Wajumbe wamejadili hatari zinazoongezeka kwa njia muhimu za usafirishaji wa bidhaa duniani, hasa athari kwa usambazaji wa nishati na misaada ya kibinadamu.

Guterres aonya kuhusu Athari za usumbufu wa Hormuz

Akilihutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa hali ya kutokuwepo utulivu katika Mlango Bahari wa Hormuz inaleta athari kubwa za kiuchumi na kibinadamu duniani. 

Amebainisha kuwa njia hiyo muhimu ya majini husafirisha sehemu kubwa ya mafuta, gesi na mbolea duniani, na kwamba usumbufu unaoendelea unaongeza gharama za usafiri na bima huku ukivuruga minyororo ya usambazaji. 

“Bahari lazima iwe eneo la amani na ushirikiano si la mivutano au shinikizo,” amesema Guterres, akionya kuwa athari zake tayari zinaonekana duniani kote kupitia kupanda kwa bei za mafuta na chakula pamoja na kuongezeka kwa hatari ya njaa na umaskini, hasa katika maeneo yaliyo hatarini.

UN Photo/Loey Felipe Arsenio Dominguez Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini IMO akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video kuhusu usalama wa baharini

IMO yatoa wito wa hatua kulinda mabaharia na biashara

Akihutubia kwa njia ya video, Arsenio Dominguez, Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Umoja wa Mataifa la usafiri wa majini  IMO, amesisitiza umuhimu wa kulinda shughuli za baharini na usalama wa wafanyakazi wa majini au mabaharia. 

“Kanuni za uhuru wa usafiri wa majini hazina mjadala” alisema, akiongeza kuwa meli zote lazima ziweze kusafiri bila vikwazo na kwamba njia nyembamba za bahari haziwezi kufungwa na mataifa ya pwani. 

Pia ameonya kuwa hakuna msingi wa kisheria wa kutoza ushuru wa forodha kwa meli zinazopita, akisema hatua hizo zinaweza kudhoofisha biashara ya baharini duniani.

Akielezea wasiwasi wake kuhusu takribani mabaharia 20,000 waliokwama katika Ghuba ya Uajemi, Dominguez amezitaka nchi wanachama kuunga mkono mpango wa IMO wa kuwawezesha kuondolewa mara tu hali ya usalama itakaporuhusu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *