Dar es Salaam. Wakati Tanzania na Uganda zikiingia makubaliano (MoU) kushirikiana katika sekta ya utalii, wadau wa sekta hiyo nchini wameomba kuboreshwa kwa miundombinu ili kuwezesha maeneo ya utalii kufikika kwa urahisi.
Wamesema vivutio vya utalii katika maeneo mbalimbali nchini ni vingi, lakini vingi vinashindwa kufikika kwa urahisi kutokana na changamoto ya miundombinu.
Wakizungumza katika mkutano wa waendesha utalii kutoka nchi mbalimbali za Afrika uliokwenda sanjari na kusaini MoU leo Aprili 28, 2026 jijini Dar es Salaam wadau hao wamesema pamoja na kuwepo kwa vivutio vingi vya kipekee, bado kuna changamoto ya miundombinu isiyofikika kwa urahisi nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo amesema wao kama wadau wa utalii walikuwa tayari kwa ushirikiano huo muda mrefu, mpango ambao utakuza na kufungua fursa mbalimbali katika sekta ya utalii.
Amesema wakati makubaliano hayo yanakwenda kuiuza biashara ya utalii na kuongeza muda wa mtalii kukaa Afrika mashariki, ameshauri Serikali pia iwekeze katika miundombinu ili maeneo yote mazuri ya utalii nchini yafikike kwa urahisi.
“Malii akitaka kwenda Serengeti, basi aende kwa urahisi, akitaka kwenda Uganda kuangalia Gorilla aende kwa urahisi, Tanzania tuangalie tunafanyaje hili huyu mgeni akija basi aje kwa urahisi na atalii kwa urahisi” amesema.
Amesema mtalii anapokuja nchini anakuja kupumzika hatakiwi kusafiri kwa saa 6 ili kufanya utalii.
“Mfano mdogo ni wa kutoka Arusha hadi Selous, unatumia saa sita, huu ni muda mwingi, mtalii atumie saa moja kufika, nchi ifanye uamuzi wa kuboresha miundombinu,” amesema.
Ameshauri kwa kuwa karibu asilimia 30 ya ardhi ya Tanzania ni eneo la mali asili, basi mipango na sera ya nchi iangalie ni namna gani wataboresha miundombinu kama ni kwa kujenga reli ya mwendokasi (SGR) au kununua ndege ili kuweka mazingira rafiki ya kuvifikia vivutio vyote vya utalii kwa haraka.
“Afrika Mashariki ni kubwa, siyo kama Europe (Ulaya) kwamba mtu utatoka Paris kwenda Barcelona kuangalia mpira na kurudi, lakini tukiwa na miundombinu inayofikika kwa urahisi, itafungua fursa zaidi, ” amesema.
Amesema makubaliano ya kushirikiana katika sekta hiyi itawaunganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki hivyo mtalii kuongeza muda wake wa kuwa Afrika Mashariki bila kujali yupo nchi gani na kutaongeza fursa ikiwamo za ajira.
Akizungumzia katika ufunguzi wa mkutano huo uliolenga kujadili fursa za pamoja na namna ya kukuza sekta hiyo kupitia ushirikiano wa karibu zaidi, Naibu Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Balozi Elizabeth Allimadi aliwahimiza Watanzania kushirikiana na waendesha utalii wa Uganda ili kuimarisha biashara hiyo.
Amesema ushirikiano huo utawezesha kampuni za utalii kutoka nchi hizo mbili kufanya kazi kwa pamoja na kunufaika na soko pana la kimataifa.
Makamu wa rais wa Bodi ya Utalii Kusini mwa Afrika, PAN Africa, Andreas Simion amesema ushirikiano huo utawezesha waendesha utalii kuuza vivutio vya ukanda wa Afrika Mashariki kama kifurushi kimoja (package), badala ya kila nchi kujitangaza kivyake.
“Mpango huu ni mzuri na unalenga kuongeza mvuto wa ukanda wa Afrika Mashariki kwa watalii wa kimataifa, kwa kuwapa fursa ya kutembelea nchi zaidi ya moja kwa safari moja, hatua itakayoongeza ushindani dhidi ya masoko mengine ya utalii duniani,”amesema.
Amesema pia utaondoa changamoto za waendeshaji utalii wa Tanzania na Uganda na yeye kutoa wito kwa serikali zote kuimarisha miundombinu katika sekta za utalii.