Dar es Salaam. Kati ya wasanii waliochipukia Mwanza na kuja kuvuma katika Bongofleva, ni pamoja na Pancras Ndaki Charles maarufu kama PNC ambaye alijizolea umaarufu kwa nyimbo zake za kubembeleza na hata kulalamika kuhusu mapenzi.
Wengi wanamkumbuka hasa kupitia nyimbo zake mbili, ‘Mbona’ na ‘Nalia’ ambazo ndio zilimtambulisha ila baada ya hapo hakuwa na mwendelezo mzuri. Fahamu zaidi.
1. PNC alianza muziki akiwa kwao Mwanza ambapo alirekodi kazi kadhaa ambazo zilimfanya kujulikana kwa kiasi Kanda ya Ziwa ambapo alikuwa anapewa show kama mmoja wa wasanii wa utangulizi katika matamasha makubwa.
Hata hivyo, ndoto yake kubwa ilikuwa ni siku mmoja aende Dar es Salaam ili arekodi katika studio kubwa kisha atoke kimuziki, na baadaye arejee Mwanza akiwa msanii mkubwa na maarufu ambaye anaweza kufanya show ya kuujaza uwanja wa CCM Kirumba.
2. Kuna rafiki yake naye alikuwa anafanya muziki, huyu jina lake ni Raja Computer ambaye alitangulia kwenda Dar es Salaam. Sasa akawa anamshawishi naye atinge katika jiji hilo ili kujaribu bahati yake, kitu ambacho PNC alikikubali, hivyo akafunga safari kutoka Mwanza hadi Dar.
3. Kufika Dar, Raja Computer akamkaribisha PNC katika familia ya Tip Top Connection ambayo wakati huo ilikuwa na wasanii wakubwa kama MB Dogg na Madee. Aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo marehemu Abdu Bonge alivutiwa sana na kipaji cha PNC na kuahidi kumshika mkono hadi afanikiwe kutimiza ndoto zake.
4. Akiwa anajitafuta, akakumbuka akiwa Mwanza alikutana na aliyekuwa DJ wa Clouds FM, Mully B ambaye alimueleza siku akifika Dar wawasiliane ili amsaidie kupiga hatua kimuziki. Basi PNC akaamua kumtafuta DJ Mully B na akampata.
5. DJ Mully B akampeleka PNC kwa muuza kanda (tape) za wasanii wakati huo, Mamu Store, msambazaji huyu pia aliona uwezo wa mwanamuziki huyo na kukubali kutoa fedha ili akarekodi huku akiwa na mkataba wa kufanya albamu moja. Wakati huu DJ Mully B akiwa ndiye meneja wake, kazi ikaanza lakini nyimbo zake mbili za mwanzo hazikufanya vizuri ila bado Mamu aliendelea kutoa fedha ya kurekodi kwa PNC akiwa na matumaini ipo siku yake.
6. Siku moja PNC akakutana na rafiki yake mmoja ambaye alikuwa redio ndogo ya CD, jamaa alikuwa anasikiliza nyimbo za mwanamuziki wa Marekani, Rayvon ambaye amezaliwa katika kisiwa cha Barbados, ambapo pia kazaliwa Rihanna.
7. Basi PNC akazipenda sana nyimbo za Rayvon, ila kuna mmoja ulimkosha zaidi, nao unaitwa Story of My LIfe (2002), ndipo akaamua kuiga melodi na midondoko (sampo) yake, vitu alivyokuja kuvitumia katika wimbo uliomtoa kimuziki, Mbona (2008).
8. Baada ya kupata maujanja kutoka kwa Rayvon, mara moja PNC akaenda studio ya MJ Records, akakutana na Bizman na kumtengemezea mdundo wimbo huo (Mbona). Akauchukua mdundo wake na kurudi nao Tip Top, kina Abu Bonge wakamuuliza anataka kumshirikisha nani humo?, ndipo akamtaja Mr. Blue.
Basi Mr. Blue akatafutwa na ngoma ikarekodiwa, na ndipo PNC akatoa na wimbo wake huo, Mbona (2008) lakini baadaye watu wakaanza kuhoji mbona kama unafanana na ule wa Rayvon, Story of My LIfe (2002)!, ila hapo tayari PNC ana jina mjini.
9. Katika video ya wimbo huo, Mbona (2008) iliyosimamiwa na Empty Soulz Production, PNC anaonekana akiwa amevalia tisheti za Tip Top Connection, hizi alihazima kutoka kwa Madee. Hata hivyo, PNC hakuwa msanii wa kundi hilo kama ilivyokuwa kwa kina Madee, bali yeye alikuwa mwanafamilia tu.
10. Wimbo huo ambao Master J alihusika upande wa mixing na mastering, ulichochea mauzo ya albamu yake, nakala za kwanza kwenda sokoni ziliuza Sh600,000 ambapo Mamu Store alichukua Sh200,000, huku PNC na meneja wake DJ Mully B wakigawana hiyo Sh400,000 iliyosalia. Mbali na ngoma hiyo, PNC alifanya vizuri pia kupitia wimbo wake ‘Nalia’ ambao pia ulitayarishwa chini ya MJ Records (Bizman na Master J), huku video yake ikiongozwa na Chapa Kazi Filmz, ambao walifanya vizuri sana wakati huo hasa upande wa video za Hip Hop.