
“Uhuru, hadhi, usawa na haki za binadamu ndizo nguzo za Katiba ya kidemokrasia ya taifa hili,” amesema Katibu Mkuu, akieleza siku hiyo kuwa “wakati wa kihistoria unaoainisha mustakabali wa nchi hiyo.”
Hata hivyo, maadhimisho hayo yamegubikwa na kile alichokiita “wasiwasi Mkubwa”kufuatia mashambulizi yanayowalenga wahamiaji na raia wa kigeni.
Vurugu hazina nafasi katika jamii ya kidemokrasia
Taarifa za unyanyasaji, vitisho na mashambulizi katika majimbo ya KwaZulu-Natal na Eastern Cape zimezua taharuki katika Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu amekemea kemea vikali kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York Marekani.
“Vurugu, ulinzi wa kujichukulia sheria mkononi na aina zote za uchochezi wa chuki hazina nafasi katika jamii jumuishi ya kidemokrasia inayotawaliwa na utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.”
Alilaani watu binafsi “wanaochochea vurugu na kutumia vibaya hali ngumu za kiuchumi,” akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni vya uhalifu na vinapaswa kushughulikiwa ipasavyo.
Kumbukumbu ya mshikamano uliojenga taifa
Akirejea historia, Guterres amekumbusha mshikamano wa kimataifa na wa Kiafrika uliosaidia kuangusha utawala wa ubaguzi wa rangi.
“Mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi yaliungwa mkono na mshikamano wa kimataifa na wa Kiafrika,” amesema, akiongeza kuwa maendeleo ya nchi hiyo yamejengwa juu ya “kuishi pamoja na mchango wa watu kutoka Afrika Kusini, bara la Afrika na kwingineko.”
Wito wa uwajibikaji na utawala wa sheria
Katibu Mkuu amekaribisha kauli za wazi za mamlaka za Afrika Kusini zinazosisitiza kuwa haki lazima itekelezwe kupitia sheria, si kwa watu kujichukulia hatua wenyewe mkononi.
Alisisitiza kuwa “Wahusika wa vitendo vya uhalifu watachunguzwa na kuwajibishwa na Uchunguzi lazima uwe wa haraka, wa kina, huru na usio na upendeleo.”
Umoja wa mataifa pia imepongeza juhudi za serikali kupambana na rushwa katika mifumo ya uhamiaji na kutekeleza Mpango wa Kitaifa dhidi ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni.
Akikiri changamoto za kijamii na kiuchumi zinazochochea mvutano, Guterres ametoa wito wa hatua za haki na zisizo na ubaguzi.
“Kushughulikia changamoto hizi lazima kufanyike kwa mujibu wa sheria, bila ubaguzi na kwa kuheshimu haki na hadhi ya kila mtu.”
Amebainisha kuwa changamoto hizi si za Afrika Kusini pekee bali ni tatizo la kimataifa.
UN iko tayari kusaidia kupunguza mvutano
Umoja wa Mataifa umeeleza utayari wake kusaidia kupunguza mvutano na kulinda jamii zilizo hatarini.
“Ushirikishwaji endelevu wa jamii, kuheshimu haki za binadamu, uongozi wenye uwajibikaji na hatua za kisheria ni muhimu kuzuia vurugu zaidi,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia “kupunguza mvutano, kukabiliana na uchochezi, kulinda walio hatarini na kuimarisha mshikamano wa kijamii.”
Wakati wananchi wa Afrika Kusini wakitafakari juu ya urithi wa uhuru walioupata mwaka 1994, ujumbe wa Katibu Mkuu unaashiria mtihani mkubwa iwapo maadili yaliyomaliza apartheid yanaweza kulinda umoja katika nyakati za changamoto za kiuchumi na kijamii.
Tofauti iko wazi kati ya sherehe na tahadhari, kati ya mshikamano wa zamani na migawanyiko ya sasa amesema
Na ujumbe uko wazi, ahadi ya Siku ya Uhuru lazima iwahusu wote wanaoishi ndani ya mipaka ya taifa hilo.