
Juhudi za kutokomeza homa ya ini ya B na C inayoambukizwa kwa virusi (Hepatitis B na C) zinaanza kuzaa matunda, huku mamilioni ya maambukizi na vifo vikizuiwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO.
Taarifa ya WHO iliyotolewa Bangkok, Thailand na New York, Marekani Aprili 28 imesema ripoti hiyo imetolewa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Homa ya Ini ulioanza tarehe 28 Aprili huko Bangkok, Thailand na utamalizika kesho Aprili 30, ikionya kuwa mafanikio hayo ya kuzuia maambukizi hayajasambaa kwa usawa—na yanaenda kwa kasi ndogo mno—kuweza kukidhi malengo yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2030.
Malengo ya 2030 ni kupunguza maambukizi mapya ya kwa asilimia 90 hadi 520,000 na vifo vitokanavyo na homa ya ini kwa asilimia vipungue hadi 450,000, hii ikiwa ni sawa na asilimia 65 ikilinganishwa na mwaka 2015.
Ikimulika mwenendo unaotia moyo pamoja na changamoto zinazoendelea katika kukabiliana na homa ya ini aina ya B na C, ambazo kwa pamoja husababisha asilimia 95 ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo duniani, ripoti inataja dalili za mafanikio
Dalili za Mafanikio: Maambukizi mapya yamepungua miongoni mwa watoto
Tangu mwaka 2015, juhudi za kimataifa zimeleta mafanikio yanayopimika ambapo maambukizi mapya ya homa ya ini B yamepungua kwa asilimia 32, huku vifo vinavyotokana na homa ya ini C vikishuka kwa asilimia 12.
Miongoni mwa watoto wadogo, kiwango cha maambukizi ya homa ya ini B kimeshuka hadi asilimia 0.6, huku nchi 85 tayari zikiwa zimefikia au kuvuka lengo la mwaka 2030.
Mafanikio haya yanahusishwa kwa kiasi kikubwa na upanuzi wa chanjo, maboresho ya matibabu, na juhudi za pamoja za kimataifa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Afya duniani mwaka 2016.
Baadhi ya nchi zimejitokeza kama mifano ya mafanikio ya uwekezaji endelevu na dhamira ya kisiasa nazo ni Misri, Georgia, Rwanda, na Uingereza ambapo zimepiga hatua kubwa kwa kupanua upimaji, kujumuisha matibabu katika huduma za afya za msingi, na kuongeza upatikanaji wa dawa za kuokoa maisha.
Wataalamu wanasema mafanikio haya yanaonesha kuwa kwa kutumia mikakati sahihi, inawezekana kutokomeza homa ya ini kama tishio la afya ya umma.
Mzigo unaoendelea duniani
Licha ya mafanikio hayo, homa ya ini inaendelea kuua watu kwa kiwango cha kutisha. Mwaka 2024 pekee, watu milioni 1.34 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na homa ya ini, huku maambukizi mapya milioni 1.8 yakiripotiwa—sawa na takriban wagonjwa wapaya 4,900 kila siku.
Inakadiriwa kuwa watu milioni 287 wanaishi na maambukizi sugu ya homa ya ini B na C wengi wao bila kutambuliwa au kutibiwa.
Mzigo huu maambukizi mapya haujasambazwa kwa usawa kwani Kanda ya WHO Afrika ilichangia asilimia 6
8 ya maambukizi mapya ya homa ya ini B, lakini ni asilimia 17 tu ya watoto wachanga waliopokea chanjo muhimu ya dozi ya wanapozaliwa.
Wakati huo huo, upatikanaji wa matibabu bado ni mdogo sana—chini ya asilimia 5 ya watu wenye homa ya ini aina B sugu wanapata matibabu.
Hepatitis C pia inaendelea kusambaa, hasa miongoni mwa watu wanaotumia dawa za kulevya kwa sindano, ambao wanachangia asilimia 44 ya maambukizi mapya duniani. Ingawa tiba zenye ufanisi mkubwa zipo, ni takriban asilimia 20 tu ya walioambukizwa wamepata matibabu tangu mwaka 2015.
Idadi ndogo ya nchi hubeba sehemu kubwa ya mzigo wa ugonjwa huu duniani. Nchi 10—ikiwemo China, India, Nigeria, na Afrika Kusini—zinachangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na homa ya ini duniani.
Kwa nini maendeleo hayako sawa
Wataalamu wa afya wanabainisha sababu kadhaa zinazosababisha kuchelewa kwa maendeleo, ikiwa ni pamoja na mifumo dhaifu ya afya, uhaba wa fedha, unyanyapaa unaohusiana na ugonjwa huu, na ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za upimaji na matibabu.
Watu wengi hawajui hali yao ya maambukizi, huku wengine wakikosa huduma nafuu za matibabu. Katika baadhi ya maeneo, hatua za msingi za kinga—kama matumizi salama ya sindano na chanjo za mapema—bado hazijatekelezwa kikamilifu.
Nini kifanyike
Ripoti inaeleza wazi kuwa zana za kutokomeza homa ya ini tayari zipo, lakini zinahitaji kupanuliwa kwa haraka na kwa usawa.
Vipaumbele vikuu ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa chanjo ya hepatitis B—hasa dozi ya kuzaliwa katika maeneo yenye mzigo mkubwa—pamoja na kuongeza upatikanaji wa matibabu kwa maambukizi sugu. Pia, kuingiza huduma za hepatitis katika huduma za afya za msingi ni muhimu ili kuwafikia watu waliotengwa.
Kuboresha usalama wa matumizi ya sindano na kuimarisha huduma za kupunguza madhara kwa watu wanaotumia dawa za kulevya kwa sindano ni hatua muhimu za kudhibiti maambukizi ya hepatitis C. Wakati huo huo, serikali zinahimizwa kuongeza uwekezaji katika mifumo ya afya na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za ndani.
Wataalamu pia wanasisitiza umuhimu wa kupambana na unyanyapaa na kuongeza uelewa, kwani haya bado ni vikwazo vikubwa kwa upimaji na matibabu.
Njia kuelekea 2030
Ingawa mafanikio ya hivi karibuni yanatoa matumaini, ripoti inaweka wazi kuwa juhudi za sasa hazitoshi kufikia malengo ya kimataifa ya mwaka 2030. Bila kuongeza kasi na uratibu wa hatua, mamilioni ya maambukizi na vifo vinavyoweza kuzuilika vinaweza kuendelea kutokea.
Uzoefu wa nchi zilizopiga hatua unaonyesha kuwa mafanikio yanawezekana—lakini tu ikiwa yatapanuliwa kwa usawa zaidi katika maeneo yote.
Kuziba pengo hili, viongozi wa afya wanasema, kutakuwa muhimu katika kubadili ndoto ya kutokomeza hepatitis kuwa uhalisia wa kimataifa.