Dar es Salaam. Ikiwa leo ni miaka 62 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, mjadala kuhusu mustakabali wake umeendelea kuwa hai, hasa  kwa vijana wa kizazi cha sasa ambao hawakushuhudia mazingira ya kihistoria yaliouzaa.

Kadii miaka inavyosonga mbele, ndivyo pengo la uelewa na tafsiri ya maana ya Muungano linavyozidi kujitokeza kati ya vizazi, jambo linalochochea mijadala yenye mitazamo kinzani.

Kwa sasa, mvutano wa kimawazo unaonekana kujikita kati ya viongozi wa kisiasa na vijana, kila upande ukiwasilisha hoja zake kuhusu umuhimu, changamoto na mustakabali wa Muungano huo.

Viongozi wengi wanasisitiza umuhimu wa historia ya Muungano, wakionya kuwa ukosefu wa elimu sahihi unaweza kuwafanya vijana kuupinga au hata kuudhoofisha.

Kwao, uelewa wa historia ni nguzo muhimu ya kujenga uzalendo na kulinda umoja wa Taifa. Hata hivyo, hoja hiyo inapewa changamoto na baadhi ya vijana wanaoona kuwa, elimu ya kihistoria pekee haitoshi bila kushughulikia matatizo halisi yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Wanasisitiza kuwa, masuala ya ajira, fursa za kiuchumi na usawa katika upatikanaji wa rasilimali, ni mambo ya msingi yanayoweza kuamua mtazamo wao kuhusu Muungano.

Kwa vijana wengi, kutoridhishwa na kile wanachokiona kama kutonufaika ipasavyo na matunda ya Muungano ndicho kiini cha malalamiko yao.

Wanalalamikia ukosefu wa ajira, changamoto za kiuchumi na kile wanachokieleza kuwa ni ukosefu wa usawa katika baadhi ya fursa.

Wapo wanaoamini kuwa Muungano una kasoro za kimuundo zinazochangia kudhoofisha maendeleo yao binafsi na ya pamoja.

Hata hivyo, badala ya kuupinga moja kwa moja, wengi wao wanasisitiza hitaji la kuona manufaa yake yakidhihirika kwa vitendo.

Kiini cha mvutano huu kinaonekana kuwa ni tofauti kati ya simulizi ya kihistoria inayosisitizwa na viongozi na uhalisia wa maisha ya sasa ya vijana.

Wakati viongozi wanasisitiza urithi wa Taifa na umuhimu wa kudumisha umoja, vijana wanatazama zaidi mustakabali wao, wakihitaji kuona fursa na manufaa yanayoweza kuboresha maisha yao.

Mkuu wa Shule ya Sayansi Asilia na Sayansi Jamii katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Dk Abdallah Mkumbukwa anasema hatima ya Muungano ipo mikononi mwa vijana, kwa kuwa wao ndio kundi kubwa zaidi katika jamii ya sasa. Anasema kizazi kilichoshuhudia kuasisiwa kwa Muungano kinaendelea kupungua, huku viongozi wengi wa sasa wakiwa wamezaliwa baada ya tukio hilo muhimu la kihistoria.

Dk Mkumbukwa anasema vijana wanapaswa kuchukua nafasi yao kwa kutafuta na kutumia taarifa sahihi kuhusu Muungano, hasa katika kutambua na kutumia fursa za kiuchumi na uwekezaji zinazotokana na uwepo wa soko pana la Muungano.

Anasisitiza kuwa, changamoto zilizopo zinahitaji kushughulikiwa kwa kuimarisha taasisi na ushirikiano kati ya pande mbili za Muungano.

Anatoa mfano wa sekta ya elimu, akieleza kuwa ingawa si sehemu ya masuala ya Muungano, bado kuna umuhimu wa taasisi husika kushirikiana ili kuboresha viwango na kushughulikia changamoto zinazowakabili wanafunzi.

Anasema iwapo malalamiko yatashughulikiwa kwa wakati, vijana wataweza kudumisha Muungano kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wa ajira, Dk Mkumbukwa anabainisha kuwa, changamoto ni kubwa kutokana na idadi kubwa ya vijana wenye elimu ikilinganishwa na fursa zilizopo.

Anashauri kuwa, ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha taarifa za fursa zinawafikia vijana, hususan kupitia mitandao ya kijamii wanayoitumia kwa wingi.

Baadhi ya viongozi wa vijana wanaeleza mitazamo yao kuhusu hali ya Muungano. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Masoud Mambo anasema malengo ya awali ya Muungano yalikuwa mazuri, yakilenga kujenga Taifa lenye nguvu kiuchumi.

Hata hivyo, anaonya kuwa changamoto za hivi karibuni, ikiwamo ubinafsi na siasa za ukanda, zinaweza kuhatarisha mshikamano huo.

Anasisitiza umuhimu wa vijana kurejea kwenye malengo ya awali ya Muungano huku wakitumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kubadilishana mawazo na kutafuta fursa za kiuchumi.

Kwa mtazamo wake, umoja wa vijana unaweza kuwa chachu ya kukabiliana na changamoto za ajira na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Katibu wa Idara ya Elimu ya Vyuo Vikuu kutoka Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Hussein Baswariyu anasema vijana wengi wanauelewa Muungano kupitia historia, lakini bado kuna tofauti za kimuundo zinazohitaji kushughulikiwa.

Anabainisha kuwa, tofauti katika mifumo ya utawala, uchumi na elimu kati ya pande mbili zinaweza kuwa kikwazo kwa vijana kunufaika kikamilifu na Muungano.

Anatoa mfano wa changamoto katika ajira na biashara, akieleza kuwa kuna vikwazo vinavyowafanya vijana kutoka upande mmoja kukosa fursa sawa upande mwingine.

Pia anagusia tofauti za viwango vya elimu zinavyoweza kuathiri udahili na uhamaji wa wanafunzi, hali inayochangia ukakasi katika mfumo mzima wa elimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Shukuru Zouma anasema pamoja na changamoto zilizopo, Muungano bado ni muhimu na unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Anasisitiza kuwa vijana wanapaswa kuhusishwa zaidi katika masuala ya kitaifa ili wawe sehemu ya uamuzi unaohusu mustakabali wao.

Kwa jumla, mjadala kuhusu Muungano unaendelea kuwa hai, ukionesha umuhimu wa kusawazisha kati ya historia yake na mahitaji ya kizazi cha sasa.

“Ili Muungano uwe endelevu, kuna haja ya kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana huku ikiendelezwa juhudi ya kuwaelimisha kuhusu misingi na umuhimu wake,” anasema.

Anasema kwa kufanya hivyo tu, ndipo Muungano utaweza kudumishwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *