali ilikuwa ikihitaji uwekezaji mkubwa, sasa inaweza kununuliwa kwa gharama ndogo kupitia tovuti za vifaa vya kielektroniki.
Ndege hizi ndogo zinaweza kubeba vifaa vya upelelezi, kamera za kisasa na hata vilipuzi katika matoleo yake yaliyorekebishwa kwa matumizi ya kijeshi. Migogoro ya hivi karibuni nchini Ukraine, Yemen na maeneo mengine imeonyesha wazi jinsi teknolojia hii ilivyobadilisha sura ya vita vya kisasa.
Kutokana na hali hiyo, Pentagon imeanzisha programu maalumu za kukabiliana na ndege zisizo na rubani.
Wakati huohuo, maendeleo ya silaha za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kushambulia kwa usahihi kutoka umbali mrefu yameongeza changamoto nyingine.
Leo hii, wataalamu wengi wa ulinzi wanakubaliana kwamba hakuna ukuta, uzio au eneo la usalama linaloweza kutoa uhakika wa asilimia 100 wa kuzuia shambulizi kutoka kwa mpinzani mwenye uwezo wa kisasa wa kijeshi.
Kutokana na hali hiyo, mkakati wa Pentagon umebadilika. Lengo si tena kufanya jengo lenyewe lisipenyeke kabisa, kwani matarajio hayo yanazidi kuwa magumu kufikiwa katika mazingira ya sasa ya kiteknolojia.
Kwa mantiki hiyo, usalama wa Pentagon wa karne ya 21 haupimwi tena kwa uimara wa kuta zake pekee, bali kwa uwezo wake wa kuhakikisha kuwa uongozi wa kijeshi wa Marekani unaendelea kufanya kazi katika mazingira yoyote, hata yale ambayo awali yalionekana hayawezekani kufikiriwa.
Pentagon si ngome pekee duniani inayolindwa kwa viwango vya kipekee. Katika maeneo mbalimbali duniani kuna vituo vya kijeshi ambavyo hatua zake za usalama zimezungukwa na za siri kubwa zaidi. Fuatilia toleo lijalo.