Dar es Salaam. Kifo cha msanii mkongwe wa filamu nchini, Hashim Kambi, kimeacha simanzi nzito kwa familia, wasanii na mashabiki wa tasnia ya burudani baada ya kudondoka ghafla Aprili 27, 2026 jijini Dar es Salaam.
Katika mahojiano na Mwananchi, msemaji wa familia Mwita Abubakari Kambi ambaye pia ni mdogo wa marehemu, amefunguka kuhusu dakika za mwisho za maisha ya ndugu yake, historia yake na namna mazishi yatakavyofanyika.
Kutoka Tabora hadi kuanguka ghafla
Mwita anasema siku ya mauti ilianza kama siku ya kawaida, bila dalili yoyote kubwa ya hatari.
Mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Hashim Kambi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
“Hashim alifika Dar es Salaam Aprili 27 asubuhi kabisa akitokea Tabora. Alipofika nyumbani hakupata hata muda wa kupumzika, akaanza kukimbilia majukumu yake ya sanaa. Ukweli ni kwamba alikuwa na presha, alitakiwa kupumzika lakini akaamua kuwahi kazi,” anasema Mwita.
Anaendelea kueleza kuwa, wakati akiwa katika harakati hizo za kikazi akiwa na wenzake, ndipo alianza kujiskia vibaya.
“Ghafla wenzake wakamuona anaanguka. Ilikuwa ni hali ya kushitukiza sana, kwa haraka huwezi kusema sababu halisi, kwa sababu hakuwa amelazwa hospitali wala kuonesha dalili kubwa kabla, inaonekana ni uchovu na presha,” anasema.
Kwa mujibu wa Mwita, juhudi za kumuwahisha hospitalini hazikuzaa matunda.
“Wakati wanamkimbiza hospitali tayari alikuwa ameshafariki palepale alipoanguka. Walimbeba kumpeleka Hospitali ya Mico iliyopo Sinza, lakini ukweli ni kwamba alikuwa tayari ameshapoteza maisha,” anasema.
Ratiba ya mazishi na taratibu zilizopangwa
Familia imeweka wazi ratiba kamili ya kumuaga marehemu, ikiwataka watu wote kushiriki kwa pamoja katika ibada na mazishi.
“Tararibu zote zitafanyika Aprili 28, 2026, kuosha na dua ni kuanzia saa nane hadi saa katika Msikiti wa Maamur, Upanga. Baada ya hapo, mazishi yatafanyika saa kumi jioni katika makaburi ya Kisutu,” anafafanua Mwita.
Mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Hashim Kambi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Anaongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa msikitini na hautapelekwa nyumbani.
“Mwili upo Msikiti wa Maamur na hautaletwa nyumbani. Kila kitu kitafanyika hapo msikitini, kisha tutaenda moja kwa moja makaburi ya Kisutu. Baada ya mazishi, familia itarudi nyumbani kuendelea na matanga,” anasema.
Kwa nini msiba umewekwa kwa mtoto wake Lulu
Mwita pia alieleza sababu za familia kuamua msiba uwe nyumbani kwa mtoto wa marehemu Lulu, eneo la Tabata Kimanga.
“Tumeamua msiba uwe kwa mtoto wake Lulu ili kumpa nafasi mtoto. Yeye mwenyewe aliomba, anasema siku za mwisho alikuwa na baba yake karibu sana na walikuwa wanashauriana mambo mengi. Hata alimwambia akifa, asisafirishwe bali azikwe pale pale alipo,” anasema.
Anaongeza kuwa pia waliona ni vyema zaidi kufanikisha ibada kwa urahisi.
“Tumeona pia ni rahisi watu wengi kukutana msikitini kwa ajili ya ibada. Ingawa kuswalia nyumbani ni suna, lakini msikiti ni sehemu tukufu zaidi kwa jambo kama hili,” anasema.
Historia ya maisha kutoka soka hadi filamu
Mbali na sanaa ya filamu, Hashim Kambi alikuwa na historia kubwa katika michezo, hasa soka.
Mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Hashim Kambi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
“Alizaliwa Morogoro na kusomea huko huko. Kabla ya kuingia kwenye filamu, alikuwa mchezaji wa mpira katika timu ya Jogoo ya Morogoro.
Baadaye akachukuliwa na Yanga African, akicheza nafasi ya namba tano pamoja na kina Selemani Jongo,” anasimulia Mwita.
Anaendelea: “Alicheza Yanga kuanzia mwaka 1978 hadi 1980. Mimi ndiye niliyemleta Dar es Salaam mwaka 1977, akawa anaishi Magomeni kwa baba yangu ambaye yeye anamuita baba mdogo.”
Familia na maisha binafsi
Katika maisha yake, marehemu ameacha watoto watatu na historia ya ndoa tofauti.
“Alioa mke wa kwanza hapa Dar es Salaam na kupata watoto wawili, Shamimu na Mohamed. Baadaye mwaka 1989 nikamuozesha mke wa pili Arusha, wakapata mtoto mmoja Lulu. Walikuja kuachana, akakaa muda mrefu bila mke, kisha mwaka 2022 nikamuozesha tena mke wake wa sasa, ingawa hawakupata mtoto,” anasema.
Utu wake na pengo aliloacha
Mwita anamkumbuka kaka yake kama mtu wa watu na mwenye upendo mkubwa kwa jamii.
“Hashim alikuwa mtu wa watu, mcheshi, na aliyependa kujichanganya na kila mtu. Alikuwa hana makuu kabisa,” anasema.
Msanii mkongwe wa filamu nchini, Hashim Kambi enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Anasisitiza kuwa pengo aliloacha ni kubwa sana kwa familia.
“Kwa sasa yeye ndiye alikuwa mkubwa wetu, hivyo kuondoka kwake ni pengo kubwa sana ambalo si rahisi kuziba,” anasema.
Urithi wa familia na uamuzi wa maziko Dar
Familia pia imeamua mazishi yafanyike Dar es Salaam badala ya Morogoro, kutokana na historia ya kifamilia.
“Baba yetu mzazi alifariki mwaka 1995 na alizikwa Magomeni, Dar es Salaam. Hata marehemu mwenyewe alikuwa na msimamo kuwa akifa azikwe hapa Dar. Hivyo tumefuata wosia wake,” anafafanua Mwita.
Katika kipindi hiki kigumu, Mwita anasema familia imefarijika na ushirikiano kutoka kwa wasanii.
“Tunashirikiana vizuri sana na wasanii katika maandalizi yote ya mazishi. Wamekuwa bega kwa bega nasi tangu mwanzo,” anasema.
Kifo cha Hashim Kambi kimeacha majonzi makubwa. Lakini simulizi ya maisha yake inaacha alama ya mtu aliyegusa maisha ya wengi, kuanzia uwanjani hadi kwenye tasnia ya filamu na zaidi katika mioyo ya waliomfahamu.