WAKATI Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga akieleza mkakati wa kuirejesha kwenye fomu timu hiyo, kiungo mshambuliaji kikosini hapo, Hassan Dilunga amekoleza utamu akitangaza kiama kwa mechi zilizobaki.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu, haijawa na matokeo mazuri licha ya jitihada za uongozi na mashabiki kuendelea kwa ajili kuiimarisha upya kuhakikisha haishuki daraja.

Timu hiyo iliyopo nafasi ya 14 katika msimamo na pointi 17, inajiandaa na mchezo ujao utakaopigwa Aprili 30 mwaka huu dhidi ya Mashujaa ukiwa wa kwanza kwa Kocha Mayanga aliyejiunga nao hivi karibuni kuchukua nafasi ya Mecky Maxime.

DILU 02

Akizungumza na Mwanaspoti, Dilunga amekiri kuwa presha ni kubwa kwa wachezaji na mashabiki kutokana na matokeo waliyonayo, lakini kwa mkakati wao wa sasa hawaoni kitakachowakwamisha kutoboa.

Amesema kwa mechi 11 zilizobaki, wanahitaji pointi tatu kila dakika 90 akieleza kuwa hilo ni jukumu na wajibu wao wachezaji akieleza kuwa licha kukaa nafasi waliyopo haijaachana sana na waliopo juu yao.

“Tunajua mashabiki hawajafurahia kwa matokeo tuliyonayo, lakini niwatoe hofu kwamba sisi wachezaji tuko imara na wajibu wetu ni kupambania timu kuhakikisha inabaki salama Ligi Kuu.

“Kwa sasa tupo nafasi ya play off, ila tukiangalia waliopo juu yetu hawajatuacha sana pointi, kazi yetu ni kila mchezo kuchukua pointi tatu ili kufikia malengo, lolote linawezekana,”  amesema Dilunga.

DILU 01

Nyota huyo aliyewahi kukipiga Simba na JKT Tanzania ameongeza kuwa ligi ni ngumu haswa kwa mechi zilizobaki akiwaomba wenzake kikosini kuongeza nguvu na kujiamini kuhakikisha hawashushi timu hiyo.

Kwa upande wake kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga, amesema anahitaji nidhamu ya kupambana kwa wachezaji akisisitiza kuwa matarajio yake ni kuona City ikirejesha ubora wake Ligi Kuu.

“Sina maajabu yoyote bali nakuja kuendeleza pale walipoishia wenzangu, hii dhamana waliyonipa viongozi kwa kuniamini nitapambana kutowaangusha,”  amesema kocha huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *