
Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Kisiasa la harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza msimamo wa msingi wa harakati hiyo kuhusu uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa Muqawama na mapambano yataendelea hadi ardhi yote ya nchi hiyo itakapokombolewa kikamilifu.
Mahmoud Qomati, Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah, amesema katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera kuwa hakutakuwa na mazungumzo yoyote yasiyo ya moja kwa moja na Israel bila usitishaji wa mapigano kamili na wa vita wa pande zote.
Afisa huyo amesisitiza kuwa operesheni za Muqawama zinaendelea na kueleza kuwa mapambano yataendelea hadi kila shibri ya ardhi ya Lebanon itakapokombolewa kutoka mikononi mwa adui.
Aidha ameunga mkono msimamo thabiti wa Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, na kupinga mazungumzo yoyote ya moja kwa moja na adui Mzayuni, akisema msimamo huo hauwezi kuvukwa.
Mwishoni, Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah ameonya kwamba subira ya Muqawama na Hizbullah mbele ya uhalifu wa Israel si ya milele, na akasisitiza kwamba msimamo huu wa kusimama kidete unaendelea kwa njia ya kujitegemea na hauna mfungamano na mzozo kati ya Israel na Iran.