Dar es Salaam. Tanzania na Belarus zimeingia katika hatua mpya ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kufuatia mazungumzo yaliyogusa maeneo saba ya kimkakati, yakiwemo kilimo, nishati, afya, elimu, biashara na utalii.
Hatua hiyo imeelezwa leo Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov.
Waziri Ryzhenkov aliwasili nchini Aprili 27, 2026 kwa ziara ya siku tatu kufuatia mwaliko wa Waziri Kombo, na anatarajiwa kukutana na viongozi wengine wa Serikali kwa lengo la kuendeleza na kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Kombo amesema miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na uwakilishi, pamoja na kupunguza urasimu unaoweza kuathiri biashara na uwekezaji.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Dar es Salaam.
“Nimependekeza Serikali ya Belarus kuanzisha ubalozi kamili hapa nchini. Hatua hiyo itakuwa chombo muhimu katika kukuza diplomasia ya uchumi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya pamoja kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Ameeleza kuwa jambo lingine ni kukamilisha mikataba ya kimkakati kupitia mapitio ya maendeleo ya hati za makubaliano (MoU) ambazo ziko katika hatua za mwisho za kukamilishwa.
Miongoni mwa nyaraka hizo ni rasimu ya mkataba wa kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Biashara na Ushirikiano wa Kiuchumi, pamoja na mpango wa msamaha wa viza kwa wenye pasi za kidiplomasia na za utumishi, hatua itakayochochea ushirikiano wa pande zote.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Kombo amesema Tanzania imeikaribisha Belarus kuwekeza katika uunganishaji wa matrekta, uzalishaji wa mbolea na uhamishaji wa teknolojia za kisasa za umwagiliaji ili kuongeza tija na thamani ya mazao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Dar es Salaam.
Katika sekta ya nishati na miundombinu, amesema wameialika Belarus kushiriki katika uwekezaji na utoaji wa huduma za kihandisi, hasa katika uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi, pamoja na nishati jadidifu na uimarishaji wa miundombinu ya gesi ya ndani.
Aidha, Kombo amesema Tanzania imepokea nia ya kampuni ya BELPHARMPROM kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) katika uzalishaji na usambazaji wa vifaa tiba, hatua itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
Katika sekta ya elimu, Kombo ameishukuru Belarus kwa kuendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, hususan katika fani ya tiba kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Amesema ushirikiano huo utaongezwa zaidi kwa kujumuisha fani za uhandisi, sayansi ya data na akili unde, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kitaaluma kati ya taasisi za elimu ya juu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na vyuo vikuu vya Belarus.
Kuhusu utalii, Kombo amesema kuna ongezeko la idadi ya watalii kutoka Belarus wanaotembelea Tanzania, ambapo zaidi ya watalii 6,000 wamewasili nchini katika miaka ya hivi karibuni.
“Ili kuendeleza mwelekeo huo chanya, tunaendelea na jitihada za kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya nchi zetu, hatua itakayorahisisha usafiri na kuchochea zaidi sekta ya utalii,” amesema.
Katika nyanja ya biashara, amesema Serikali imejipanga kushughulikia changamoto ya uwiano wa biashara kwa kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Belarus, hususan kahawa, parachichi na maua.
Kwa upande wake, Waziri Ryzhenkov amesema mazungumzo hayo yamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano na kuonyesha uwezo mkubwa wa mataifa hayo mawili kujenga maendeleo ya pamoja.
“Tumejadili kwa uwazi hali ya mahusiano yetu pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu,” amesema.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo akiwa na Waziri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus, Maxim Ryzhenkov Habari Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika kilimo, teknolojia na biashara ni nguzo muhimu zitakazosaidia kukuza uchumi wa Tanzania na Belarus, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora ya kisheria na kifedha ili kuhakikisha ushirikiano huo unaleta matokeo yenye tija kwa wananchi.
Ryzhenkov amesema Belarus inatarajia kuwapokea maafisa na wafanyabiashara wa Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya kilimo mwaka 2026, pamoja na kuendeleza ushirikiano wa elimu kupitia kubadilishana wanafunzi, wataalamu na kushiriki katika tafiti na mikutano ya kisayansi.