Dar es Salaam. Jina la Cole Tomas Allen, mwanamume mwenye umri wa miaka 31 kutoka mji wa Torrance, California, limeibuka ghafla kwenye vichwa vya habari duniani baada ya kuhusishwa na tukio la ufyatuaji risasi lililotikisa hafla ya White House Correspondents’ Dinner jijini Washington DC, Marekani.

Tukio hilo lilitokea katika Hoteli ya Washington Hilton, ilipofanyika hafla hiyo ambako mtuhumiwa alikuwa amefikia kama mgeni wa muda mfupi.

Allen, ambaye kwa mujibu wa kumbukumbu za umma alikuwa mwalimu wa muda katika kampuni ya maandalizi ya mitihani pamoja na mtengenezaji wa michezo ya video, sasa anachunguzwa na vyombo vya usalama kufuatia tuhuma za kujaribu kufanya shambulio dhidi ya viongozi wa serikali akiwamo Rais wa Marekani, Donald Trump.

Cole Tomas Allen (31) kutoka mji wa Torrance, California akiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za jaribio la kumuua Rais wa Marekani, Donald Trump. Picha na Mtandao

Shirika la Habari la CNN, limefanya uchunguzi wa kina kuhusu Allen na hapa wanamwelezea kwa kina zaidi.

Maisha yake kabla ya tukio

Kwa nje, Allen alionekana mtu wa kawaida na mwenye mafanikio. Alihitimu masomo ya uhandisi wa mitambo katika Chuo cha California Institute of Technology kati ya mwaka 2013 hadi 2017. Akiwa chuoni, alihusishwa na shughuli mbalimbali ikiwamo ushirika wa Kikristo na vikundi vya wanafunzi.

Mwaka 2017 aliwahi kuangaziwa kwenye taarifa ya habari za ndani baada ya kubuni kifaa cha dharura cha kusimamisha viti vya magurudumu, jambo lililoonesha ubunifu wake wa kiteknolojia.

Baada ya kuhitimu, alianza kufanya kazi kama mwalimu wa muda katika Kampuni ya C2 Education, ambapo hata alitunukiwa tuzo ya Mwalimu Bora wa Mwezi, Desemba 2024.

Mbali na ualimu, Allen pia alikuwa mtengenezaji wa michezo ya video. Aliunda mchezo wa kujitegemea unaoitwa Bohrdom, uliouzwa kwa bei nafuu kwenye jukwaa la Steam. Mchezo huo ulielezewa kuwa wa ujuzi na usio wa vurugu, jambo linaloonesha tofauti kubwa kati ya kazi yake na tuhuma zinazomkabili sasa.

Mabadiliko ya mienendo

Hata hivyo, uchunguzi wa awali unaonesha katika miaka ya hivi karibuni, Allen alianza kubadilika kitabia. Kwa mujibu wa familia yake, alianza kutoa kauli kali za kisiasa alipokuwa akijihusisha na harakati za mrengo wa kushoto jijini Los Angeles.

Inadaiwa pia alijiunga na kundi la wanaharakati liitwalo The Wide Awakes, na kuanza kujihusisha zaidi na mijadala ya kisiasa yenye misimamo mikali.

Aidha, rekodi zinaonesha alichangia fedha kidogo kwenye kampeni ya kisiasa ya Kamala Harris mwaka 2024.

Sambamba na mabadiliko hayo ya kiitikadi, Allen alinunua silaha kihalali bastola ya kaliba 38 ya mwaka 2023 na bunduki aina ya shotgun mwaka 2025, baada ya kupita ukaguzi wa usalama wa Federal Bureau of Investigation (FBI).

Safari ya kuelekea Washington

Kwa mujibu wa mamlaka, siku chache kabla ya tukio, Allen alisafiri kwa treni kutoka Los Angeles kupitia Chicago hadi Washington DC. Alifika na kufikia katika Hoteli ya Washington Hilton, ambayo huwa mwenyeji wa hafla ya kila mwaka ya waandishi wa habari.

Ndani ya hoteli hiyo ndipo viongozi wakuu wa Serikali ya Marekani, wanahabari na watu mashuhuri hukutana kwa chakula cha jioni.

Maandishi yaliyoshtua familia

Kabla ya shambulio hilo, Allen alituma ujumbe kwa familia yake uliosababisha taharuki. Katika maandishi hayo, alianza kwa kuomba radhi kwa watu aliowaumiza kwa vitendo vyake.

Maofisa wa usalama wakiimarisha ulinzi wakati jaribio linalodaiwa kuwa la kuumua Rais wa Marekan, Donald Trump. Picha na Mtandao

“Naomba nianze kwa kuomba radhi kwa kila mtu ambaye nimevunja imani yake,” aliandika, akiongeza, “sitarajii kusamehewa.”

Katika ujumbe huo, alijitaja kama ‘Friendly Federal Assassin’ na kueleza hasira zake dhidi ya utawala wa serikali ya Marekani. Pia, alidai alikuwa akilenga maofisa wa serikali, akionesha wazi nia ya kisiasa nyuma ya tukio hilo.

Allen aliandika hakulenga polisi moja kwa moja, lakini alikiri kuwa angeweza kupitia kwa yeyote ili kufikia malengo yake.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe huo, alijaribu kuhalalisha matendo yake kwa misingi ya dini, akisema kukaa kimya wakati wengine wanateswa si tabia ya Kikristo.

Shambulio lenyewe

Siku ya tukio, Allen alijaribu kuvunja ulinzi mkali nje ya ukumbi wa hafla hiyo. Inadaiwa alifyatua risasi kadhaa, ambapo mmoja wa maofisa wa Secret Service alipigwa lakini aliokolewa na koti la kuzuia risasi.

Rais Donald Trump na viongozi wengine waliondolewa haraka ukumbini kwa usalama huku mshukiwa akikamatwa papo hapo.

Uchunguzi unaoendelea

Mamlaka za Marekani sasa zinaendelea kuchunguza historia ya Allen, ikiwamo shughuli zake kwenye mitandao ya kijamii, maandishi yake na mawasiliano yake ya karibu.

Mkuu wa muda wa sheria nchini humo amesema dalili za awali zinaonesha mshukiwa alikuwa na lengo la kisiasa, ingawa bado wanajaribu kubaini chanzo kamili cha msukumo wake.

Familia yake, akiwamo ndugu yake wa kiume, waliripoti kwa polisi baada ya kupokea ujumbe wake, hatua ambayo huenda ilisaidia kuharakisha ufuatiliaji wa tukio hilo.

Mashtaka yanayomkabili

Allen anakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwamo kutumia silaha kinyume cha sheria na kumshambulia ofisa wa serikali kwa kutumia silaha hatari.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hadi sasa hajawa tayari kushirikiana na wachunguzi.

Taswira pana

Kesi ya Allen imeibua mjadala mpana kuhusu mabadiliko ya kitabia ya watu, athari za misimamo mikali ya kisiasa, pamoja na udhibiti wa silaha nchini Marekani.

Kutoka kuwa mwalimu aliyepata tuzo na mbunifu wa michezo ya video, hadi kuwa mshukiwa wa shambulio dhidi ya viongozi wa Taifa, simulizi ya Cole Tomas Allen inaacha maswali mengi bila majibu hasa kuhusu ni nini hasa kilimsukuma kuvuka mstari huo hatari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *