Tathimini mpya mpya iliyotoleqa leo na shirika hilo inaonesha hali mbaya,ambapo hadi walimu wanawake 20,000 na wahudumu wa afya 5,400 wanaweza kuondoka katika sekta hizo hali itakayodhoofisha mifumo ya elimu na afya ambayo tayari iko katika hali tete.

Afghanistan haiwezi kumudu hasara hii

Kiini cha tahadhari hiyo kwa mujibu wa UNICEF ni mgogoro unaoongezeka wa rasilimali watu, ambapo wasichana wanazuiwa kupata elimu huku wanawake waliobobea wakiondoka kazini.

“Afghanistan haiwezi kumudu kupoteza walimu, wauguzi, madaktari, wakunga na wahudumu wa kijamii wa baadaye, ambao ndio wanaobeba huduma muhimu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell na kuongeza kuwa “Hili ndilo litakalotokea ikiwa wasichana wataendelea kunyimwa elimu.”

Ametoa wito kwa mamlaka husika, “Tunawasihi viongozi waliopo kuondoa marufuku ya elimu ya sekondari kwa wasichana na tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono haki ya wasichana ya kujifunza.”

Wasichana milioni moja tayari wamezuiwakusoma

Tangu marufuku ya elimu ya sekondari kwa wasichana ilipoanzishwa mwaka 2021, zaidi ya wasichana milioni moja wamekosa haki yao ya kupata elimu.

Ikiwa hali itaendelea hadi 2030, UNICEF inasema idadi hiyo inaweza kuzidi milioni mbili na kuongeza pengo la usawa katika nchi ambayo tayari ina viwango vya chini vya usomaji kwa wanawake.

Shule tayari zinaathirika. Idadi ya walimu wanawake katika elimu ya msingi imeshuka kwa zaidi ya asilimia 9 kutoka takriban waalimu 73,000 mwaka 2022 hadi karibu 66,000 mwaka 2024.

Mfumo wa afya unakabiliwa na shinikizo

Kwa mujibu wa tathimini hiyo ya UNICEF athari hazipo tu katika elimu bali pia katika huduma za afya.

UNICEF inaonya kuwa kuondolewa kwa wanawake katika sekta za elimu na afya ambapo bado wanaruhusiwa kufanya kazi kutakuwa na athari za moja kwa moja kwa maisha ya watu.

Katika jamii nyingi nchini humo, mila na desturi huzuia wanawake kupokea huduma kutoka kwa wahudumu wa afya wanaume, hivyo kupungua kwa wahudumu wa afya wanawake kutapunguza upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama, mtoto mchanga na watoto.

Gharama za kiuchumi zinaongezeka

Vikwazo hivi pia vinaathiri uchumi kwa kiasi kikubwa imesema tathimini hiyo.

Afghanistan tayari inapoteza takriban dola milioni 84 kila mwaka kutokana na kuwanyima wanawake na wasichana fursa za elimu na ajira hasara ambazo zinaendelea kuongezeka kadri muda unavyopita.

Wakati huo huo, tathimini imeeleza kuwa uwakilishi wa wanawake katika utumishi wa umma umeshuka kutoka asilimia 21 mwaka 2023 hadi asilimia 17.7 mwaka 2025.

© UNICEF/Shehzad Noorani Wasichana wakisoma vitabu vyao vya kiada katika Kituo cha Elimu cha Dasht-e-Barchi huko Kabul, Afghanistan. (Maktaba)

Mgogoro wa pande mbili kwa mustakabali

Ripoti inaeleza hali hiyo kama “mgogoro wa pande mbili”, nchi inapoteza wataalamu wanawake waliopo huku kizazi kipya kikizuiwa kuchukua nafasi zao.

Kila mwaka wa kuchelewa unaongeza pengo hilo imebainisha tathimini.

“Kuwanyima wasichana wa Afghanistan elimu ya sekondari ni kulinyima taifa zima uwezo wake,” ameonya Russell.

Ameongeza kuwa hatua hiyo “Inawafungia wasichana, familia zao na jamii zao katika umaskini, inadhoofisha afya, na inazima injini ya kiuchumi ambayo wanawake walioelimika wangeweza kuiendesha.”

Juhudi zinaendelea licha ya vikwazo

Licha ya changamoto hizo, UNICEF inaendelea kusaidia elimu nchini Afghanistan.

Mwaka 2025 pekee:
  • Zaidi ya watoto milioni 3.7 walipokea msaada wa dharura katika shule za umma
  • Watoto 442,000 na asilimia 66 miongoni mwao wasichana walinufaika na programu za elimu za kijamii
  • Shule 232 zilijengwa au kukarabatiwa

Wito wa hatua za haraka

UNICEF inatoa wito wa hatua za haraka kurejesha haki ya wasichana kupata elimu ya sekondari na ya juu, huku ikiendeleza uwekezaji katika elimu ya msingi.

Imesema hatua hizi ni muhimu kwa mustakabali wa afya, elimu na uchumi wa Afghanistan.

Bila hatua za haraka, nchi hiyo iko katika hatari ya kupoteza si tu maelfu ya wataalamu bali pia uwezo wa kizazi kizima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *