
Dar es Salaam. Katika makala ya jana tuliona namna wajawazito wanavyotozwa fedha kupata matibabu, licha ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 kuelekeza kundi hilo kupata huduma hiyo bila malipo.
Gharama hizo wanazotozwa wajawazito hutofautiana, wapo wanaoeleza kulipa Sh15, 000 na wengine Sh30,000 ili kupata matibabu jambo ambalo kwao ni kikwazo cha huduma.
Pia, wanapokwenda kujifungua hutakiwa kubeba pamba, dawa za kuua vijidudu, glovu, sindano na plastiki za kujifungulia.
Hayo yanatokea wakati Sera ya Afya 2007, kifungu cha 5.3.4 (c)(i)), kinaeleza Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi isiyotoa huduma kwa faida na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto chini ya miaka mitano.
Kifungu cha 5.4.8.3, sera inabainisha wajawazito ni miongoni mwa makundi maalumu ambayo Serikali inatambua hayana uwezo au hayapaswi kuchangia gharama za huduma za afya.
Lengo la msamaha huo ni kuwezesha makundi haya kupata huduma bora sawa na wananchi wengine.
Katika kusisitiza hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi baada ya kukagua soko na stendi Bunju B, jijini Dar es Salaam, Desemba 29, 2025 amesisitiza utekelezaji wa sera hiyo akisema:-
“Mjamzito akishafika Hospitali asisubirishwe, sijui lete beseni, lete ndoo, afikishwe kwenye matibabu moja kwa moja, kila hospitali iwe na mambo haya kwa ajili ya kusaidia Watanzania, masuala ya uzazi sio dharura, tunajua watoto wanakuja na nchi hii ni tajiri, haiwezi kukosa ndoo ya kumhudumia mama mmoja masikini,” alisema.
Ili kuwa na mafanikio katika utekelezaji wa sera hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Tanzania (Aphta), Dk Samwel Ogilo anasema ni lazima matibabu kwa watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wasiokuwa na uwezo.
Pia, ni lazima sera itafsiriwe na iwe sheria, sheria iwe na miongozo na bajeti.
“Kwa hiyo sera kuhusu suala hili, bado utekelezaji wake haujakamilika, wakuu wa vituo hupata fedha kutoka serikalini, na halmashauri husika iweke bajeti; kama mkuu wa hospitali hana bajeti kwa makundi haya, hawezi kutekeleza,”anasema.
Dk Ogillo anasema kwa sekta binafsi, ili itekelezwe, inabidi halmashauri ziingie mikataba na hospitali husika na ziwatengee bajeti kwa ajili hiyo, na fedha zitolewe kwa wakati; bila hayo kufanyika sera haitaweza kuwahusu sekta binafsi.
“Sababu Serikali kwa sasa inakumbana na tatizo la kutokuwepo kwa bajeti ya uhakika kwa makundi haya maalumu, naona njia ya uhakika ni kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote,” anasema.
Mfuko wa uzazi
Mtaalamu wa Afya, Alex Mlwisa anasema suluhu kubwa ya kuepukana na vifo visivyo vya lazima ni kuanzisha mfuko wa uzazi.
“Mfuko huu unachangiwa na mwananchi mwenyewe tangu atakapokuwa ameanza kliniki, kwani uzazi si wa siku moja ni miezi saba hadi tisa. Mfuko uitwe uzazi funds utasaidia mno. Lakini pia, Serikali itenge bajeti ya kusaidia mfuko huo na hili naamini linawezekana,”anasema.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Nkoronko Mugisha anasema huduma za afya ni gharama, lazima mnyororo wa upatikanaji wa huduma hizi ugharamiwe.
Anasema ni lazima mgharimiaji aweke mfumo thabiti unaofanikisha matamko ya kisera kwa kuwa, kumekuwa na udhaifu katika utekelezaji kwa vitendo.
Kuhusu mkwamo wa matibabu bure kwa wajawazito, Mtaalamu wa Afya, Dk Ernest Winchislaus anasema Tanzania haina sheria mahsusi inayotamka wazi huduma zote za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ni bure, kama haki inayolindwa moja kwa moja na sheria.
“Kile kilichopo kwa sasa ni Sera ya Afya ya Taifa na miongozo ya kiutendaji ya Wizara ya Afya inayotoa msamaha wa malipo kwa makundi haya, pamoja na sheria pana kama sheria ya mtoto inayotambua haki ya mtoto kupata huduma za afya na mifumo ya bima ya afya inayolenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi,” anasema.
Hata hivyo, anasema sera na miongozo havina nguvu sawa na sheria; haviweki wajibu wa moja kwa moja unaoweza kudaiwa kisheria pale huduma inaponyimwa au malipo yanapotozwa.
Kutokana na kukosekana kwa sheria, Dk Winchislaus anasema ndio maana utekelezaji wa sera hutofautiana kati ya vituo na maeneo, hasa pale rasilimali zinapokuwa finyu.
“Kwa mtazamo wa uchambuzi wa afya ya umma, pengo hili la kisheria lina athari za moja kwa moja kwa usalama wa mama na mtoto.
“Kukosekana kwa sheria mahsusi kunafanya huduma hizi kutegemea zaidi uamuzi wa kiutawala badala ya wajibu wa kisheria, hali inayoweza kuchelewesha huduma muhimu za ujauzito, kujifungua na matibabu ya watoto wadogo,” anasema.
Anasema kuweka huduma za kundi hilo kwenye msingi wa sheria kungeimarisha uwajibikaji, kuweka viwango vinavyofanana kitaifa na kulinda kaya masikini dhidi ya gharama zisizotarajiwa za afya.
“Kwa hiyo, mjadala wa kuwepo kwa sheria inabidi utazamwe kama hatua ya kitaalamu ya kuimarisha mfumo wa afya, kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika; na kuhakikisha ulinzi wa wajawazito na watoto wadogo unakuwa haki inayotekelezeka.
“Si dhamira ya sera pekee; na mpango unaendelea kuandaliwa wa Bima ya Afya kwa Wote, iwapo utatekelezeka kwa ufasaha unaweza kuwa mojawapo ya suluhisho kubwa la suala hili,” anasema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema kwa sasa kinachotajiwa ni ujio wa Bima ya Afya kwa Wote.
“Hatutarajii kuwa na mgawanyo wa kusemekana wazee, wajawazito au watoto wapate matibabu bure hivi ni vitu vidogo, hatutarajii kiongozi wa Taifa aruhusu maiti kutoka hospitali bila kulipiwa kama fursa kwake kisiasa.
“Tunapokuja kwenye suala la Bima ya Afya kwa Wote ni jambo linalopaswa kuwa ni la watu wote bila kujali makundi maalumu,”anasema.
Anasema jambo linalopaswa kuhojiwa sasa ni namna ambavyo Serikali imejipanga kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote bila kuwepo kwa malalamiko kwa wananchi.
Pia, anahoji ni kwa namna gani Serikali imejipanga kutoa ruzuku kwenye bima ya afya na sekta binafsi kushirikishwa kwenye mfumo huo.
Itaendelea kesho