Njombe. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesisitiza kuwa kipaumbele kwa usalama wa afya na mwili kazini ni kichocheo kikubwa cha ari ya kazi kwa wafanyakazi.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa maonesho ya Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yanayofanyika mkoani Njombe kuanzia Aprili 24 hadi 30, 2026, ambapo kampuni hiyo imeonesha dhamira yake ya kuimarisha usalama kazini zaidi ya kufuata sheria, kwa kuzingatia pia afya ya kisaikolojia na ustawi wa wafanyakazi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema ustawi wa watu hauko nje ya mafanikio ya mgodi, bali ndio msingi wake. Amesema mgodi wenye tija unategemea wafanyakazi walio na afya njema, wanaoungwa mkono na kuheshimiwa.

“Kampuni inaamini hakuna lengo la kibiashara linaloweza kupewa kipaumbele kuliko afya ya kimwili na kiakili ya wafanyakazi wake. Sambamba na usalama, heshima na ushirikiano ni misingi muhimu inayotuongoza katika kufanya kazi na wafanyakazi pamoja na jamii inayotuzunguka,” amesema.

Amesema Wiki ya Usalama ya OSHA inatoa jukwaa muhimu kwa kampuni kuthibitisha dhamira hiyo na kushiriki katika mjadala wa kitaifa kuhusu afya ya kisaikolojia kazini.

Mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, yanayoadhimishwa Aprili 28, yamebeba kaulimbiu isemayo, “Mazingira Bora ya Kazi ya Kisaikolojia: Njia ya Wafanyakazi Wenye Mafanikio na Taasisi Imara.”

Wafanyakazi wa GGML wakiwaonesha wananchi taratibu za usalama mahala pa kazi katika maonesho ya Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yanayoendelea mkoani Njombe.

Kaulimbiu hiyo inatambua kuwa mzigo wa kazi, mawasiliano, mtindo wa uongozi na msaada wa taasisi ni mambo muhimu sawa na mazingira ya kimwili katika kuhakikisha usalama kazini. Kwa GGML, kaulimbiu hiyo inaendana moja kwa moja na namna kampuni inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, usalama si suala la kufuata sheria pekee, bali ni thamani kuu inayoongoza maamuzi yote ya kiutendaji.

GGML inaendesha mfumo wa kina wa huduma za afya ndani ya eneo la kazi, ukiwa na wataalamu waliobobea, unaowapa wafanyakazi huduma za matibabu, ufuatiliaji wa afya kazini na msaada wa ustawi.

Aidha, kampuni hiyo ina programu mbalimbali za afya na ustawi zinazolenga kujenga nguvu kazi yenye afya na ari. Dhamira hiyo pia imepanuliwa kwa jamii zinazozunguka mgodi mkoani Geita, ambapo inaunga mkono huduma za afya kupitia ushirikiano na vituo vya afya vya ndani pamoja na Serikali katika ngazi za mkoa na taifa.

“Ushiriki wetu katika Wiki ya OSHA unaakisi imani hiyo,” amesema Dk Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML.

“Hatujaja tu kuonesha mifumo yetu ya usalama, bali pia kushiriki katika mjadala wa kitaifa kuhusu namna bora ya kuwajali watu wetu wanapokuwa kazini—afya yao ya mwili, ustawi wao wa akili, pamoja na heshima na thamani yao kama binadamu,” amesema.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, ameutaka uongozi wa GGML kuhakikisha shughuli zake zinakuwa na athari chanya katika uchumi wa jamii zinazowazunguka.

Amesema ni muhimu kwa kampuni hiyo kutoa fursa za kazi za muda mfupi na kuwezesha miradi mbalimbali ya kijamii ili kuongeza manufaa kwa wananchi.

Aidha, amezitaka kampuni za uchimbaji wa madini nchini kuwawezesha wachimbaji wadogo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa na usimikaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi, ili kujenga uchumi jumuishi unaotokana na sekta ya madini.

Waziri Sangu alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Aliipongeza menejimenti ya mgodi huo, alisema imefanikiwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania, ambapo GGML imeajiri wafanyakazi 2,366 moja kwa moja na wengine 4,629 kupitia wakandarasi wanaotoa huduma katika mgodi huo.

“Ninawapongeza kwa kuweka usalama na afya kama tunu yenu ya kwanza, na hii imejidhihirisha katika wasilisho lenu mlilofanya hapa, ambapo masuala ya usalama na afya yamechukua nafasi ya juu zaidi kuliko biashara mnayofanya,” amesema Waziri Sangu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, alisema OSHA ni miongoni mwa taasisi muhimu zinazowezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa tija katika Mkoa wa Geita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *