
Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia fundi ujenzi, Salmin Rajabu (20) kwa tuhuma za kumuua mtoto wake, Sahiri Salmin mwenye umri wa miezi minane kwa kumchinja na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana usiku na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, tukio hilo limetokea jana Jumanne, Aprili 28, 2026, jioni katika eneo la Sinoni, jijini Arusha.
“Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wa miezi nane aliyemchinja shingoni na kumtenganisha kichwa na kiwiliwili. Uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya majirani kubaini tukio hilo, walikusanyika kwa lengo la kutaka kumshambulia mtuhumiwa, hata hivyo Jeshi la Polisi lilifika kwa haraka na kumchukua kwa ajili ya taratibu za kisheria.
Baadhi ya majirani wa mtuhumiwa wameeleza kushtushwa na tukio hilo na kuitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya ukatili wa aina hiyo.
Mkazi wa eneo hilo, Warda Adam amesema mama wa mtoto aliondoka nyumbani na kumuacha mwanawe akiwa na baba yake, lakini aliporudi na kutaka kufungua mlango, ulikuwa mgumu.
“Akiwa anarudi kutoka dukani, alijaribu kufungua mlango lakini mumewe alikataa kufungua. Ilibidi majirani waje kusaidia ndipo walipogundua tukio hilo la kusikitisha,” amesema Warda.
Mkazi mwingine, Jackson Motika amesema tukio hilo limewashtua wengi, akieleza kuwa ni vigumu kuamini mzazi anaweza kufanya kitendo hicho dhidi ya mtoto wake.
Naye Hassan Mollel amesema muda mfupi kabla ya tukio, walikuwa pamoja na mtuhumiwa na hakuonyesha dalili zozote zisizo za kawaida.
“Jana tulikuwa pamoja na hata nilimletea ndizi kwa ajili ya mtoto. Hakuonyesha mabadiliko yoyote ya kitabia,” amesema.
Kwa upande wake, Latifa Waziri amesema tukio hilo limeumiza hisia za wengi, akisisitiza umuhimu wa haki kutendeka na ukweli kubainishwa.
“Kitendo hiki kimeumiza sana. Tunaiomba Serikali ichunguze kwa kina ili ukweli ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.