Dar es Salaam. Viongozi wanawake waliowania nafasi za juu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wameweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuamua kuunda jukwaa la pamoja lenye lengo la kuunganisha sauti za wanawake wenye maono na kuendeleza ajenda ya maendeleo nchini Tanzania.

Viongozi hao wameungana chini ya mwamvuli mpya unaojulikana kama Jukwaa la Wanawake Viongozi Tanzania (WLF), taasisi isiyo ya kisiasa wala ya kiserikali, ambayo imeanzishwa hivi karibuni na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi katika siku za usoni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 24, 2026, mwenyekiti wa jukwaa hilo, Dk Evaline Munisi amesema mpango huo umetokana na dhamira ya pamoja ya kuendeleza taifa licha ya tofauti za kisiasa.

Dk Munisi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, mgombea mwenza wa urais mwaka 2025 na kwa sasa ni mbunge, amesema jukwaa hilo linalenga kuimarisha umoja miongoni mwa viongozi wanawake.

“WLF ni jukwaa linalowaleta pamoja viongozi wanawake nchini Tanzania ili kujenga umoja na kukuza sauti ya wanawake katika uongozi,” amesema.

Amesema jukwaa hilo linajumuisha wanawake waliowania nafasi za urais na makamu wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wake, WLF ni taasisi iliyoanzishwa Novemba 2025 na baadaye kusajiliwa Januari 14, 2026 na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002.

“Hiki ni chombo cha viongozi wanawake kinacholenga kuwaunganisha wanawake wenye ushawishi katika nafasi za uongozi. Licha ya tofauti za kiitikadi, tumeungana kujenga mshikamano na kuchangia maendeleo ya taifa bila kujali vyama,” amesisitiza.

Dk Munisi amesema jukwaa hilo linatarajia kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na kushiriki katika shughuli za kitaifa na kimataifa, ikiwemo maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Taasisi hiyo inalenga kuunganisha sauti, uwezo na dhamira ya wanawake katika uongozi, ikiwa na mtazamo wa kupanua ushawishi wake kitaifa, kikanda na kimataifa, chini ya kaulimbiu: “Wanawake wanaongoza mabadiliko na kuunda mustakabali wa baadaye.”

Aidha, amewataka Watanzania kuweka mbele umoja na kulinda amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa jukwaa hilo si la kisiasa wala la kiserikali.

“Tunawasihi wananchi wote kuendelea kulinda amani na kuiweka nchi mbele. Pia tunaiomba Serikali na wadau kuendelea kuhimiza umoja, upendo na ushirikiano,” amesema.

Kwa mujibu wake, maandalizi ya uzinduzi rasmi wa jukwaa hilo yako katika hatua za mwisho, huku yakitarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uongozi wa wanawake katika medani ya siasa nchini.

Naye Mwajuma Mirambo wa UMD, aliyewahi kugombea urais na ambaye ni Katibu Mkuu wa WLF, amesema baada ya kupitia changamoto na fursa mbalimbali za kijamii na kitaifa wakati wa uchaguzi, wameona umuhimu wa kuungana baada ya uchaguzi kwa kuweka kando tofauti zao za kiitikadi.

“Sote ni Watanzania na tumeona umuhimu wa kuweka kando itikadi zetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *