Dar es Salaam. Mwanahawa Selemani ambaye ni mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa Bongo Fleva, marehemu Ramadhan ‘Spack’, ameeleza alivyozungumza na mwanae kwa mara ya mwisho. Huku akisema vipimo vimeonesha msanii huyo hakuumwa chochote

Akizungumza na Mwananchi mama huyo amesema alizungumza na Spack juzi akiulizia hali za wajukuu wake

“Mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa juzi usiku tulizungumza kuanzia saa 1 mpaka saa 4 usiku. Asubuhi jana ndio nikapigiwa simu kwamba amefariki sikuambiwa kama alikuwa anaumwa au amepata tatizo gani.

Mama mzazi wa mwanamuziki Spack akiwa msibani nyumbani kwake Chamazi 

“Tuliongea tuu mambo mazuri kuhusu maendeleo ya watoto wake shule hakuna kingine ni mtu ambaye alikuwa anawapenda watu wake. Kwasababu wengine nakaa nao mimi kwangu.”

Akizungumza kuhusu chanzo cha kifo cha mwanawe, Mwanahawa ameeleza mpaka umauti unamfikia mtoto wake hakuwa akiugua wala kuwa na changamoto yoyote ya kiafya.

“Mpaka umauti wake umemfikia sijajua alichuogua sijasikia ugonjwa nimesikia tu umauti. Hajawahi kunambia kama anachangamoto yoyote zaidi ya kusema kusumbuliwa na homa za kawaida kama kichwa na mafua. Vipimo vya madaktari vinaeleza kwamba hakuna tatizo ambalo wameliona. 

“Spack ameacha watoto watano. Alikuwa mtoto wa tatu kwangu ni mtoto wa pekee sana unachoongea anakusikiliza kama mama kaongea nini,” amesema.

Picha ya mwanamuziki Spack enzi za uhai wake

Aidha ameongezea; “Ameacha pengo kubwa sana kwa sababu yeye ni mtoto wangu wa kwanza wa kiume ameniachia pengo kubwa ambalo sitokuja kusahau kwenye maisha yangu,” ameeleza.

Hatahivyo katika msiba huo  mwanamuziki Madee amekabidhi  rambirambi kwa niaba ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda.

Akikabidhi fedha hizo bila kutaja kiasi, mwanamuziki Madee  amesema serikali imetoa pesa hizo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mazishi za msanii huyo.

“Nimepewa salamu kutoka kwa Paul Makonda ambaye ni Waziri anayehudumu eneo letu. Yeye ametupa kiasi kidogo cha fedha kitakachosaidia kuendesha mazishi ya Spack mpaka yatakapo tamatika,” amesema Madee.

Spack alifariki dunia jana Aprili 27, 2026 anatarajia kuzikwa kesho Jumatano Aprili 29, 2026 mkoani Tanga majira ya saa 10 jioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *