Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kukuza biashara za taifa la Belarus ili kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 28,2025 katika mkutano wa kibiashara uliowakutanisha wadau kutoka Tanzania na Belarus, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk Latifa Khamis amesema ushirikiano huo utajengwa kwa karibu na taasisi inayosimamia ukuzaji wa mauzo ya nje ya Belarus kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya biashara.
Amesema kupitia ushirikiano huo, TanTrade itaweka mkazo katika kuwafungulia wafanyabiashara wa Tanzania njia za kuingia kwenye masoko mapya pamoja na kujenga daraja la mafanikio litakalowezesha kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuvutia fursa za biashara na uwekezaji zitakazowanufaisha wafanyabiashara na uchumi wa nchi kwa ujumla. Amesema kuwa wafanyabiashara wa Tanzania wanakwenda .bali lakini hawajafanya vizuri nchini Belarus ina fursa nyingi ikiwamo teknolojia katika kilimo, Tehama na katika afya ambapo wameendelea sana. “Wafanyabiashara wa Tanzania waanze kuifikiria sasa Beralus kibiashra na wenyewe si wachoyo wapo tayari kutupatiq teknolojia yao na kufungua milango ya kufanya nao biashara,”amesema Dk Latifa.
Akizungumza baada ya kutembelea TanTrade, Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Masoko cha Belarus, Mikalai Barysevich amesema ziara hiyo imelenga kuongeza uelewa wa pande zote kuhusu fursa zilizopo na namna ya kukuza biashara ya moja kwa moja kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo.
Amesema kuna nafasi kubwa ya kuendeleza biashara na kupanua uwekezaji wa pamoja, akisisitiza kuwa hatua ya kwanza ni kwa mataifa hayo kufahamiana zaidi kuhusu bidhaa, huduma na teknolojia zinazopatikana kwa kila upande.
Barysevich amesema jukumu la taasisi za kukuza biashara ni kusaidia wafanyabiashara kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja yatakayorahisisha utendaji wao na kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi.
Ameeleza kuwa Belarus imefika Tanzania ikiwa na moyo wa wazi na utayari wa kushirikiana, akibainisha kuwa nchi hiyo ipo tayari kwenda mbali katika ushirikiano huo kulingana na utayari wa Tanzania.
Aidha, amesema Belarus ina fursa nyingi katika uzalishaji wa bidhaa pamoja na teknolojia ambazo ipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.