Njombe. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe inakabiliwa na ukosefu wa mashine za kusafisha damu kwenye figo (dialysis), hali inayowalazimu wagonjwa kusafiri hadi mkoani Mbeya kufuata huduma hiyo muhimu.
Hali hiyo inaelezwa kuwaongezea mzigo wa gharama ambao wengi wanasema hawawezi kuzimudu.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Aprili 29, 2026, na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga, kwenye hafla ya kupokea vifaa vya hospitali na shule vilivyotolewa na Benki ya NMB, iliyofanyika hospitalini hapo.
Dk Mfanga amesema wananchi wa Njombe pamoja na wilaya jirani ya Songea, iliyoko mkoani Ruvuma, hulazimika kusafiri hadi mkoani Mbeya ili kupata huduma ya dialysis.
Kutokana na hali hiyo, Dk Mfanga amesema kuna haja kwa wadau kusaidia upatikanaji wa mashine hizo mkoani Njombe, itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za wananchi za kusafiriumbali mrefu kufuata huduma hiyo mkoani Mbeya.
Hata hivyo, ameishukuru Benki ya NMB na taasisi nyingine za kifedha zinazoendelea kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Nisisitize tu hasa kwenu ninyi wadau wetu, muelekeze pia nguvu katika ununuzi wa mashine za dialysis hapa kwenye Hospitali yetu ya Rufaa ya Njombe ili kuokoa maisha ya wananchi wengi wanaohitaji huduma hii,” amesema Dk Mfanga.
Amesema gharama za kusafisha damu kwenye figo ni kubwa na si kila mwananchi anayekumbwa na tatizo hilo anaweza kumudu gharama za usafiri na matibabu.
“Upatikanaji wa mashine hizi hapa mkoani utaleta unafuu mkubwa kwa wagonjwa,” amesema Dk Mfanga.
Amesema mgonjwa wa figo huhitaji kufanyiwa dialysis mara tatu kwa wiki, hali inayoongeza mzigo wa kifedha kwa wagonjwa na familia zao, hivyo kuhitajika msaada wa haraka kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa vifaa vya shule na hospitali vilivyotolewa na benki ya NMB.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ametoa wito kwa taasisi za kifedha nchini kusaidia upatikanaji wa mashine hizo badala ya kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.
Amesema taasisi za ndani zina uwezo wa kuchangia maendeleo ya sekta ya afya, hatua aliyosema inaweza kuongeza heshima na kuonesha juhudi za ndani katika kuboresha huduma za kijamii.
“Hatua iliyofanywa na benki hii ya NMB ni nzuri, lakini naamini mkichukua jukumu la kununua mashine za dialysis mtakuwa mmewagusa moja kwa moja wananchi, hasa wale wanaosafiri umbali mrefu hadi Mbeya,” amesema Mtaka.
Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Njombe, Nelasi Mulungu, ameishukuru benki hiyo kwa kutoa msaada wa madawati 400 kwa shule za msingi pamoja na viti na meza kwa shule za sekondari mkoani humo.
Hata hivyo, ameomba taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali kuboresha sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wagofya Mfalamagoha, amesema benki hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Amesema NMB imetoa Sh80 milioni kuchangia maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa yanayofanyika mkoani Njombe, pamoja na Sh120 milioni zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya shule na hospitali katika halmashauri za Mkoa wa Njombe.
Baadhi ya wananchi mkoani humo, akiwamo Benitho Chaula, amesema upatikanaji wa mashine za dialysis utapunguza gharama kubwa wanazokumbana nazo wanapokwenda kutafuta huduma hiyo mkoani Mbeya.
“Gharama ni kubwa sana kufuata huduma Mbeya, lakini tukipata mashine hapa Njombe itakuwa nafuu kwetu,” amesema Chaula.