Akilihutubia Baraza hilo, Khaled Khiari Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki ameonya kuwa mvutano wa hivi karibuni umeondoa umakini wa dunia kutoka hali halisi inayozidi kuwa mbaya katika eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel, huku mateso ya raia yakiendelea kwa kiwango kikubwa.

“Mvutano na mapigano yameelekeza umakini mbali na hali ya Palestina,” amesema. “Mbali na macho ya dunia, hali ya Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Yerusalemu Mashariki, inazidi kuwa mbaya.”

Picha ya Umoja wa Mataifa/Eskinder Debebe Khaled Khiari, Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki, akitoa taarifa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.

Ameongeza kuwa wakazi wa Gaza wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya mauti pamoja na uhaba mkubwa wa huduma muhimu kama chakula, maji safi, umeme na dawa. 

Katika Ukingo wa Magharibi, amebainisha kuwa vurugu za walowezi, ufurushwaji wa watu na upanuzi wa makazi mapya vinaongeza hali ya taharuki.

“Jamii nzima ziko hatarini, na matumaini ya suluhisho la mataifa mawili yanaendelea kudhoofika,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Gaza, takribani Wapalestina 800, wakiwemo watoto zaidi ya 200, wameuawa tangu usitishaji vita uanze. Wakati huo huo, watu milioni 1.8 wamekimbia makazi yao na wengi wanaishi katika mazingira magumu yasiyo na huduma za msingi.

Amesisitiza kuwa “Mipango ya misaada, uokoaji na ujenzi mpya lazima iharakishwe kwa dharura.”

Tathmini ya pamoja ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na Benki ya Dunia inaonesha kuwa zaidi ya dola bilioni 71 zinahitajika kwa ujenzi mpya wa Gaza katika muongo ujao.

Picha ya Umoja wa Mataifa/Eskinder Debebe Espen Barth Eide (kwenye skrini), Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway na Mwakilishi wa Kamati maalum ya Uunganisho, akitoa hotuba katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.

Wafadhili watakiwa kujiongeza 

Espen Barth Eide  waziri wa mambo ya nje wa Norway na mwenyekiti wa kamati amesema kuna maendeleo chanya katika juhudi za uratibu wa wafadhili, lakini bado kuna haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji.

“Tumepiga hatua katika kuhamasisha wafadhili kushirikiana kwa pamoja, lakini hatua zaidi zinahitajika ili kuleta mabadiliko halisi,” amesema.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo mipya ya utawala na taasisi zilizopo ili kuhakikisha uwazi na ufanisi katika utoaji wa misaada.

Ametoa wito kwa Hamas kuweka chini silaha na kwa Mamlaka ya Palestina kuendelea na mageuzi ya taasisi zake.

“Mpango wa vipengele 20 unategemea hatua hizi muhimu, zikiwemo dhamana, ufuatiliaji na hatua za kujenga imani,” amesema.

Ameitaka Israel kupunguza vizuizi vya usafiri na biashara, kusitisha upanuzi wa makazi na kuchukua hatua dhidi ya vurugu za walowezi.

Eide  ameongeza kuwa “Uwajibikaji ni msingi wa kurejesha imani na utulivu wa kudumu.” 

Picha ya Umoja wa Mataifa/Mark Garten Tony Blair Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na, mwanachama wa Bodi ya Utendaji wa Bodi ya Amani, akitoa hotuba katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.

Hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu Gaza

Tony Blair Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mjumbe wa Bodi ya Utendaji ya Amani, amesema dunia ipo katika wakati muhimu ambao utaamua mustakabali wa Gaza na eneo zima.

“Tumefikia hatua ya mabadiliko,” alisema akisisitiza umuhimu wa kuongeza ufadhili wa haraka kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na ujenzi mpya kupitia mifumo ya pamoja ya kimataifa.

Ameeleza kuwa mpango wa amani unahitaji Hamas kujiondoa katika utawala wa Gaza na kukubali mchakato wa kuondoa silaha.

“Hamas haiwezi kuwa sehemu ya utawala wa Gaza,” amesema.

Mpango huo unatoa uwezekano wa kuondoa vizuizi iwapo hatua za usalama zitatekelezwa kikamilifu.

Ameendelea kusema kuwa “Hii ni fursa kubwa kwa watu wa Gaza kupata nafuu na matumaini mapya”.

Hata hivyo, amekiri kuwa ukosefu wa imani kati ya pande husika ni changamoto kubwa, na hivyo kuhitaji kipindi cha mpito chenye uangalizi wa kimataifa.

Tunahitaji pande zote kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu na uwazi,” 

Bwana Blair ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utafungua njia ya msaada zaidi, huduma bora za afya, uhuru wa usafiri na hatimaye utulivu wa kudumu.

Amehitimisha tarifa yake kwa kusema kuwa “Gaza ni mtihani kwa wote  kubadilisha historia au kuirudia”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *