Hiyo ni kwa mujibu wa makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA.

Shirika hilo linanukuu taarifa za Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC, (UNJHRO) inayoeleza kuwa katika eneo la Beni, jimboni Kivu Kaskazini, wanawake na wasichana wameathirika vibaya  na mashambulizi ya makundi yenye silaha dhidi ya raia.

Takwimu zinaonesha kuwa manusura 1,534 wa ukatili wa kijinsia walirekodiwa mwaka 2025, huku matukio ya utumwa wa kijinsia yakiripotiwa pia ingawa idadi halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kutokana na hofu na unyanyapaa.

Manusura wakikabiliwa na mateso makubwa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wengi wa manusura walipitia matukio ya kutekwa nyara, unyanyasaji wa muda mrefu na kutenganishwa na familia zao, hali inayowaacha na majeraha ya kimwili na kisaikolojia.

Miongoni mwao ni Maman Masika, ambaye alitekwa nyara mwezi Agosti baada ya kijiji chao kushambuliwa. Alifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa siku kadhaa kabla ya kufanikiwa kutoroka na kukimbilia usalama mjini Beni pamoja na familia yake.

Changamoto za huduma za dharura

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa saa 72 za kwanza baada ya tukio la unyanyasaji ni muhimu kwa matibabu ya kuzuia maambukizi ya VVU na mimba zisizotarajiwa. Hata hivyo, manusura wengi kama Masika hukosa huduma hizo kwa wakati kutokana na mazingira ya migogoro.

Alipofika Beni, Masika alipatiwa huduma katika hospitali ya rufaa, akipokea matibabu ya mwili pamoja na msaada wa kisaikolojia uliomsaidia kukabiliana na mshtuko, hofu na huzuni.

Safari ya uponyaji na kujijenga upya

Baada ya matibabu, Masika alianza hatua ya kujenga upya maisha yake. Kupitia msaada wa mfuko wa kitaifa wa fidia kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, alipata mafunzo ya ujasiriamali na mtaji wa kuanzisha biashara.

Licha ya changamoto, ikiwemo biashara yake kuvamiwa na kuporwa, aliendelea kusonga mbele na sasa anaendesha biashara ya kuuza vitambaa inayomsaidia kuhudumia familia yake.

Kurejesha heshima na matumaini

Leo hii, Masika anajiona kama mfanyabiashara na nguzo ya familia yake, akihakikisha wajukuu zake wanapata elimu na maisha bora.

Anasema sasa ana uwezo wa kupanga maisha yake ya baadaye na anaishi kwa matumaini mapya, akionesha uthabiti wa manusura wengi katika mazingira ya migogoro.

Wito wa kuimarisha msaada kwa manusura

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia.

Mashirika hayo yameonya kuwa bila msaada wa kutosha, manusura wengi wataendelea kukosa huduma muhimu zinazoweza kuwasaidia kurejesha maisha yao na heshima waliopoteza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *