Ukeketaji ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na pia tatizo la afya ya umma katika baadhi ya maeneo ya Uganda, hasa vijijini na maeneo ya mbali. Bi. Cheptoek anafanya kazi na wasichana kutoka jamii za Sebei, ambao hukabiliwa na mila na mitazamo ya kijinsia iliyojikita sana, inayochangia viwango vya juu vya ukeketaji na ndoa za utotoni.

“Mtazamo huu unapuuza uwezo wao wa kijamii, kielimu na kitamaduni. Michezo inatusaidia kukabiliana na hilo.” Anasema.

Ukeketaji mara nyingi hufuatwa na ndoa za mapema na kuacha shule, mambo ambayo yanahusiana kwa karibu na umaskini. Wasichana maskini wako katika hatari kubwa zaidi ya madhara haya, hali inayodumisha mzunguko wa umaskini. Hata hivyo, kupinga mila hizi kunakuja na gharama kubwa binafsi, wengine hutengwa na jamii zao au hata vurugu na unyanyasaji.

Licha ya changamoto hizo, mabadiliko yanaanza kuonekana katika shule na kupitia juhudi za wanawake wanaobadili mitazamo ya jamii.

Kocha anayeaminika na nafasi salama

© UNFPA/Stuart Tibaweswa Zuena Cheptoek, mkufunzi wa riadha katika Joshua Cheptegei Development Foundation, anafanya kazi na wasichana na wanawake vijana kutoka jamii za Sebei zilizo katika maeneo magumu kufikia mashariki mwa Uganda, ambazo zina viwango vya juu vya ukatili wa viungo vya uzazi na ndoa za watoto.

Bi. Cheptoek, ambaye anafanya kazi na Taasisi inayofahamika kwa jinaJoshua Cheptegei Development Foundation kwa ushirikiano na mpango wa pamoja wa mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA na la kuhudumia watoto UNICEF, ili kutokomeza ukeketaji, anatumia michezo kama njia ya kuleta mabadiliko ya kijamii.

© UNFPA/Stuart Tibaweswa Michezo inaweza kuwa chombo chenye nguvu cha kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake.

Kila mwaka, mbio za Krismasi huwaleta pamoja wavulana na wasichana kutoka jamii za Sebei. Lakini tukio hilo si la michezo pekee,kabla ya mbio, mijadala hufanyika kati ya wazazi, viongozi wa jadi, shule na wadau wengine, kwa kutumia maigizo na mijadala ya rika ili kufungua mazungumzo kuhusu ukeketaji na ndoa za utotoni.

“Bila michezo na elimu, wengi wao wangekuwa tayari wameolewa au wameacha shule,” anasema Cheptoek.

Kutokana na mbio hizo, wasichana 12 huchaguliwa kila mwaka kupata ufadhili wa masomo, huku ushirikiano na shule za sekondari ukiendelea kusaidia maendeleo yao.

Mafanikio ya wasichana katika michezo na elimu yameanza kubadilisha mitazamo ya wazazi. “Baadhi yao sasa wanaona kuwa michezo inaweza kubadilisha si maisha ya msichana mmoja tu, bali jamii nzima,” anaongeza. “Wanapokimbia, wanakimbia mbali na mila hatarishi na kuelekea maisha wanayochagua wenyewe.”

Haki za afya ya uzazi na msaada wa kisaikolojia

© UNFPA/Stuart Tibaweswa Kwa kuunga mkono mbinu zinazotawaliwa na jamii na zinazoweka waathirika kwenye kati, UNFPA na washirika wake wanahakikisha kwamba wasichana na wanawake wanaweza kuishi bila unyanyasaji.

Kambi za mafunzo pia ni sehemu salama ambapo wasichana wanaweza kujifunza, kuuliza maswali na kujenga kujiamini bila shinikizo la kijamii.

Kama kocha, Cheptoek hutoa ushauri kuhusu afya ya uzazi, usalama binafsi na msaada wa kisaikolojia. Pia huwasaidia wasichana kukabiliana na changamoto za mafanikio katika jamii ambayo bado inapingana na uhuru wa wanawake.

“Wanariadha wa kike mara nyingi huambiwa waache michezo na waolewe,” anasema. “Lakini elimu na uhuru wa kifedha huwapa chaguo.”

Pia anazungumzia wazi unyanyasaji wa kijinsia, mahusiano salama, ridhaa na dalili za hatari. Mazungumzo haya yamekuwa muhimu zaidi kufuatia matukio ya kusikitisha kama kifo cha mwanariadha Rebecca Cheptegei mwaka 2024.

“Tunahimiza usalama kwa sababu hatutaki kupoteza wanawake zaidi,” anaeleza Cheptoek na kuongeza akisema,“wanawake wanapofanikiwa na kuwa huru zaidi, wakati mwingine hukumbana na hatari katika jamii ambazo bado zina mitazamo ya kizamani.”

Nafasi ya UNFPA katika Kuleta Mabadiliko

Kwa kuwa kinga ya mapema na msaada wa kisaikolojia ni muhimu katika kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, Bi. Cheptoek huanzisha mazungumzo kuhusu mamlaka, udhibiti na dalili za awali za ukatili, ili kuhakikisha wanariadha wanaelewa haki zao na wanajua wapi pa kupata msaada.

“Michezo inapaswa kuwapa wasichana uhuru, si kuhatarisha maisha yao.”

Aidha, matukio na shughuli za michezo hutoa fursa ya kuanzisha mijadala kuhusu umuhimu wa kukomesha ukeketaji, kuimarisha afya na haki za uzazi, pamoja na kukuza usawa wa kijinsia. UNFPA kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na wa kijamii nchini Uganda, inaendelea kuhamasisha jamii kupitia michezo, ambapo mamia ya vijana, wazazi na viongozi wa jamii hufikiwa katika mazingira jumuishi na yasiyotishia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *