
Dar es Salaam. Wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi wameibua malalamiko mazito kuhusu fidia wanazolipwa kupisha mradi wa uendelezaji wa bonde hilo, wakidai kutothaminiwa kwa ardhi yao na viwango vidogo vya fedha vinavyotolewa mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Wakazi hao wameiomba Serikali kuingilia kati ili kuhakikisha fidia ya ardhi inalipwa kwa haki na kwa wakati, pamoja na kuondoa tofauti wanazodai kuwepo katika utekelezaji wa mradi huo.
Wakizungumza mbele ya Dk Mwigulu leo Jumapili, Aprili 26, 2026, aliyekuwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, jijini Dar es Salaam, wananchi hao wamesema licha ya kuupokea mradi huo kwa matarajio ya maendeleo, utekelezaji wake umeacha maumivu makubwa kutokana na kile walichodai ni ukosefu wa haki katika mchakato wa fidia.
Mkazi wa eneo hilo, Salehe Cheo, amesema awali waliridhia mradi huo na kuruhusu wataalamu kupima majengo na ardhi zao kwa matarajio ya kulipwa fidia stahiki.
“Walikuja wakapima majengo yetu na ardhi, lakini wakati wa malipo walikadiria majengo pekee na ardhi hawakuipa thamani yoyote. Tuliletewa karatasi za kusaini bila kipengele cha ardhi,” amesema Cheo.
Amesema jitihada za kufuatilia haki yao zilifikishwa hadi ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), lakini walijibiwa waende mahakamani, hali iliyowalazimu hata kupeleka malalamiko yao Benki ya Dunia, inayofadhili mradi huo.
“Tunachosisitiza ni fidia ya ardhi ilipwe. Hadi sasa hakuna mwananchi hata mmoja aliyelipwa fidia ya ardhi,” amesema Cheo.
Mkazi mwingine amesema alikataa kusaini fidia ya Sh4 milioni kwa ardhi, akieleza kuwa kiasi hicho hakimwezesha kupata eneo lingine la kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato.
“Hili suala linaumiza. Tunahamishwa, lakini kuna wengine wanaachwa kuendelea na shughuli zao ndani ya eneo la mradi,” amesema.
Kwa upande wake, Nuru Kikopa amesema tathmini ya awali ilimpa Sh1 milioni, ambayo aliikataa, kabla ya kuongezwa hadi Sh2.5 milioni na baadaye kukubali.
Hata hivyo, amesema alipokea jumla ya Sh4 milioni kwa nyumba na kiwanja, fedha ambazo hazijamwezesha kupata makazi mapya.
“Mpaka sasa sijafanya chochote na fedha hiyo, hailingani na gharama za kupata kiwanja kingine. Nimejikuta nalazimika kuishi kwa watoto wangu,” amesema Kikopa.
Naye Thomson Moshi amesema hajapokea fidia hadi sasa licha ya kufanyiwa tathmini, akidai walipewa ahadi ya kulipwa fidia ya ardhi na majengo, lakini hadi sasa kilichotolewa kinahusu majengo pekee.
“Wakati wa malipo tulioneshwa fomu yenye fidia ya majengo tu, tukiahidiwa ardhi italipwa baadaye, jambo ambalo halijatekelezwa,” amesema Moshi.
Akijibu kuhusu madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mchakato wa fidia ulizingatia mazingira ya kisheria ya eneo hilo, huku akiahidi Serikali iko tayari kurejea tathmini ili kupata suluhu ya kudumu.
Amesema tayari Sh54 bilioni kimeshatumika kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi katika bonde hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa eneo hilo.
Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa sheria zilizopo, wakazi wa bonde hilo hawakuwa na sifa ya kulipwa fidia ya ardhi kwa sababu eneo lote la Bonde la Msimbazi linahesabika kama ardhi oevu, ambayo chini ya masharti ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia hairuhusiwi kulipwa fidia ya ardhi.
“Kwa mujibu wa sheria hizi, Bonde la Mto Msimbazi lote hakuna aliyekuwa na sifa ya fidia ya ardhi kwa sababu eneo lile lipo kwenye ardhi oevu,” amesema.
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi, Serikali ilichukua hatua ya ziada kwa kuwapatia kila mwananchi Sh4 milioni ili kuwasaidia kununua ardhi katika maeneo mengine.
Ameeleza kuwa uamuzi huo haukutokana moja kwa moja na matakwa ya kisheria, bali ulikuwa ni jitihada za Serikali kuwapunguzia wananchi athari za kuondolewa katika makazi yao.
“Fedha ile ya Sh4 milioni haikuwa kwa mujibu wa sheria, bali ilikuwa ni hatua ya kuwasaidia wananchi waweze kupata maeneo mbadala,” amesisitiza.
Kutokana na kuendelea kwa malalamiko ya baadhi ya wakazi kuhusu kiwango na utaratibu wa fidia, Chalamila amesema Serikali ipo tayari kurejea upya kazi ya tathmini ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.
Amebainisha kuwa kazi hiyo inaweza kufanyika kwa kushirikiana na ofisi husika ili kupitia upya madai ya wananchi na kuangalia uwezekano wa maboresho.
“Tuko tayari kurudia zoezi hili la tathmini na kulileta kwenye ofisi yako ili tupate suluhisho linalokubalika,” amesema.
Akitoa maelekezo kuhusu hilo, Waziri Mkuu amekubali pendekezo la Chalamila na kuelekeza kuundwa kwa timu ya wataalamu kutoka Tamisemi, Wizara ya Ardhi, ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wawakilishi wa wakazi hao kwa ajili ya utatuzi wa suala hilo.
Katika ziara hiyo, Dk Mwigulu ametembelea na kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, ambayo ameonesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi.
Alichokisema Waziri Ulega
Akizungumza katika eneo hilo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mradi wa daraja la Mkwajuni, wenye urefu wa mita 20 na kimo cha mita 5.5, unaambatana na barabara unganishi zenye urefu wa mita 560.
Mradi huo, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 98, unagharimu Sh11.6 bilioni, ulianza Februari 3, 2025, ukiwa na muda wa utekelezaji wa miezi 16 na unatarajiwa kukamilika Mei 20, 2026.
Kwa upande wa daraja la Kigogo, amesema mradi huo una urefu wa mita 50 na kimo cha mita 8.9, ukiwa na barabara unganishi zenye urefu wa mita 625.
“Ujenzi wake ulianza Novemba 7, 2024, kwa muda wa miezi 18 na unatarajiwa kukamilika Mei 20, 2026. Mradi huo unagharimu Sh17.7 bilioni, na mkandarasi ameshalipwa Sh15.1 bilioni, huku utekelezaji wake umefikia asilimia 89,” amesema.
Kuhusu daraja la Jangwani, Ulega amesema litakapokamilika mambo ya njia kufungwa kwa sababu ya mafuriko yatakuwa historia.