Mfalme wa Oman Haitham bin Tariq amemkaribisha Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika Kasri la Al-Barakah mjini Muscat, mapema Jumapili.

Kwa mujibu wa taarifa , viongozi hao wawili walifanya mashauriano kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo, juhudi za upatanishi, na mikakati iliyofanyika hadi sasa ili kusaidia kumaliza migogoro ya kikanda. 

Sutlan wa Oman amepokea kwa makini maoni yaliyowasilishwa na upande wa Iran kuhusu masuala haya.

Aidha, Sultan Haitham bin Tariq alieleza mtazamo wake kuhusu namna ya kuendeleza juhudi hizi ili kuongeza uwezekano wa kufikiwa kwa suluhu za kisiasa zilizo thabiti, na jinsi ya kukabiliana na athari za migogoro kwa mataifa ya eneo hili.

Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Oman katika kikao hicho, Mfalme wa Oman amesisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo na diplomasia katika utatuzi wa masuala, ili kuimarisha misingi ya amani.

Kwa upande wake, Araghchi alitoa shukrani kwa msimamo wa Oman wa kuunga mkono mazungumzo na juhudi za kuleta amani na utulivu katika eneo, hasa kwa kuzingatia changamoto zinazoikabili kanda kwa sasa.

Kabla ya kufika Muscat, waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa ametembelea Pakistan na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusu mchakato wa mazungumzo ya amani na Marekani.

Iran imesisitiza kuwa haitakubali matakwa ya kupitiliza ya Marekani katika mapatano ya kusitisha vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *