Baada ya kupita takribani miezi miwili tangu Marekani na utawala wa kizayuni zilipoanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran, wakosoaji wa sera za kushupalia vita za Trump katika kila pembe ya dunia wanaendelea kukiri na kutamka kwa uwazi zaidi kwamba Marekani imeshindwa katika vita hivyo.

Kansela Friedrich Mertz wa Ujerumani, ametoa kauli mpya kuhusu uvamizi wa kijeshi uliofanywa na utawala wa kizayuni na Marekani dhidi ya Iran akisema: “Wairan wameonekana dhahiri kwamba wana nguvu zaidi ya ilivyofikiriwa.”
Mertz ameongeza kuwa, licha ya kuendelea kuwepo mivutano, Wairan “wanafanya mazungumzo kwa umahiri wa hali ya juu”. Lakini mbali na hayo, Kansela wa Ujerumani ametamka kinagaubaga kwamba, hivi sasa Marekani inadhalilishwa na uongozi wa Iran. 
Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Juni mwaka jana, wakati kansela huyo wa Ujerumani alipoziunga mkono Israel na Marekani katika vita vya siku 12 zilivyoanzisha dhidi ya Iran, alitamka hivi, kuhusu jinai za utawala wa kizayuni: “Wao (akimaanisha Israel) wamefanya kazi hii ngumu na chafu kwa niaba yetu sote.” Matamshi hayo ya kibaguzi aliyotoa Mertz kuunga mkono uvamizi uliofanywa na Wazayuni na Marekani dhidi ya Iran yalikabiliwa na mijibizo mikali na hasi mno ndani ya Ujerumani na katika duru za kisiasa na za vyombo vya habari. Kumsikia hivi sasa kansela huyo wa Ujerumani na baada ya kupita karibu miezi miwili akiungama hadharani kuhusu nguvu na uwezo wa kijeshi wa Iran kunaashiria ukweli usioweza kukanushika. 
Kilichomfanya Mertz alazimike kukiri hivyo ni wasiwasi alionao wa kuhatarishwa maslahi na usalama wa Ulaya na matokeo hasi kimataifa yatakayosababishwa na uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Wazayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 
Nchi za Ulaya hazina vyanzo endelevu vya kujidhaminia nishati; kwa sababu hiyo zinaathirika kirahisi kutokana na mtikisiko wowote unaotokea katika soko la nishati. Mtikisiko mdogo kabisa katika soko hilo umekuwa na athari kwenye mnyororo wa uzalishaji na wa matumizi ya nishati, na kusababisha mfumuko wa bei na mdororo wa uchumi. Wazungu, na hasa Wajerumani wanamjua vizuri Trump; na licha ya uadui wao dhidi ya wananchi na serikali ya Iran, wanaelewa fika kwamba kuendelea kwa sera za kushupalia na kuwasha moto wa vita za Trump katika eneo la Asia Magharibi hakutakuwa na tija nyingine yoyote isipokuwa kuendelea kuyumbisha soko la nishati na mnyororo wa uzalishaji katika kilimo na sekta nyingi za viwanda.

Viongozi wa nchi washirika wa Marekani barani Ulaya wamekiri kushindwa Marekani katika vita dhidi ya Iran sambamba na kutaka zitumike njia za kidiplomasia kuhitimisha vita hivyo, huku wakiwa wanaihitajia Marekani kwa ajili ya vita vyao na Russia huko Ukraine. Lakini pamoja na hayo, hali halisi ilivyo katika medani inawafanya wachukue hadhari ya kutomuunga mkono Trump. Hakuna nchi hata moja ya Ulaya ambayo imeunga mkono sera za Trump na Netanyahu za kuwasha moto wa vita dhidi ya Iran. Serikali za Ulaya ama zimeamua kunyamaza kimya, au kupinga wito wa Trump wa kuzitaka zishiriki katika vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Moja ya nchi zilizopinga waziwazi uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni Uhispania.
“Hakuna suluhisho lolote la kijeshi kwa mgogoro uliopo kati ya Marekani na Iran”, ndivyo alivyotamka Waziri wa Mambo ya nje wa Uhispania José Manuel Álvarez wakati wa ziara yake nchini Puerto Rico, na akaongezea kwa kusema: “na ninataka niwakumbushe watu wote kwamba, huu ndio mgogoro mkubwa zaidi duniani kwa karne hii, ambao una taathira za kiuchumi kwa ulimwengu.” 
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez, yeye tangu mwanzo wa vita amekuwa akipaza sauti ya “hapana kwa vita”. Hata hivi karibuni, Sánchez ametamka kuwa vita vya Marekani na Wazayuni katika Asia Magharibi ni “vibaya zaidi” mara kadhaa kuliko vita vya Iraq vya mwaka 2003 na ni “maafa hasa”; na kwamba utawala wa Israel unataka kuyarudia tena huko Lebanon “maangamizi” yale yale uliyosababisha huko Ghaza.
Alipohutubia kikao cha hadhara cha bunge, na katika kutetea msimamo wa serikali yake wa “hapana kwa vita” waziri mkuu huyo wa Uhispania aliuliza suali la ukosoaji na kuutoa maanani uvamizi haramu na usio na mashiko ulioanzishwa dhidi ya Iran akihoji: “Na yote haya, ni kwa ajili ya nini?”; “ni kwa ajili ya kudhoofisha sheria za kimataifa, kuiyumbisha Mashariki ya Kati, kuwasha tena moto wa mapigano Iraq na Lebanon, na kuizika Ghaza chini ya vifusi vya kusahauliwa na kutojaliwa.” 
Pedro Sánchez, alikwenda mbali zaidi kwa kukumbusha kwamba, mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yalianza wakati Washington “ilikuwa nao mkononi mwake” mkataba wa makubaliano ya nyuklia na Iran, lakini ikaukataa “bila kutoa maelezo, bila kuwajulisha washirika, bila ya kuwa na msukumo wa kisheria, na bila ya kuwa na lengo maalumu”. Huko ndani ya Marekani kwenyewe, kushindwa kwa Trump katika vita dhidi ya Iran kunabainishwa na kuungamwa kwa uwazi zaidi.
Jeffrey Sachs, Profesa wa Chuo Kikuu cha Columbia katika Jiji la New York, amesema  katika mahojiano: “Iran imeonyesha kuwa ina nguvu muhimu sana ya kuzuia hujuma na yenye sauti ya mwisho, ina wenzo wa mashinikizo na hairudi nyuma kirahisi kwa sababu ya vitisho.” Mhadhiri huyo mtajika wa Chuo Kikuu cha Columbia amelaani vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa kizayuni dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa malengo ya vita hivyo hayawezekani kufikiwa. Na akaonya pia kwamba, kuendelea kwake, kutauvuruga uchumi wa Marekani na dunia na kuutaja utawala wa Kizayuni kuwa ni “utawala wa kifashisti.” Jeffrey Sachs ameongezea kwa kusema: “Imethibitika kwamba, badala ya kupelekea kupatikana amani na usalama, vituo vya kijeshi vya Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni chanzo kikuu cha matatizo na migogoro. Ninavyoamini mimi, kambi hizo hazitarudi tena kwenye hali yake ya zamani. Na tafsiri yangu kuhusiana na hali hii, ni kuwepo ishara isiyo na shaka, ya kuwa na mipaka nguvu na uwezo wa Marekani”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *