Kupitia taarifa ya UN Women iliyosambazwa leo kwa vyombo vya habari katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba na katika ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswisi, Anna Mutavati amenukuliwa akisema, “takribani asilimia 60 ya watu 223,641  ya waliokimbia makazi yao tangu mwanzo wa mwaka huu nchini Sudan Kusini ni wanawake na wasichana, wastani wa wanawake 104 kila saa,” na akaongeza kuwa baadhi ya wanawake na wasichana “wanakula mimea ya porini ili kuishi,” huku wengine wakikaa siku kadhaa bila kula.

Amefafanua zaidi kuwa sehemu kubwa ya watu waliokimbia makazi yao ni kutoka Jimbo la Jonglei, ambako takribani wanawake na wasichana 174,197 wameathiriwa na mapigano. Bi. Mutavati amesema wanawake na wasichana ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi ya kulengwa, ikiwemo shambulio la Machi katika Eneo la Utawala la Ruweng lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 169 akionya kuwa ghasia zinazidi kuongeza hatari kwa wale waliokwishakimbia makazi yao.

Pia ameeleza wasiwasi kuhusu kusambaratika kwa huduma muhimu, akisema uporaji na uharibifu wa vituo vya afya umeacha wanawake bila huduma muhimu za matibabu. “Wanawake wanajifungua bila huduma yoyote ya kitabibu kwa hatari kubwa ya kupoteza maisha,” amesema.

UN Women inakadiria wanawake na wasichana milioni 5 nchini Sudan Kusini wanahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu, wakiwemo milioni 2.5 wanaohitaji huduma zinazohusiana na ukatili wa kijinsia.

Akitoa wito wa hatua za haraka, Bi. Mutavati amesema uongozi wa wanawake lazima ubaki kuwa kiini cha juhudi za amani na ametoa wito wa kuheshimiwa kwa kiwango cha asilimia 35 cha uwakilishi wa wanawake serikalini chini ya makubaliano ya amani. “Hakuna njia ya amani ya kudumu iliyothibitika zaidi kuliko uongozi wa wanawake,” amesema, huku pia akitaka ufadhili kwa mashirika yanayoongozwa na wanawake na msaada kwa kaya zinazoongozwa na wanawake.

Wakati Sudan Kusini ikielekea katika uchaguzi wa mwaka huu 2026, Mkurugenzi huyo wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wa UN Women ametoa wito wa kuwepo kwa mchakato wa uchaguzi unaoaminika, jumuishi na wa uwazi unaohakikisha ushiriki wa wanawake katika kila hatua. Amenukuliwa akisema, “tunatoa wito wa utekelezaji kamili na wa haraka” wa makubaliano ya amani,  na akasisitiza kuwa kulinda wanawake na wasichana na kuhakikisha wanashiriki katika uamuzi ni msingi wa kufikia amani ya kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *