Katika taarifa iliyotolewa tarehe 22 Aprili 2026 kutoka Geneva, Washington D.C. na Nassau, WHO imesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za muda mrefu za serikali, wahudumu wa afya na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya kwa wanawake wajawazito na watoto.

Mafanikio makubwa katika afya ya mama na mtoto

Kwa mujibu wa WHO, mafanikio ya Bahamas yanaakisi dhamira thabiti ya kisiasa na uwekezaji endelevu katika sekta ya afya. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema hatua hiyo inaonesha uwezekano wa kujenga kizazi kisicho na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi au HIV.

Aidha, viongozi wa afya wa kikanda wamesema mafanikio hayo ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine katika juhudi za kutokomeza magonjwa ya kuambukiza.

Msingi wa mafanikio waelezwa

WHO imebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na mfumo jumuishi wa huduma za afya unaowezesha upatikanaji wa huduma kwa wote. Hatua muhimu zilizochangia mafanikio hayo ni pamoja na:

·         Upatikanaji wa huduma za kabla ya kujifungua kwa wanawake wote wajawazito bila ubaguzi

·         Mfumo imara wa upimaji wa HIV unaofanyika mapema na kurudiwa wakati wa ujauzito

·         Ujumuishaji wa huduma za kinga na matibabu ya HIV katika huduma za afya ya mama na mtoto

·         Matumizi ya dawa za kinga (PrEP) na matibabu ya muda mrefu kwa wanaohitaji

·         Ufuatiliaji wa karibu kwa mama wenye HIV na watoto walio katika hatari

Vigezo vya uthibitisho vya WHO

Ili kufikia hadhi hiyo, WHO imesema nchi lazima itimize vigezo maalum vya kiafya, ikiwemo:

·         Kupunguza maambukizi ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hadi chini ya asilimia 2

·         Kurekodi chini ya maambukizi mapya 5 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa hai

·         Kufikia angalau asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma za wajawazito, vipimo na matibabu

Ushirikiano wa kimataifa waonesha mafanikio

Mashirika ya kimataifa yakiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Ukimwi (UNAIDS) yamepongeza hatua hiyo, yakisema inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza.

Yamesema mafanikio ya Bahamas yanaongeza kasi ya juhudi za kikanda za kutokomeza HIV pamoja na magonjwa mengine kama kaswende na homa ya ini B. (hepatitis B).

Hatua za kuendeleza mafanikio

WHO imeeleza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya mpango mpana wa EMTCT Plus unaolenga kutokomeza maambukizi ya HIV na magonjwa mengine kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ifikapo mwaka 2030.

Shirika hilo limetoa wito kwa nchi nyingine kuimarisha uwekezaji katika mifumo ya afya na kuhakikisha huduma bora zinawafikia wanawake na watoto wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *