Mbeya. Wakati vijana na wahitimu wa elimu ya juu nchini wakiendelea kulalamikia ukosefu wa ajira, hali tofauti imeripotiwa mkoani Mbeya ambako vyuo vinane vya mafunzo ya udereva vimefungwa kutokana na uhaba wa walimu wenye sifa.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limewataka wahitimu kujitokeza kuchangamkia fursa zilizopo.
Vyuo hivyo ni vya mafunzo ya udereva, imeelezwa kuwa pamoja na uhitaji mkubwa wa walimu katika kada hiyo, mwitikio wa wasomi umekuwa mdogo, hali inayosababisha kukosekana kwa wataalamu wa kufundisha.
Akizungumza leo Jumapili Aprili 26, 2026, wakati wa mahafali ya wahitimu wa ualimu wa udereva yaliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Mkoa wa Mbeya, Kamanda wa Usalama Barabarani mkoani humo, Notker Kilewa amesema hadi sasa vyuo vinane vimefungwa kutokana na kukosa walimu, huku vingine vikiwa na mipango ya kuanzishwa lakini vikikosa rasilimali watu.
Amesema fani ya ualimu wa udereva kwa sasa ina fursa kubwa ya ajira na ni muhimu kwa wahitimu kujitokeza kuisomea ili kusaidia kupunguza ajali zisizo za lazima barabarani.
“Kama kuna mtu ana sifa na anahitaji ajira, ajitokeze. Nipo tayari kusaidia kuhakikisha anapata nafasi. Kuna vyuo vingi vinahitaji walimu na vingine vinataka kufunguliwa lakini vinakosa wataalamu,” amesema Kilewa.
Aidha, amebainisha kuwa ameanzisha utaratibu wa kurekodi taarifa za ajali kwa kuhusisha chuo alichosoma dereva husika, hatua itakayosaidia kupata takwimu sahihi za ubora wa mafunzo yanayotolewa.
Picha tofauti zikionesha wanafunzi wahitimu wa ualimu wa madereva wakiwa na viongozi wa serikali akiwamo Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Notker Kilewa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa huo, ACP Anthony Mkwawa.
“Tumeanza kuweka kumbukumbu za kila ajali, ikiwamo chuo alichosoma dereva, ili baadaye tuweze kubaini maeneo yenye changamoto na kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na mamlaka husika,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya, ACP Anthony Mkwawa aliyemwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa huo, amesema awali, sekta ya udereva ilikumbwa na changamoto kubwa kutokana na uwepo wa madereva wasiokuwa na sifa.
Amesema baadhi ya madereva wamepewa vyeti na leseni bila kupitia mafunzo sahihi, hali iliyochangia kuongezeka kwa ajali.
Amesema baada ya kufanyika uhakiki, imebainika kuwa leseni nyingi zilikuwa batili na hatua kali zilichukuliwa kudhibiti hali hiyo.
“Tumefanya uhakiki wa vyuo na walimu wake na kubaini mapungufu makubwa. Hivyo, tukaona umuhimu wa kuimarisha mafunzo kwa walimu wa udereva ili kuhakikisha tunapata madereva wenye ujuzi na wanaofuata sheria,” amesema Mkwawa.
Amesema matarajio yao ni kuona wahitimu wa mafunzo hayo wanazalisha madereva bora watakaochangia kupunguza ajali barabarani.
Pia, amempongeza Kamanda Kilewa kwa juhudi zake za kuboresha usalama barabarani, akibainisha kuwa ajali zimepungua tangu aanze kutekeleza mikakati mbalimbali ya elimu na ufuatiliaji.
Hata hivyo, ameonya kuhusu ajali zinazotokana na uchovu na usingizi kwa madereva, akisisitiza umuhimu wa madereva kupumzika wanapohisi kuchoka ili kuepuka madhara.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Tanzania, Odas Ngoma amesema fani ya ualimu wa udereva ni ajira yenye uhakika, akibainisha kuwa zaidi ya vyuo 180 vinahitaji walimu.
“Vijana wengi wanatafuta ajira, lakini huku kuna fursa kubwa. Kila siku napokea simu nyingi kutoka vyuo vinavyohitaji walimu, hivyo ni wakati wa vijana kuchangamkia nafasi hizi,” amesema Ngoma.
Mratibu wa mafunzo ya kozi fupi Veta Mbeya, Rajabu Ghuliku amesema mafunzo hayo yalidumu kwa miezi mitatu na kuwahusisha wanafunzi 16, huku akibainisha kuwa bado muitikio ni mdogo licha ya uhitaji uliopo.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Anthony Malamla amesema elimu waliyoipata itawasaidia kuzalisha madereva bora na kuchangia maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini.