YANGA na Simba baada ya kumalizana katika Kombe la Muungano pale Zanzibar, kituo kinachofuata ni jeshini kwenye Dimba la Meja Jenerali Isamuhyo ikiwa ni mchezo ya Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumapili hii Mei 3, 2026.

Ni mechi iliyobeba hisia za mashabiki wengi wa soka ndani na nje ya Tanzania, huku ikinogeshwa zaidi na taarifa za kwamba huenda waamuzi wakatokea Morocco. Kama ikiwa hivyo, itakuwa ni mara ya pili kushuhudia Kariakoo Dabi ndani ya Ligi Kuu Bara ikichezeshwa na waamuzi kutoka nje baada ya Juni 25, 2025, Wamisri kuiamua mechi ambayo Yanga ilishinda 2-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Mbali na hilo la waamuzi, kitendo cha mechi hiyo kupelekwa Meja Jenerali Isamuhyo, uwanja ambao Simba inautumia kwa mechi zake za nyumbani, imeibua hisia mpya.

Hata hivyo, matokeo ya fainali ya Kombe la Muungano, kwa namna moja ama nyingine yanaleta picha ya Kariakoo Dabi ijayo itakuwaje kwani aliyepoteza hatakubali kupoteza kwa mara nyingine.

Ukiangalia rekodi zilivyo, kabla ya Yanga na Simba kukutana katika fainali ya Kombe la Muungano iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, timu hizo zilitoka 0-0 mara ya mwisho kucheza uwanjani hapo ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara iliyofanyika Machi Mosi mwaka huu.

Kabla ya hapo, Yanga iliifunga Simba mara sita mfululizo katika mechi za mashindano tofauti ambapo Ligi Kuu Bara nne na Ngao ya Jamii mbili. Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga ilikuwa Agosti 13, 2023 katika Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1.

Mechi hii ya Jumapili, inazifanya Simba na Yanga kuingia kwa tahadhari kubwa ikizingatiwa kwamba hivi sasa zinatajwa kuwa ndiyo timu shindani zaidi katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ukiangalia msimamo wa ligi ulivyo kwa sasa, Yanga inaongoza kwa pointi 47, inafuatia Simba (42), kisha Azam (37). Kutoka nafasi ya tatu hadi kuifikia ya nne, tofauti ni pointi nane ambayo ni Singida Black Stars na JKT Tanzania zote zikiwa na 29.

JKT Tanzania iliyokuwa kileleni kwa muda mrefu wakati ambao kulikuwa na viporo vingi vya Yanga, Simba, Azam na Singida, imeanza kushuka chini taratibu, suala la kurudi tena kileleni inaweza kuwa miujiza.

Ligi hiyo raundi ya 20 ambayo inarejea leo baada ya kusimama kwa takribani wiki mbili kupisha michua-no ya Kombe la Muungano, kuna mechi 11 za hesabu kali ambazo Simba na Yanga inazitolea macho, huku zikianza na Kariakoo Dabi.

Yanga katika mechi 11 zilizobaki, itacheza dhidi ya Simba (ugenini), KMC (ugenini), Coastal (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani), Namungo (nyumbani), Mashujaa (ugenini), Fountain Gate (ugenini), Azam (nyumbani), TRA United (nyumbani) na JKT Tanzania (ugenini).

Kwa upande wa Simba, itacheza dhidi ya Yanga (0-0), JKT Tanzania (2-1 nyumbani), Tanzania Prisons (2-0), Mashujaa (2-0), Coastal Union (2-0), Dodoma Jiji (0-0), Pamba Jiji (1-1), Mbeya City (3-0), Mtibwa Sugar (1-1), Singida Black Stars (2-1) na KMC (2-0). Ukiangalia takwimu za msimu huu, Yanga ilipokutana na wapinzani wake hao 11 waliobaki, waliambulia kukusanya pointi 27 kati ya 33, baada ya kushinda nane dhidi ya dhidi ya KMC (4-1), Coastal (1-0), Dodoma Jiji (3-1), Singida Black Stars (3-0), Namungo (1-0), Mashujaa (6-0), Fountain Gate (2-0), na JKT Tanzania (5-0). Sare zikiwa tatu zote bila ya mabao dhidi ya Simba, Azam na TRA United.

Simba matokeo dhidi ya wapinzani wake waliobaki, walikusanya pointi 25, hiyo ilitokana na kushinda mechi saba dhidi ya JKT Tanzania (2-1), Tanzania Prisons (2-0), Mashujaa (2-0), Coastal Union (2-0), Mbeya City (3-0), Singida Black Stars (2-1) na KMC (2-0), huku sare zikiwa nne dhidi ya Yanga (0-0), Do-doma Jiji (0-0), Pamba Jiji (1-1) na Mtibwa Sugar (1-1).

Hivyo basi, Kariakoo Dabi ya Jumapili hii, Simba ina uhitaji mkubwa wa kushinda ili kurudisha heshima yake mbele ya Yanga, lakini pia kupunguza gepu la pointi kutoka tano la sasa hadi mbili ili kuisogelea nafasi ya kwanza.

Simba haijachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo ambapo Yanga imeendelea kutawala, hivyo umuhimu wa ushindi kwao ni mkubwa zaidi. Hata hivyo, Yanga nayo ina umuhimu wa kusaka ushindi wa mechi hii kwani inahitaji kutanua wigo la pointi dhidi ya mtani wake huyo wa jadi na kuusogelea ubingwa, pia kuendeleza ubabe wake kwa Simba. Hii itakuwa Kariakoo Dabi ya tatu ku-wakutanisha Steve Barker wa Simba na Pedro Goncalves wa Yanga tangu wakabidhiwe mikoba ya kuviongoza vikosi hivyo.

Pedro aliyetambulishwa Oktoba 25, 2025 kuchukua nafasi ya Romain Folz, huku Barker akitambulishwa Desemba 19, 2025 akimrithi Dimitar Pantev, walikutana kwa mara ya kwanza Machi Mosi 2026 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika bila ya kufungana, kisha jana wakakutana tena katika fainali ya Kombe la Muungano ambapo ilihitaji lazima mshindi apatikane, hivyo mechi ya tatu haitakuwa rahisi kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *