
Mkutano wa 11 wa Mapitio ya Mkataba wa kutozalisha na kutoeneza silaha za nyuklia NPT umeanza leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, ukileta pamoja viongozi wa dunia kutathmini maendeleo katika kudhibiti uenezaji wa silaha za nyuklia na kuendeleza juhudi za upokonyaji silaha hizo.
Mkutano huo wa ngazi ya juu, ulioitishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Upokonyaji Silaha UNODA, utaendelea hadi tarehe 22 Mei, na miongoni mwa mambo yanayojadiliwa ni changamoto za kisiasa na usalama wa kimataifa pamoja na kusuasua kwa hatua za kupunguza silaha za nyuklia.
Mvutano wazuka kuhusu nafasi ya Iran katika mkutano wa NPT
Katika Mkutano huo wa NPT, mvutano uliibuka kuhusu nafasi ya Iran kama Makamu wa Rais wa Kamati Kuu, huku Marekani ikipinga uteuzi wake na Uingereza kwa niaba ya Ufaransa na Ujerumani na Australia na Emarati pia zikipinga.
Hata hivyo, licha ya upinzani huo, Marekani wala Australia hawakuomba kura rasmi, wakisema hawataki kuvuruga kazi ya mkutano huku wakijitenga na makubaliano hayo na kuhoji uhalali wa Iran kushika nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Iran imesisitiza kuwa mjadala ulenge masuala ya msingi ya nyuklia badala ya siasa.
| Rais wa mkutano ameeleza kuwa uamuzi kuhusu makamu wa rais ulikuwa tayari umefikiwa katika kikao kilichopita na, kwa kuwa hakuna aliyedai kura, utaendelea kutumika huku pingamizi zote zikirekodiwa. |
Wakati huo huo, Urusi imekosoa kile ilichokiita kuingizwa kwa siasa katika mkutano huo, ikieleza kuwa upinzani huo ni shambulio la kisiasa lisilo la kawaida dhidi ya nchi mwanachama.
Mkataba muhimu
Mkataba wa NPT, ulioanza kutumika mwaka 1970, bado ni msingi mkuu wa juhudi za kimataifa za kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia.
Ukiwa na wanachama 191, wakiwemo mataifa matano yenye silaha za nyuklia, ni moja ya mikataba inayoungwa mkono zaidi duniani katika masuala ya upokonyaji silaha.
Mkataba huu unajengwa juu ya nguzo tatu kuu: upokonyaji silaha za nyuklia, kuzuia uenezaji, na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.
Pia ndio mkataba pekee wa kisheria unaoyalazimu mataifa yenye silaha za nyuklia kujitolea kupunguza silaha hizo.
Wanadiplomasia na wachambuzi wanasema uaminifu wa mkataba huu unazidi kuwekewa shinikizo kadri hali ya usalama duniani inavyobadilika na kuaminiana kati ya mataifa makubwa kupungua.
Uongozi na matarajio
Mkutano huo unaongozwa na Do Hung Viet, Mwakilishi wa Kudumu wa Viet Nam katika Umoja wa Mataifa, anayechukua nafasi ya Rais mteule wa mkutano huu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hatari za nyuklia.
Wajumbe wameanza mkutano huo kwa mdahalo mkuu unaohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje pamoja na wawakilishi waandamizi wa mashirika ya kimataifa ukifauatiwa na majadiliano ya kina kulingana na nguzo tatu za mkataba.
Mkuu wa UN aonya kuhusu ongezeko la nyuklia
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Kumi na Moja wa Mapitio NPT, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa António Guterres ameonya kuwa dunia inaingia katika hali hatari ya “kusahau kwa pamoja kuhusu madhara makubwa ya silaha za nyuklia”.
Amesema kuongezeka kwa kutoaminiana kimataifa, mashindano mapya ya silaha na kudhoofika kwa kanuni za kimataifa vinaweka ubinadamu katika hatari mpya ya vita vya nyuklia, miongo kadhaa baada ya Vita Baridi.
Hatari zinazoongezeka duniani
Guterres amechora taswira ya dunia inayosahau mafunzo ya historia, akibainisha kuwa idadi ya vinu vya nyuklia inaongezeka kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa huku majaribio ya nyuklia yakianza kujadiliwa tena.
Ameeleza pia kuwa matumizi ya kijeshi duniani yamefikia dola trilioni 2.7 mwaka jana, sambamba na kudorora kwa mifumo ya kudhibiti silaha na kuongezeka kwa hatari ya uenezaji wa silaha hizo.
“Je, tumesahau kwamba vita vya nyuklia haviwezi kushindwa na havipaswi kupiganwa?” amehoji, akiwataka viongozi kukumbuka madhara mabaya ya silaha za nyuklia.
Wito wa kuimarisha ahadi na kukabili hatari mpya
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa NPT bado ni “msingi mkuu wa juhudi za kimataifa za upokonyaji silaha na kuzuia uenezaji wa nyuklia, lakini akaonya kuwa mkataba huo unadhoofishwa na ahadi ambazo hazijatekelezwa na kupungua kwa imani”.
Amezitaka nchi kurejea kikamilifu katika ahadi zao bila masharti, kuimarisha mifumo ya ulinzi chini ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA, na kudumisha marufuku ya majaribio ya nyuklia.
Pia amehimiza mkataba huo ubadilike ili kukabiliana na hatari mpya zinazotokana na teknolojia kama akili mnemba na kompyuta za quantum, huku akisisitiza umuhimu wa binadamu kubaki na udhibiti wa silaha za nyuklia.
Ujumbe wa waathirika waongeza dharura ya hatua
Nje ya ukumbi wa mkutano, manusura wa mashambulizi ya mabomu ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki wanaojulikana kama Hibakusha wameandaa maonesho maalum kukumbusha viongozi gharama halisi ya vita vya nyuklia.
Guterres ametaja kutambuliwa kwa Nihon Hidankyo kwa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2024 kama ishara ya juhudi zao zisizokoma. “Upokonyaji silaha si tuzo ya amani, bali ndio msingi wa amani,” amesema, akitoa wito wa hatua za haraka za kimataifa kuondoa silaha za nyuklia na kuzuia janga la kibinadamu.
Changamoto baada ya kukwama kwa makubaliano
Matarajio ya kufikia makubaliano yanaonekana kuwa ya tahadhari. Mikutano ya mapitio ya mwaka 2015 na 2022 haikuweza kufikia makubaliano ya hati ya mwisho yenye uzito, jambo lililoonesha mgawanyiko mkubwa kati ya nchi wanachama kuhusu masuala muhimu kama ahadi za upokonyaji silaha na usalama wa kikanda.
Mzunguko huu wa mapitio utachunguza utekelezaji wa mkataba tangu mwaka 2022 na kutafuta njia za kuimarisha ushirikiano.
Wachambuzi wanasema kuwa kuziba pengo la tofauti za kisiasa kutakuwa muhimu ili mkutano huu uweze kuzaa matokeo yenye maana.
Mvutano wazuka kuhusu nafasi ya Iran katika NPT
Katika Mkutano huo wa NPT, mvutano uliibuka kuhusu nafasi ya Iran kama Makamu wa Rais wa Kamati Kuu, huku Marekani ikipinga uteuzi wake na Uingereza kwa niaba ya Ufaransa na Ujerumani na Australia na Emarati pia zikipinga.
Hata hivyo, licha ya upinzani huo, Marekani wala Australia hawakuomba kura rasmi, wakisema hawataki kuvuruga kazi ya mkutano huku wakijitenga na makubaliano hayo na kuhoji uhalali wa Iran kushika nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Iran imesisitiza kuwa mjadala ulenge masuala ya msingi ya nyuklia badala ya siasa.
Rais wa mkutano ameeleza kuwa uamuzi kuhusu makamu wa rais ulikuwa tayari umefikiwa katika kikao kilichopita na, kwa kuwa hakuna aliyedai kura, utaendelea kutumika huku pingamizi zote zikirekodiwa.
Wakati huo huo, Urusi imekosoa kile ilichokiita kuingizwa kwa siasa katika mkutano huo, ikieleza kuwa upinzani huo ni shambulio la kisiasa lisilo la kawaida dhidi ya nchi mwanachama.
Mwelekeo wa hatua za baadaye
Mbali na kutathmini ahadi zilizopita, mkutano huu unalenga kubaini hatua za vitendo za kuendeleza upokonyaji silaha za nyuklia na kuimarisha mifumo ya kuzuia uenezaji, huku pia ukihamasisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani.
Kadri mvutano wa kimataifa unavyoendelea, wengi wanaona mkutano huu kama kipimo muhimu cha uwezo wa jumuiya ya kimataifa kuimarisha umuhimu na ufanisi wa mkataba wa NPT katika mazingira yanayozidi kuwa magumu ya usalama duniani.