
Kilwa. Tangu mwaka 2020 wakazi wa Njinjo walikuwa wanapata changamoto ya huduma za afya na kuwalazimu kutembea umbali wa kilomita tano kufuata huduma hizo katika Zahanati ya Miguruwe au Zahanati ya Kipindimbi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Scola Alex mkazi wa Njinjo amesema kuwa ujio wa zahanati hiyo umekuja kuondoa changamoto waliyokuwa wanaipata kwa muda mrefu na kuishukuru Serikali pamoja na wananchi kujitoa katika kuchangia ujenzi wa Zahanati hiyo.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuliona hili kwani wametuondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya katika kijiji cha Miguruwe.”amesema Alex.
Tulia Ndepei amesema kuwa zahanati ya awali ilisombwa na mafuriko yaliyotokea mwaka 2020, hali iliyowalazimu wananchi hao kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
“Tunashukuru kwa kusogezewa huduma hii muhimu hapo awali tulikuwa tunapata shida kubwa kutokana na umbali mrefu wa kufuata matibabu,” amesema Tulia.
Naye Dk.Essau Chomola akizungumza jana Jumatatu Aprili 27, 2026 mara baada ya kuzunduliwa kwa Zahanati hiyo na Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa Wazo Wang’onda,amesema kuwa Zahanati hiyo itawanufaisha wakazi zaidi ya 2000,huku hadi kumalizika kwake imegharimu kiasi cha Sh200milioni.
Dk. Chomola, amesema kabla ya ujenzi huo wakazi wa Njinjo walikuwa wakifuata huduma katika kijiji cha Kipindimbi au Kijiji cha Miguruwe, kilichopo umbali wa takriban km sita, kwa gharama ya usafiri ya Sh4000.