Dar es Salaam. Kifo cha msanii mkongwe wa filamu nchini, Hashim Kambi, kimeacha simanzi nzito kwa familia, wasanii na mashabiki wa tasnia ya burudani.

Kambi alifariki dunia ghafla, Jumatatu ya Aprili 27, 2026, Dar es Salaam, na mwili wake umezikwa jana Jumanne katika makaburi ya Kisutu jijini humo.

Katika mahojiano na Mwananchi, msemaji wa familia, Mwita Abubakari Kambi, ambaye ni mdogo wa marehemu, amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo dakika za mwisho za maisha ya ndugu yake sambamba na historia yake.

Mwita anasema siku ya umauti wake ilianza kama siku ya kawaida, bila dalili yoyote kubwa ya hatari, lakini mwisho wa siku ikajawa na huzuni.

“Hashim alifika Dar es Salaam leo (Jumatatu, Aprili 27, 2026) asubuhi akitokea Tabora. Alipofika nyumbani hakupata hata muda wa kupumzika, akaanza kukimbilia majukumu yake ya sanaa. Ukweli ni kwamba alikuwa na presha, alitakiwa kupumzika, lakini akaamua kuwahi kazi,” anaeleza Mwita.

Anasema kuwa akiwa katika harakati hizo za kikazi pamoja na wenzake, ndipo tukio la kushtua lilipotokea.

“Ghafla, wenzake wakamuona anaanguka. Ilikuwa ni hali ya kushitukiza sana, kwa haraka huwezi kusema sababu halisi, kwa sababu hakuwa amelazwa hospitalini wala kuonesha dalili kubwa kabla. Inaonekana ni uchovu na presha,” anasema.

Kwa mujibu wa Mwita, juhudi za kumuwahisha hospitalini hazikuzaa matunda.

“Wakati wanamkimbiza hospitali tayari alikuwa ameshafariki pale pale alipoanguka. Walimbeba kumpeleka Hospitali ya Mico iliyopo Sinza, lakini ukweli ni kwamba alikuwa tayari ameshapoteza maisha,” anasema.

Nguli huyo enzi za uhai wake ameigiza filamu kama Simu ya Kifo, Kipusa, The Lost Twins, Kipuri, Zuadiswa, Honey Moon, Surprise, Ripple of Tears, Miss Call, Romance, 20%, Furaha Iko Wapi, The Passion na Damu ya Mjomba.

Soka hadi sanaa

Mbali na sanaa ya filamu, Kambi alikuwa na historia kubwa katika michezo, hasa soka.

“Alizaliwa Morogoro na kusomea huko huko. Kabla ya kuingia kwenye filamu, alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu katika timu ya Jogoo ya Morogoro.

“Baadaye akachukuliwa na timu ya Yanga, akicheza nafasi ya beki namba tano pamoja na kina Selemani Jongo,” anasimulia Mwita.

Anaendelea:“Alicheza Yanga kuanzia mwaka 1978 hadi 1980. Mimi ndiye niliyemleta Dar es Salaam mwaka 1977, akawa anaishi Magomeni kwa baba yangu ambaye yeye anamuita baba mdogo.”

Kwa mujibu wa familia, baada ya kuacha soka, alijishughulisha na masuala mengine kabla ya mwaka 2003 kuingia rasmi katika kiwanda cha filamu.

Enzi za uhai wake, katika mahojiano yake na Mwananchi alipokuwa akielezea safari yake kwenye sanaa, Kambi hakuwahi kusita kumtaja Richie Richie (Single Mtambalike) kama mtu aliyemuingiza kwenye sanaa hiyo, hivyo ni mtu anayemheshimu na kumuona kama baba yake.

Kambi alisema siku moja akiwa katika shughuli zake za biashara alikutana na msanii huyo na kumueleza namna anavyopenda kuigiza.

“Nilimueleza Richie namna nilivyokuwa nikivutiwa na uigizaji wake na ule wa kina Natasha na Jacob Steven kwenye tamthiliya ya ‘Mambo Hayo’, hivyo nikamuomba kama naweza kupata nafasi ya kuigiza.

“Richie kwa kuwa tulijuana kwenye mashabiki wa timu ya Yanga, nilipomwambia hivyo ilikuwa rahisi, na hapo ndipo akampigia simu Baba Haji na kumueleza kuwa wamepata mtu wa kucheza nafasi ya Benjamini katika tamthiliya ya ‘Uhondo wa Ngoma’,” alisema.

Tamthiliya hiyo ilikuwa ikiigizwa na wasanii kutoka kundi la maigizo la Kamanda Arts Family chini ya uongozi wa Haji Adam maarufu ‘Baba Haji’, na kurushwa katika kituo cha TVT enzi hizo, ambapo kwa sasa inajulikana kama Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Humo nilipewa nafasi ya kucheza kama Mzee Benjamin aliyekuwa tajiri katika hadithi ya tamthiliya hiyo, na kujikuta nakuwa maarufu na kupata kazi nyingi za filamu.

“Ni kutokana na Richie kunifungulia njia huko mpaka sasa hivi nimeweza kuwa msanii mkubwa na ninayeheshimika. Namshukuru kwa hilo, kwani huwa namuita baba yangu wa sanaa,” aliwahi kusema Hashim Kambi enzi za uhai wake.

Familia na maisha binafsi

Katika maisha yake, marehemu ameacha watoto watatu, huku akiwa ameoa mara tatu.

“Alioa mke wa kwanza hapa Dar es Salaam na kupata watoto wawili, Shamimu na Mohamed. Baadaye mwaka 1989 nikamuozesha mke wa pili Arusha, wakapata mtoto mmoja, Lulu. Walikuja kuachana na huyo mkewe, akakaa muda mrefu bila mke, kisha mwaka 2022 nikamuozesha tena mke wake wa sasa, ingawa hawakupata mtoto,” anasimulia Mwita.

Pengo aliloacha

Mwita anamkumbuka kaka yake kama mtu wa watu na mwenye upendo mkubwa kwa jamii.

“Hashim alikuwa mtu wa watu, mcheshi na aliyependa kujichanganya na kila mtu. Alikuwa hana makuu kabisa,” anasema na kueleza kuwa pengo aliloacha ni kubwa kwa familia.

“Yeye ndiye alikuwa mkubwa wetu, hivyo kuondoka kwake ni pengo kubwa sana ambalo si rahisi kuziba,” anasema Mwita.

Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Eliya Mjatta, naye anasema:“Kambi atakumbukwa kwa uhodari wake wa kazi na kuibua vipaji vya watu wengine zaidi. Mchango wake utaendelea kuishi.”

Watu mbalimbali wametoa salamu za rambirambi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan aliyeeleza kupokea kwa masikitiko

taarifa ya kifo cha mwigizaji huyo na kwamba Taifa limepoteza kipaji adhimu kilichochangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuitangaza tasnia ya filamu nchini.

“Ninatoa pole kwa Shirikisho la Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), wasanii wa filamu nchini, familia ya marehemu, wadau wa filamu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu.”

Kwa upande wake, klabu ya Yanga imetoa taarifa ikisema umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa mchezaji wao wa Hashim Kambi.

“Tunatoa pole za dhati kwa familia ya marehemu, Baraza la Sanaa la Tanzania (Basata), wadau wa mpira wa miguu, Shirikisho la Filamu Tanzania, wasanii wa filamu, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu,” inaeleza taarifa hiyo.

Kwa nini kuzikwa Dar

Mazishi ya mkongwe huyo wa sanaa yalifanyika jana kwenye makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, na familia imeeleza sababu ya kumzika Dar badala ya Morogoro alipozaliwa.

“Baba yetu mzazi alifariki mwaka 1995 na alizikwa Magomeni, Dar es Salaam. Hata marehemu mwenyewe alikuwa na msimamo kuwa akifa azikwe hapa hapa Dar, hivyo tumefuata wosia wake,” anafafanua Mwita.

Katika kipindi hiki kigumu, Mwita anasema familia imefarijika na ushirikiano kutoka kwa wasanii.

“Tunashirikiana vizuri sana na wasanii katika maandalizi yote ya mazishi. Wamekuwa bega kwa bega nasi tangu mwanzo,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *