Mwaka 2005, tahadhari ya kwanza ya UNICEF ilionya kuwa watoto wa Darfur walikuwa wanakabiliwa na mustakabali usio na uhakika. Miaka 20 baadaye, huku mgogoro mpya ukiingia mwaka wake wa nne, watoto tena wamekwama katika janga la kibinadamu. 

Kwa mujibu wa UNICEF wasichana na wavulana wameshuhudia shule zao zikiharibiwa, jamii zao kushambuliwa, na haki zao kukiukwa waziwazi. Wengi wameshuhudia mauaji, kupoteza wazazi, na mamilioni wamelazimika kuhama makazi yao.

Hali hii ni mtihani kwa jumuiya ya kimataifa iwapo haitachukua hatua madhubuti zaidi si tu kulinda watoto, bali pia kuvunja mzunguko wa mateso uliokwisha kuharibu utoto wa wengi.

© UNOCHA/Giles Clarke Wakimbizi wa Sudan, wengi wao ni wanawake na watoto, wanasimama kwenye foleni ya chakula katika eneo la usambazaji la jikoni ya jamii ya Save the Children katika kambi ya Daba Naira huko Tawila.

Nini kinaendelea Darfur?

Katika maeneo yote ya Darfur, janga kubwa la kibinadamu linaendelea, njaa kali, utapiamlo unaoongezeka, huduma za afya zilizoporomoka, na upatikanaji duni wa maji safi na usafi wa mazingira imesema tahadhari hiyo. 

Migogoro imeharibu vyanzo vya kipato na mifumo ya chakula, na kusukuma jamii kuelekea baa la njaa. Maelfu ya watoto wanaoishi katika makambi ya wakimbizi wa ndani wako katika hatari kubwa ya maisha.

Pia tahadhari imebainisha kuwa vituo vingi vya afya vimeharibiwa, kuporwa au kufungwa. Darfur Kaskazini pekee, vituo 35 vya afya vimeshambuliwa tangu mwaka 2023, ikiwemo hospitali kuu ya uzazi huko Al Fasher

Wahudumu wa afya wamekimbia, dawa ni haba, na huduma za chanjo zimevurugika, hali inayochochea milipuko ya magonjwa kama surua na malaria.

Inakadiriwa kuwa mwaka 2026, takribani watu milioni 4.2 nchini Sudan watakumbwa na utapiamlo mkali, wakiwemo watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha ambapo zaidi ya 825,000 watakuwa katika hali mbaya zaidi.

© UNOCHA/Giles Clarke Halima, mwenye umri wa miaka 30, aliyekimbia mapigano katika mji wa El Fasher uliopo karibu, anabeba bintiye Samira, mwenye umri wa miezi sita, ambaye ana sindromu ya Down na alitibiwa hivi karibuni kutokana na utapiamlo huko Tawila.

Changamoto za maji safi

Huduma za maji, usafi na mazingira (WASH) zimeathirika vibaya imesema UNICEF. Katika makambi ya Tawila, familia nyingi hazipati maji ya kutosha kwa mahitaji ya kila siku. 

Zaidi ya nusu ya wakazi wanapata chini ya kiwango cha chini kinachohitajika kwa Maisha takribani lita 8 hadi 9 kwa mtu kwa siku kinachotosha kunywa na kupika pekee, bila nafasi ya usafi wa mwili.

Hata kabla ya vita, Sudan ilikuwa na changamoto kubwa ya elimu, ambapo takribani watoto milioni 7 hawakuwa shuleni. Tangu Aprili 2023, elimu rasmi katika sehemu kubwa ya Darfur imesimama. Kati ya watoto milioni 3.9 wenye umri wa kwenda shule, milioni 3.3 hawapo shuleni.

Shule nyingi zimefungwa au kubadilishwa kuwa makazi ya wakimbizi. Walimu wamekimbia au hawalipwi, na wazazi wana hofu ya usalama wa watoto wao. Vijana waliokosa elimu wako katika hatari kubwa ya kujiunga na makundi yenye silaha au kunyanyaswa.

UNICEF inasaidia vipi?

UNICEF kwa kushirikiana na washirika wake inaendelea kutoa huduma muhimu kama afya, lishe, elimu na ulinzi wa watoto, ikiwa ni pamoja na maeneo salama ya watoto. Hata hivyo, misaada mara nyingi hukwama kutokana na ukosefu wa usalama, vikwazo vya kiutawala na mapigano yanayoendelea.

UNICEF imesisitiza kuwa njia za misaada ya kibinadamu zinapaswa kufunguliwa na kubaki wazi, na harakati za misaada kuwezeshwa badala ya kuzuiwa. Raia pamoja na miundombinu muhimu ya kiraia,ikiwemo shule, vituo vya afya na mifumo ya maji lazima zilindwe dhidi ya mashambulizi. 

Watoto waliotenganishwa na familia zao wanapaswa kutafutwa na kuunganishwa tena, manusura wa unyanyasaji wa kijinsia wapewe msaada unaostahili, na ukiukwaji wote mkubwa wa haki za watoto ukomeshwe mara moja.

Aidha, hatua zinahitaji ufadhili unaolingana na ukubwa na uharaka wa mahitaji yaliyopo. Ufadhili unaonyumbulika na wa muda mrefu unaweza kusaidia kuendeleza huduma muhimu za lishe, afya, maji, elimu na ulinzi, na hivyo kuzuia mifumo ambayo tayari ni dhaifu isiporomoke. Mafuta, chanjo na maeneo ya muda ya kujifunzia si vitu vya ziada ni huduma za msingi za kuokoa maisha. Imesema UNICEF

© UNICEF/Mohammed Jamal Msaada ukigawanywa katika kambi ya wakimbizi ya Zam Zam mjini Tawila Darfur Kaskazini Sudan kwa watu waliofurushwa makwao

Hakuna nafasi ya kukata tamaa

Tahadhari hiyo imesema watoto wa Darfur wanaishi katika mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu na ulinzi duniani. Miaka 20 baada ya dunia kupaza sauti kwa mara ya kwanza, wasichana na wavulana wamekwama tena katika mzunguko wa vurugu, njaa na hofu. Kizazi kingine cha watoto sasa kinabeba gharama kubwa ya kushindwa kwa mara kwa mara kuzuia na kumaliza migogoro.

Hata hivyo, licha ya vijiji vilivyoteketezwa na makambi yenye msongamano mkubwa katika Darfur na Chad, watoto bado wanaonyesha uthabiti. Wanaota siku ambayo risasi zitanyamaza, madarasa yatafunguliwa tena, urafiki utarejea, na usiku utapita bila hofu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *